Tafuta

Papa Francisko: Msiogope Enyi Kundi Dogo! Kuweni Tayari!

Msiogope ni maneno ambayo Kristo Yesu anayatumia kuwatia wafuasi wake shime, akikazia: huruma, upendo na ukarimu unaobubujika kutoka kwa Mungu. Ukosefu wa imani, msongo wa magumu ya maisha, machungu na hofu ya kutofanikiwa katika malengo ni kati mambo yanayopelekea watu kujenga hofu na wasi wasi katika maisha na hivyo kukosa amani, utulivu na furaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Woga, hofu, mashaka na usingizi wa maisha ya kiroho ni hatari sana kwa waamini. Ndiyo maana Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, huku wakiendelea kukesha na kukita maisha yao katika sala, silaha madhubuti ya maisha ya kiroho. Mwenyezi Mungu anawataka waamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano thabiti pamoja naye kwa njia ya: Kusoma, kutafakari na hatimaye, kulinafsisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Ni mwaliko wa kusimika maisha katika Sakramenti za Kanisa zinazomtakatifuza mwamini, zinazojenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, na hatimaye, kumtolea Mwenyezi Mungu ibada, jambo la msingi ni imani thabiti kwa sababu Sakramenti zina nguvu kwa sababu Kristo Yesu mwenyewe anatenda kazi ndani yake! Kristo Yesu ili kuwaondolea wanafunzi wake hofu, mashaka na wasiwasi anawaalika kuiishi neema ya Mungu: kwa kutoogopa na daima wakiwa tayari. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Dominika ya 19 ya Mwaka C wa Kanisa, tarehe 7 Agosti 2022 amekazia mambo makuu mawili katika tafakari yake akisema: “Msiogope enyi kundi dogo” na pili “kuweni tayari.” Haya ni maneno muhimu sana katika mapambano ya maisha ya kiroho ili hatimaye kushinda hofu na majaribu.

Msiogope enyi kundi dogo, jiwekeni tayari
Msiogope enyi kundi dogo, jiwekeni tayari

Msiogope ni maneno ambayo Kristo Yesu anayatumia kuwatia wafuasi wake shime, akikazia: huruma, upendo na ukarimu unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, historia na hatima ya maisha ya mwanadamu viko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Ukosefu wa imani, msongo wa magumu ya maisha, machungu na hofu ya kutofanikiwa katika malengo ni kati mambo yanayopelekea watu kujenga hofu na wasi wasi katika maisha. Na matokeo yake ni watu kukosa amani, utulivu na furaha ya kweli. Ni hofu inayowafanya watu kuwa na uchu wa mali, ili kujihakikishia usalama wa maisha yao, lakini matokeo yake ni kutumbukia katika mahangaiko zaidi! Ndiyo maana Kristo Yesu anasema, “Msiogope.” Changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, licha ya kupata uhakika huu, hakuna sababu ya “kuuchapa usingizi wa maisha ya kiroho” na hatimaye, kujikuta umetumbukia katika “dimbwi” la uvivu, makazi ya Shetani, Ibilisi. Waamini wanapaswa kuwa macho, kwa kuwapenda na kuwathamini wengine; kwa kuguswa na mahitaji yao msingi, tayari kuwasikiliza na kujibu kilio chao cha ndani. Waamini wanaalikwa kuwa tayari katika hali yoyote ile ya maisha, kwa sababu hii hekima ya maisha ya Kikristo kama inavyofafanuliwa na Kristo Yesu katika mifano mitatu yaani: watumwa wanaokesha, mwenye nyumba anayelinda nyumba yake dhidi ya wezi na wavamizi na wakili mwaminifu.

Papa Jiwekeni tayari siku zote.
Papa Jiwekeni tayari siku zote.

Ujumbe mahususi ni kukesha, daima kuwa tayari na kamwe waamini wasielemewe na uvivu, kwani hata katika hali wasiyo tarajia Kristo Yesu atakuja tena katika utukufu wake kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, mwisho wa safari ya maisha yao hapa duniani, watatakiwa kutoa hesabu ya mali ambayo Mwenyezi Mungu amewakabidhi katika maisha. Ni katika muktadha huu, waamini wanahamasishwa kukesha na kuendelea kuwa macho, kwa kuwajibika; kwa kulinda na kusimamia mali, utajiri na mapaji aliyowakirimia kwa uaminifu mkubwa. Mwenyezi Mungu amewajalia zawadi ya maisha na imani; familia, mahusiano na mafungamano; ajira, lakini pia na maeneo wanamoishi: vijiji, miji na majiji wanamoishi, bila ya kusahau mazingira ambayo ni kazi ya uumbaji. Jambo msingi kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanalopaswa kujiuliza, Je, wamekuwa mstari wa mbele kutunza amana na urithi huu ambao Mwenyezi Mungu amewaachia? Je, wako imara kulinda na kudumisha uzuri wao au watu wanatumia mambo haya kwa mafao yao binafsi na urahisi wa maisha ya sasa?

Tunzeni mazingira nyumba ya wote kwa mafao na ustawi wa wengi
Tunzeni mazingira nyumba ya wote kwa mafao na ustawi wa wengi

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuenenda bila woga, wawe na uhakika kwamba, Kristo Yesu anawasindikiza katika hija ya maisha yao huku Bondeni kwenye machozi. Wanapaswa kukesha katika imani na kamwe wasipitiwe na usingizi wakati Kristo Yesu atakapokuwa anapita. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyethubutu kumkaribisha na kumpokea Mwana wa Mungu kwa nguvu na ukarimu mkuu, aliposema “Mimi hapa” awasaidie katika safari ya maisha yao.

Papa Francisko Msiogope

07 August 2022, 15:14

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >