Papa Francisko Apongeza Udugu na Mshikamano wa Kimisionari Argentina Kwa Watu Asilia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa na umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii na wajenzi wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu.
Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia salama na pongezi wamisionari wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, kwa kujisadaka kwa ajili ya utume wa upendo na mshikamano miongoni mwa watu asilia wa Salta na Victoria Este walioko Jimbo Katoliki la Oràn nchini Argentina. Utume huu umeongozwa na kauli mbiu “Ndoto hujengwa pamoja.” Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kufanya uamuzi wa kutoka na kuwaendea watu mahalia; ni bora kutoka katika nafsi na kuwaendea wengine! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wamisionari wote walioshiriki katika utume huu, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika uhalisia wa maisha yao. Wakati huo huo, Padre Mariano Cordeiro wa Jimbo Katoliki Rio Cuarto anasema, utume huu wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu umewawezesha kuona, kugusa na kushiriki maisha ya watu asilia wa Salta na Victoria Este walioko Jimbo Katoliki la Oràn. Wamesikitishwa na athari za mifumo mbalimbali ya ukoloni ambao wameushuhudia katika maeneo haya, hasa ni kutokana na umaskini wa vitu, ingawa ni matajiri tunu msingi za maisha ya binadamu na utu wema. Wameanza kujenga mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu!