Tafuta

Papa Francisko tarehe 23 Februari 2022 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee. Papa Francisko tarehe 23 Februari 2022 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee.  

Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee: Muhtasari Wake

Hii ni changamoto kwa wazee kuwa ni mfano bora wa unabii kwa vijana wa kizazi kipya katika maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wazee wanapaswa kuwa ni divai njema inayoleta faraja na furaha kwa vijana wa kizazi kipya; wawe ni wajumbe wa Habari Njema na wala si kinyume chake; waheshimiwe na kutunzwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tangu Jumatano tarehe 23 Februari 2022 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee. Alihimiza muungano thabiti kati ya umri na maisha, ili kutegemeana na kukamilishana katika hija ya maisha, bila ya wazee kuonekana kama mzigo kwa jamii na hivyo kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Wazee wanapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Anasema inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Wazee wana ndoto, na vijana wana maono. Rej. Yoe 3:1. Utu, heshima na haki msingi za wazee zinapaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kutambua kwamba, uzee ni amana, utajiri na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wazee wana hekima wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya, ili hata wao waweze kukua na kukomaa kwani wao wanayo mizizi ya historia ya watu wao ni kielelezo cha neema na baraka kwa jamii husika. Uzee kama rasilimali kwa vijana wasiokuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha. Hii ni changamoto kwa wazee kuwa ni mfano bora wa unabii kwa vijana wa kizazi kipya katika maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wazee wanapaswa kuwa ni divai njema inayoleta faraja na furaha kwa vijana wa kizazi kipya; wawe ni wajumbe wa Habari Njema na wala si kinyume chake. Wazee waheshimiwe na kuthaminiwa na jamii na kamwe wasibezwe na kutwezwa. Kwa hakika, ulimwengu unawahitaji vijana shupavu na wenye nguvu pamoja na wazee wenye hekima na busara katika maisha.

Mshikamano wa dhati kati ya marika ni muhimu kwa ajili ya Injili ya uhai.
Mshikamano wa dhati kati ya marika ni muhimu kwa ajili ya Injili ya uhai.

Mahusiano ya Kifamilia: Ruthu ni ishara ya mahusiano ya kifamilia yanayofumbatwa katika upendo; Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika ushuhuda wa tunu msingi za kifamilia, muungano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee; dhamana ya Naomi mkwewe Ruthu pamoja na wosia wa watu wa ndoa kuwaheshimu na kuwathamini wakwe zao katika uzee wao! Upendo na Uaminifu Machoni Pa Mungu. Leo hii kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu kuna haja ya kuwa na uzee unaosheheni hisia changamfu za kiroho zenye uwezo wa kutambua ishara za Mwenyezi Mungu. Hii ni Ishara ambayo inawapatia watu changamoto kwa sababu ni "ishara inayonenwa" (Lk 2:34), lakini ambayo inawajaza furaha, amani na utulivu wa ndani kutokana na huduma inayotolewa kwa Mungu na jirani. Uzee ni amana: Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu maana na thamani ya uzee amefafanua sehemu ya Maandiko Matakatifu kuhusu, Nyakati za Mwisho, kadiri ya Mafundisho ya Kristo Yesu, Uharibifu wa mazingira nyumba ya wote na kwamba Mzee Nuhu ni mfano bora wa kuigwa katika maadili na utu wema.

wazee na vijana wanapaswa kushikamana na kutegemezana.
wazee na vijana wanapaswa kushikamana na kutegemezana.

Rushwa, vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu kamwe yasiwe ni mambo ya kawaida hata kidogo, kiasi cha kuzoeleka na wengi. Maisha marefu: Ni alama na fursa ya kutafakari kuhusu maana ya maisha; Mwingiliano kati ya vijana na wazee; madhara ya janga la UVIKO-19 pamoja na maisha ya mwanadamu kuwa ni marefu. Sehemu ya Maandiko Matakatifu imebainisha kuhusu maisha marefu kadiri ya Maandiko Matakatfu ni kama njia ya kurithisha maisha ya mwanadamu mintarafu kazi ya Uumbaji. Huu ni mwanzo wa historia ya kazi ya uumbaji inayomtambua Mwenyezi Mungu kuwa ni chemchemi ya roho na maisha ya mwanadamu kwa kuwa na dhamiri hai pamoja na uhuru; mang’amuzi na uwajibikaji mpana. Maisha ya mwanadamu yanakita mizizi yake katika sura na mfano wa Mungu; udhaifu wake wa kibinadamu na hatimaye, kifo. Haya ni mambo msingi ambayo mwamini anapaswa kuyafahamu. Muda mrefu kiasi hiki unamwezesha mwanadamu kukuza na kuboresha maisha yake ya kiroho. Huu ni mwaliko wa kuangalia tena maana ya maisha na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza hasa katika zama hizi za utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Uzee kwa muhtasari
10 August 2022, 16:06