Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Agosti 2022 amezindua maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Agosti 2022 amezindua maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V 

Maadhimisho ya Mwaka 728 wa Msamaha wa Papa Celestin: Amani, Msamaha na Maridhiano

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, ameonesha matumaini makubwa kwamba, mji wa L’Aquila utaweza kugeuka na kuwa ni mji mkuu wa: msamaha, amani na maridhiano. Uwe ni chachu ya mageuzi: “Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha...!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Agosti 2022 amezindua maadhimisho ya Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V, kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la Aquila, nchini Italia. Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa na baadaye, ameongoza Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio.” Msamaha wa Celestin ni tukio la kihistoria na kidini linaloadhimishwa kila mwaka huko L'Aquila nchini Italia kuanzia tarehe 28 na 29 Agosti. Sherehe hii ilianzishwa na Papa Celestine V kunako mwaka 1294 kwa kuchapisha Waraka wa Kitume “Inter Sanctorum Solemnia”; Waraka huu unajulikana pia kama “Msamaha wa Celestin” unaojikita katika huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa watu wote. Waamini wanaweza kujipatia rehema kamili, ikiwa kama watafuata masharti, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa. Kwa kuingia na kushiriki katika Ibada kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la L’Aquila la “Santa Maria wa Collemaggio” Masifu ya jioni ya tarehe 28 Agosti hadi masifu ya jioni ya tarehe 29 Agosti. Mama Kanisa mwaka 2022 anaadhimisha Tukio hili kwa mwaka wake wa 728 kama sehemu ya utangulizi wa Maadhimisho ya Jubilee ya Kanisa la Kiulimwengu iliyoanzishwa na Papa Boniface VIII kunako mwaka 1300 na kwa muda mrefu imekuwa ikisindikizwa na matukio mengine mengi ya kitamaduni na ya kihistoria, ambayo hufanyika katika kipindi cha juma zima, mwishoni mwa mwezi Agosti. Maadhimisho hayo yamekuwa ni sehemu ya "Urithi wa Italia kwa mila" tangu 2011 na kuandikwa katika kumbukumbu za UNESCO kama urithi wa binadamu.

Habari Njema ya Wokovu ilete mageuzi katika maisha ya waamini
Habari Njema ya Wokovu ilete mageuzi katika maisha ya waamini

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, ameonesha matumaini makubwa kwamba, mji wa L’Aquila utaweza kugeuka na kuwa ni mji mkuu wa: msamaha, amani na maridhiano. Uwe ni chachu ya mageuzi kama yanavyoimbwa na Bikira Maria kwenye utenzi wake wa “Magnificat”: “Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.” Lk 1: 51-53. Na Kristo Yesu katika Injili anakaza kusema, “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Lk 14: 11. Bikira Maria anaheshimiwa na watu wa Mungu Jimboni humo kama Wokovu wa Watu wa L’Aquila, mwaliko na changamoto kwa waamini kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao, ili Bikira Maria aweze kuombea msamaha na amani kwa dunia nzima. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, ili wote watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba yao na anawapenda wote upeo. Hiki ndicho kiini cha Injili na ushuhuda wa Injili hii ni Fumbo la Umwilisho, kwani Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Maadhimisho ya Dominika ya 22 ya Mwaka C wa Kanisa kwa mwaka 2022 yanachukua uzito wa pekee kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la L’Aquilla, kwani Mama Kanisa anaadhimisha Mwaka wa 728 wa Msamaha wa Papa Celestin V, uliozinduliwa kwa kufungua lango la Kanisa kuu la “Santa Maria in Collemaggio” Jimbo kuu la Aquila. Papa Celestin V ni kielelezo cha sehemu ya Maandiko Matakatifu isemavyo “kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana”. YbS 3:18. Papa Celestin V alikuwa ni kiongozi mwenye utashi thabiti, aliyejitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wake, kwa kujivika fadhila ya unyenyekevu iliyomwezesha kutambua na hatimaye, kutekeleza mapenzi ya Mungu, kwa kupata kibali machoni pa Bwana, kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu. Rej. YbS 3: 19-20. Katika ulimwengu ambamo kiburi ambalo kimsingi ni kaburi la utu wema, kisheheni, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kujivika fadhila ya unyenyekevu na upole wa moyo. Fadhila ya unyenyekevu ni udongo wenye rutuba safi ambamo fadhila zote huoteshwa, hustawi na hatimaye, kuzaa matunda ya toba, wogonfu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha uhuru wa ndani.
Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha uhuru wa ndani.

