Papa Francisko atoa wito kuombea Nicaragua
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana Baba Mtakatifu Francisko akiwageuikia mahujaji na waamini waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 21 Agosti 2022 amezungumzia juu ya nchi ya Nikaragua na kuonesha wasi wasi mkubwa kwa kile kinachoendelea. Baba Mtakatifu Francisko amesema jinsi ambavyo anafuatilia kwa karibu na wasi wasi na uchungu wa hali ambayo imeundwa nchini humo ambayo inawahusisha watu na taasisi.
“ Ninapendelea kuonesha uaminifu wangu na matashi yangu kwamba kwa njia ya mazungumzo ya wazi na ukweli, inawezekana bado kupata misingi kwa ajili ya kuishi kwa kuheshimiana na amani. Tuombe Bwana kwa njia ya maombezi ya Msafi kabisa ambaye auhishwe katika mioyo uthabiti wa utashi huo”., amesema papa Francisko.
Baba Mtakatifu Francisko ametoa wito huo kutokana na kwamba katikati ya usiku, wa tarehe 18 Agosti 2022 vikosi vya polisi na mawakala wa kijeshi wa Nikaragua walivamia jengo la kiaskofu la jimbo katoliki la Matagalpa, ambapo Askofu Rolando José Álvarez na baadhi ya mapadre, waseminari na walei waliokuwa tayari chini ya kifungo cha nyumbani tangu tarehe 4 Agosti 2022 wakawachukua kwa nguvu watu hao 9, akiwemo askofu, kulingana na baadhi ya mashahidi, katika msafara wa magari manane. Jimbo lenyewe kwenye mitandao ya kijamii lilitoa taarifa ambayo ilizua taharuki kwa raia. Mamia ya watu, waliposikia kengele za Kanisa zikilia huku polisi wakivamia Uaskofuni walikaribia kujaribu kumlinda askofu huyo na wengine. Katika taarifa ya polisi imebainishwa kuwa Askfofu Alvarez, kama watu wengine wote waliokamatwa, walipelekwa Managua, Askofu huyo akiwa chini ya kizuizi cha nyumbani katika makazi yake ya kibinafsi na wengine 8 kwenye kambi ya polisi kwa uchunguzi.
Baba Mtakatifu mara baada ya kusema hayo amewasalimia wote kuanzia na warumi na mahujaji kutoka nchi mbali mbali: familia, makundi ya maparokia, na vyama. Kwa namna ya pekee amewasalimia Chuo cha Kipapa cha Amerika Kaskazini hasa waseminari wapya waliofika hivi karibuni na kushauri kuwa na jitihada za kiroho na kwa uaminifu wa Injili na kwa Kanisa. Amewasalimia pia watawa wa ’Ordo virginum na kuwatia moyo ili kushuhudia furaha kwa upendo wa Kristo. Baba Mtakatifu Francisko pia amesalimia waamini wa Verona, Trevignano, Pratissolo; vijana wa Paternò, Lequile na wale wa Njia ya Msalaba (cammino della Via lucis) ambao kwa kusaidiwa na mifano ya Watakatifu wa ‘mlango wa karibu’ watakutana na maskini ambao wanaishi katika vituo mbali mbali vya treni. Na salamu hata kwa vijana wa Moyo Safi wa Maria.
Sala kwa ajili ya Ukraine
Papa Francisko ameomba kudumisha ukaribu na katika sala kwa ajili ya watu wapendwa wa Ukraine ambao wanaendelea kuishi katika ukatili. Na hatimaye amewatakia Dominika njema wote lakini wasisahahu kusali kwa ajili yake. “Buon pranzo e arrivederci!” yaani Mlo mwema na kwaheri ya kuonana!