Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Agosti 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali pamoja na Baraza la Makardinali: Utume wa Kanisa Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Agosti 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali pamoja na Baraza la Makardinali: Utume wa Kanisa 

Papa Francisko: Makardinali Tangazeni na Kushuhudia Matendo Makuu ya Mungu Katika Maisha

Utenzi wa Mtume Paulo ni chemchemi ya historia ya ukombozi. Kila mwamini anayo Galilaya. Neno la Mungu linaamsha ndani mwao mshangao wa kuwa Kanisa na ndani ya Kanisa, chimbuko lake ni Sakramenti ya Ubatizo. Makardinali kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wanatumwa kumshuhudia Kristo Yesu, huku wakiendelea kutangaza matendo makuu ya Mungu kwa watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 27 Agosti 2022 amewatangaza na kuwasimika Makardinali wapya 20 pamoja na kuwapigia kura wenyeheri wanaotarajiwa kuingizwa kwenye orodha ya watakatifu wa Kanisa, Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa yaani tarehe 9 Oktoba 2022, kwenye Uwanja waq Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni: Mwenyeheri Padre Giovanni Battista Scalabrini aliyetangazwa kuwa Mwenye heri na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 9 Novemba 1997. Alizaliwa tarehe 8 Julai 1839 na hatimaye kufariki dunia tarehe Mosi Juni 1905. Alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, Italia na Mwanzilishi wa Mashirika ya Wamisionari wa Mtakatifu Carlo Borromeo, maarufu kama Wascalabrini na pia ni Muasisi wa Taasisi ya waamini Walei Wascalabrini, iliyoanzishwa kunako mwaka 1961. Pili ni Mwenyeheri Artemide Zatti, Bruda wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco aliyezaliwa tarehe 12 Oktoba 1880, nchini Italia. Akafariki dunia tarehe 15 Machi 1951 huko Viedma nchini Argentina. Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika huduma kwa maskini kwa kuongoza hospitali na duka la dawa kwa ajili ya maskini kwa muda wa miaka 40. Tarehe 14 Aprili 2002 atakatangzwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mwenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 29 na Jumanne tarehe 30 Agosti 2022 ameongoza mkutano wa Baraza la Makardinali kwa faragha, ili kutoa nafasi ya kufanya tafakari ya kina kuhusu Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.”

Makardinali wanatumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu
Makardinali wanatumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu

Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuanza kujifunza utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Baraza hili limekuwa na ushiriki mkubwa wa Makardinali, kati ya Makardinali 226, waliohudhuria ni zaidi ya 200. Baba Mtakatifu Jumanne jioni tarehe 30 Agosti 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kushirikiana na Makardinali wapya pamoja na Baraza lote la Makardinali kwa ajili ya Kanisa. Katika mahubiri yake amekazia zaidi umuhimu wa Makardinali kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wao. Utenzi wa Mtume Paulo ni chemchemi ya historia ya ukombozi. Kila mwamini anayo Galilaya yake ya kwanza, alipokutana na Kristo Yesu. Neno la Mungu linaamsha ndani mwao mshangao wa kuwa Kanisa na ndani ya Kanisa, chimbuko lake ni Sakramenti ya Ubatizo tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, huku wakiendelea kutangaza matendo makuu ya Mungu kwa watu wa Mataifa.

Ushirika na Umisionari ni mambo makuu ya kuzingatiwa.
Ushirika na Umisionari ni mambo makuu ya kuzingatiwa.

Kristo Yesu ni chanzo na hatima ya maisha ya mwanadamu na kwa njia yake, amekuwa ni baraka kwa binadamu, akawachagua, ili wawe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo, na katika Kristo Yesu, wanao ukombozi na msamaha wa dhambi, chanzo cha ushirika mkamilifu na kwa kutiwa muhuri wa Roho Mtakatifu, amekuwa arabuni ya urithi na ukombozi wao kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba. Rej. Efe 1: 14. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kutambua tena ndani mwao mshangao unaobubujika kutoka katika Utenzi wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Wakristo wanakumbushwa kwamba, wako duniani kwa lengo la kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wanapaswa kutambua kwamba, hapa duniani ni mahujaji na wala hawana makazi ya kudumu, bali wajitahidi kujielekeza zaidi kwa mambo ya mbinguni. Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwamba, anawatangulia Galilaya, huko ndiko watakakokutana naye, ili kumtambua na kushiriki katika furaha yake ya milele. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mwamini anayo Galilaya yake ya kwanza katika maisha, siku ile alipokutana na Kristo Yesu kwa mara ya kwanza. Ili kuwa kweli mwamini bora, kuna haja ya kuwa na kumbu kumbu endelevu ya siku ile ya kwanza ya kukutana na Yesu pamoja na mwendelezo wake.

Hii ni neema ya kumbukumbu inayomwezesha mwamini kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yake wakati wa majaribu! Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wanatumwa kuwabatiza watu wa Mataifa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kweli waweze kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo; faraja kwa wale wanaoteseka. Ni dhamana inayotekelezwa kama mtu mmoja mmoja na kama: jumuiya na hatimaye, kama Baraza la Makardinali, daima wakijivika fadhila ya unyenyekevu na kamwe wasimezwe na malimwengu wakasahau wajibu na dhamana yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuvutwa na mshangao wa kuwa ndani na sehemu ya Kanisa, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa. Mtakatifu Paulo VI analitaka Kanisa kujitambua; kutambua asili na utume wake kadiri ya mpango wa Mungu katika historia ya ukombozi. Kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria, Makardinali wote wajaliwe neema na baraka ya mshango wa kuwa ni kwa ajili na sehemu ya Kanisa ili kutangaza na kushuhundia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.

Misa Makardinali

 

31 August 2022, 16:08