Fadhila ya unyenyekevu inamwezesha mwamini kutambua karama, mapaji na mapungufu yake kama binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu badala ya mwamini kujiangalia na kujitafuta mwenyewe, kwani yote yanawezekana kwa mtu anaye amini! Mwenyezi Mungu ndiye nguvu ya waja wake na wala si kwa juhudi zao binadamu au kwa kufuata mantiki za ulimwengu mamboleo. Papa Celestin V ni shuhuda wa ujasiri wa Injili na huruma ya Mungu, ambayo kimsingi ndicho kiini cha Habari Njema ya Wokovu! Hapa mwamini anajitambua na hivyo kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa ari na moyo mkuu pasi na kujificha! Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele ni ufunuo wa Uso wa upendo wa Mungu unaookoa. Mji wa L’Aquila umeonesha uaminifu wa hali ya juu kabisa kwa kuendeleza Mapokeo ya Kanisa yanayokita mizizi yake katika huruma ya Mungu, inayowawezesha waamini kuhisi kwamba, wamepokelewa, wamekubalika na kusimama imara kwa miguu yao; wametiwa nguvu na kuponywa na hatimaye, wakatiwa ujasiri wa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Msamaha ni mchakato wa kutoka katika kifo na kuingia katika mwanga wa maisha; ni kutoka katika hali ya kujisikia kuelemewa sana na dhambi na kuanza kuelekea kwenye uhuru na furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Msamaha wa Papa Celestin V, iwe ni fursa ya kuambata: Upatanisho na kujenga utamaduni wa kukimbilia kuchota neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika maisha, kila wakati ili kujenga amani inayosimikwa katika msamaha uliopokelewa na hatimaye, kutolewa kwa wengine. Baba Mtakatifu amewatia shime kusonga mbele baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni maafa ambayo yameacha madonda na machungu makubwa katika akili na noyo za watu, lakini wakaonja huruma ya Mungu baada ya kuwa wamepoteza walau kila kitu, lakini kwa sasa wanaonja upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo. Kwa udhaifu, mateso na mahangaiko yao sasa wanaweza kuwa watunzaji na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha. Baba Mtakatifu mwishoni mwa mahubiri yake anakaza kusema, “tetemeko la moyo” iwe ni fursa ya waamini kujitambua jinsi walivyo kwa karama na mapungufu yao ya kibinadamu na hivyo kuwa na ujasiri wa kujifunza unyenyekevu.

Papa Celestin V alikuwa ni shuhuda wa unyenyekevu wa Kiinjili.
Papa Celestin V alikuwa ni shuhuda wa unyenyekevu wa Kiinjili.

Fadhila ya upole na unyenyekevu iwawezeshe kutunza na kushuhudia huruma ya Mungu, uadilifu na nidhamu katika maisha, wakijitahidi kufuata mfano wa Kristo Yesu aliyejinyenyekesha katika Fumbo la Umwilisho na hatimaye, akatundikwa juu ya Msalaba, kielelezo cha juu kabisa cha unyenyekevu katika huduma ya upendo na uhuru wa kweli! Habari Njema ya Wokovu imeleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu, lakini vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia, ukosefu wa haki msingi za binadamu, ubinafsi na uchoyo ni kielelezo makini cha ukosefu wa uhuru wa ndani! Kukiri na kutambua udhaifu na mapungufu yako ya kibinadamu ni kielelezo makini cha wema na huruma ya Mungu.

Papa Msamaha
28 August 2022, 15:55