Tafuta

Baraza la Maaskofu Kenya, KCCB, linawaalika waamini na watu wote wa Mungu nchini Kenya katika ujumla wao, kusali kwa ajili ya kuombea amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Baraza la Maaskofu Kenya, KCCB, linawaalika waamini na watu wote wa Mungu nchini Kenya katika ujumla wao, kusali kwa ajili ya kuombea amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu.   (AFP or licensors)

Papa Francisko Siasa Safi Ni kwa Ajili ya Huduma: Uchaguzi Mkuu Nchini Kenya Agosti, 2022

Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo cha huduma. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha, utu na haki msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Changamoto za siasa safi! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anasema amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini ikitumiwa vibaya inaweza kuwa ni chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA katika ujumbe wake kwa watu wa Mungu Afrika Mashariki na Kati, inaiombea Kenya ili uchaguzi wake tarehe 9 Agosti uweze kuwa huru, haki na kweli ili amani iweze kutawala nchini Kenya kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu tarehe 9 Agosti 2022. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Kenya, KCCB, linawaalika waamini na watu wote wa Mungu nchini Kenya katika ujumla wao, kusali kwa ajili ya kuombea amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Siasa safi ni kwa ajili ya huduma ya watu wa Mungu
Siasa safi ni kwa ajili ya huduma ya watu wa Mungu

Baba Mtakatifu anasema siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri!

Umoja, upendo na mshikamano wa kweli.
Umoja, upendo na mshikamano wa kweli.

Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbali mbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. Siasa safi ni chombo cha huduma ya amani inayosimikwa katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa vizazi kuheshimiana na kuthaminiana. Vilema vya wanasiasa vinajionesha katika maisha ya hadhara, kwenye taasisi wanazohudumia pamoja na utunzaji bora wa mazingira; mambo yanayoweza kuwafanya watu kumwamini mwanasiasa, katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati yake kama kielelezo cha demokrasia. Vinginevyo, wanasiasa wanaoelemewa na vilema vyao ni hatari sana katika kujenga na kukuza demokrasia jamii. Hawa ni watu ambao “wamepekenywa” kwa rushwa na ufisadi; watu wasioheshimu wala kujali utawala wa sheria; ni watu wenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka; ni wachochezi wa ubaguzi na hofu miongoni mwa jamii wala utunzaji bora wa mazingira kwao si kipaumbele, lakini matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi. Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

AMECEA: Uchaguzi uwe: huru, haki na kweli ili amani iweze kutawala tena
AMECEA: Uchaguzi uwe: huru, haki na kweli ili amani iweze kutawala tena

Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza”. Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Matumizi ya nguvu ni kinyume cha kanuni maadili inayopania suluhu ya amani na utulivu. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotumia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni mbinu mkakati wa kujijenga kisiasa kwa kuwashutumu wakimbizi na wahamiaji kuwa ni sababu ya umaskini na majanga yanayowaandama watu wao. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni ushuhuda wa urithi wa utajiri wa kimaadili kizazi baada ya kizazi! Watoto wanaoishi katika maeneo ya vita, vurugu na kinzani wanapaswa kulindwa na haki zao msingi na utu wao kuheshimiwa na kamwe wasipelekwe mstari wa mbele kama chambo cha vita kwani wao ndio leo na kesho ya binadamu!

Uchaguzi Kenya
08 August 2022, 16:09