Tafuta

Papa Francisko: Mzunguko Mpya wa Katekesi Kuhusu Utambuzi Katika Maisha ya Kila Siku

Mambo ya kupewa uzito wa juu mintarafu Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi ni: Akili, ustadi na utashi kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kutenda kwa busara. Utambuzi unagusia mahusiano ili kupata furaha ya kweli na hatimaye, Siku ya Mwisho, binadamu watahukumiwa kutokana na utambuzi wa Mwenyezi Mungu, ambalo ni zoezi gumu lakini la muhimu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 23 Februari 2022 alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee ambazo kwa sasa zimefikia hatima yake kwa kuzama katika Maandiko Matakatifu yanayomwonesha Kristo Yesu kuwa ni njia ya kwenda kwa Baba wa milele, akisema “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yn 14:1-3. Kristo Yesu tayari alikwisha mwambia Mtume Petro kwamba, baadaye atamfuata kule anakokwenda, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu. Kristo Yesu alitambua udhaifu wa imani, ushuhuda na changamoto za ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwao. Huu ni wosia mzito ambao waamini wanapaswa kuufanyia tafakari ya kina. Baba Mtakatifu alihitimisha Kuhusu Katekesi ya Maana na Thamani ya Uzee, kwa kumwangalia Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mwioi na roho. Kanisa linaungama kweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Kanisa linamwita kuwa ni Eva mpya kutokana na utii wake kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria ni kielelezo cha imani na ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kumbe, kwa njia ya imani na utii wake thabiti, Bikira Maria akapewa upendeleo wa pekee kuweza kushiriki katika kazi ya ukombozi kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa utii wake amekuwa Eva mpya, Mama wa walio hai.

Mzungumko Mpya wa Katekesi Kuhusu Utambuzi
Mzungumko Mpya wa Katekesi Kuhusu Utambuzi

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 31 Agosti 2022 ameanzisha Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi. Hili ni tendo muhimu sana linalomwathiri kila mtu, kwa sababu kupanga ni kuchagua mambo mbalimbali katika maisha; ambayo kimsingi yanapaswa kufanywa kwa uthabiti mkubwa kwa kutambua kwamba, kuna pia mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna mambo yanayopaswa kupewa uzito wa juu mintarafu Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi unaofanywa katika maisha ya kila siku, kwani hili ni zoezi linalohusishwa na: akili, ustadi na utashi kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kutenda kwa busara. Utambuzi unagusia mahusiano ili kupata furaha ya kweli na hatimaye, Siku ya Mwisho, binadamu watahukumiwa kutokana na utambuzi wa Mwenyezi Mungu. Utambuzi ni zoezi gumu lakini la muhimu katika maisha. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, anatumia picha za maisha halisi kufafanua utambuzi wake kuhusu maisha ya wavuvi na taaluma yao: wanakusanya samaki wazuri na kuwatia chomoni na wale wabaya kuwatupa baharini au mfanya biashara aliyegundua lulu ya thamani, akauza alivyo navyo vyote, ili aweze kuipata. Baba Mtakatifu anasema, Injili inakazia kipengele muhimu kinachogusa utashi, kama yule mfanya biashara hakuona ugumu wa kuuza mali yake yote ili aweze kununua ile lulu ya thamani kubwa, kama kielelezo cha furaha yake kubwa. Rej. Mt 13:44.

Utambuzi una karaha sana, lakini ni muhimu katika maisha
Utambuzi una karaha sana, lakini ni muhimu katika maisha

Hii ni furaha ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu, kama walivyokuwa wale Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, Rej. Mt. 2:10; wale wanawake waliporejea nyumbani baada ya kuona kaburi tupu, Kristo Yesu amefufuka, wakaondoka upesi, kwa hofu na furaha nyingi, kwa sababu ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, sasa amefufuka kwa wafu. Kristo Yesu, siku ile ya mwisho atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, atawatambua. Na picha inayotumika ni ya yule mkulima, mvuvi na mfanya biashara. Hii ina maana kwamba, Ufalme wa mbinguni unajidhihirisha katika matendo ya kila siku, jambo la msingi ni kwa mwamini kuwa na msimamo thabiti. Ndiyo maana kuna umuhimu wa kufanya utambuzi wa kina kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa kwanza wa Yesu walipokutana na Kristo Yesu na kumuuliza “Rabi unakaa wapi? Na Kristo Yesu akawaambia “Njooni nanyi mtaona.” Rej Yn 1:38-39. Haya ni maneno machache sana lakini, lakini yalisababisha mabadiliko makubwa sana katika maisha ya wanafunzi wa Yesu. Wanakumbuka hata ule muda kwani “ilikuwa yapata saa kumi.” Rej. Yn 1:39. Kumbe, maarifa, uzoefu na utashi ni vipengele muhimu katika utambuzi. Mwenyezi Mungu anawaalika waja wake kutathmini na kuchagua, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu katika uhuru wake wote na hivyo anamtaka mwanadamu kuutumia vyema uhuru, wake ndiyo maana utambuzi ni muhimu sana.

Utambuzi ujenge mahusiano na mafungamano na Mungu
Utambuzi ujenge mahusiano na mafungamano na Mungu

Mwanadamu ameumbwa tofauti kabisa na viumbe wengine kwani anao utashi anapaswa kuutumia vyema ili kufanya uchaguzi makini, lakini bahati mbaya mwanadamu mara nyingi ameshindwa kuchagua kwa usahihi. Re. Mwa 2: 16-17. Ikumbukwe kwamba, mwanadamu si kigezo cha mema na mabaya, lakini uchaguzi wowote anaoufanya, matokeo yake ni ya kwake. Mwanadamu anaweza kuifanya dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, lakini anaweza kuigeuza na kuifanya kuwa jangwa la mauti. Utambuzi makini ni kiini cha mazungumzo ya kwanza kati ya Mungu na mwanadamu. Mwishoni mwa Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, Baba Mtakatifu amesema kwamba, utambuzi una karaha zake lakini ni muhimu sana kwa maisha, ili kujenga mahusiano na mafungamano ya kimwana na Mwenyezi Mungu, Baba wa milele, ambaye daima yuko yatari kushauri, kuwatia shime, kuwakaribisha na kuwakumbatia. Mwenyezì anapenda mwanadamu atumie vyema uhuru na utashi, ili aweze kupata furaha ya kweli. Kujifunza kuishi, lazima mtu ajifunze kupenda. Mwenyezi Mungu anataka watu wampende na wala wasimwope! Hili ni jambo muhimu sana la kutambua. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu, ili aweze kuwaongoza. Kamwe waamini wasiache kusali na kumwomba Roho ili awasaidie katika mchakato wa kuchagua.

Katekesi Utambuzi
31 August 2022, 15:31

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >