Kongamano la 5 la VIWAWA Kitaifa, Tabora: Ujumbe Kwa Vijana 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kongamano la Tano la Taifa la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, VIWAWA, linazinduliwa rasmi kuanzia tarehe 4 hadi 8 Agosti 2022, huko Jimbo kuu la Tabora kwa kuongozwa na kauli mbiu “Simama nimekuteua uwe shahidi wa yale uliyoyaona.” Rej. Mdo 26: 16. VIWAWA wanasema, wanalo jambo lao na wanawakaribisha vijana wa kizazi kipya kujiunga nao kwenye Viwanja vya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Jimbo kuu la Tabora. Waamini wanahamasishwa kutoka kwa haraka kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na matumaini kwa watu waliokata tamaa kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu baada ya kukumbana mubashara na Kashfa ya Msalaba, “wakanywea na kubaki wadogo sana.” Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana pale wanapokumbana na vikwazo katika imani au imani yao inapoanza kuyeyuka kama ndoto ya mchana, wawe na ujasiri wa kumkimbilia Bikira Maria, Mama wa Kanisa, ili awafundishe, kwani anawaelewa na atawasaidia katika mchakato wa kupyaisha imani, ili kuwa na mwelekeo wa matumaini mapya katika maisha. Kamwe vijana wasiridhike na mafanikio waliyopata, bali wawe na ujasiri wa kuthubutu kuota ndoto, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu sanjari na kuwasaidia walimwengu kujenga dunia inayofumbatwa katika udugu wa kibinadamu. Ushuhuda wa imani uwawezeshe vijana ili kwa kuona waweze kuamini. Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kujenga na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.
Vijana wamtambue Kristo anayeteseka kati ya wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wawe na subira, wajenge utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu tayari kuthubutu kufanya hija katika ushirika unaowawezesha kushikamana kama watu wa Mungu na hivyo kuwa na uhakika wa maisha. Ubinafsi na uchoyo ni sumu ya maisha ya pamoja na ni chanzo cha maafa na majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu. Mtakatifu Petro katika Injili kuhusu Ufufuko wa Kristo aliingia kaburini, akaona na kuamini. Haya ndiyo yale yaliyojitokeza kwenye Arusi ya Kana, Yesu alipogeuza maji yakawa divai; alipowaponya wagonjwa na kuwalisha watu elfu tano, Neno la uzima na mkate ulioshuka kutoka mbinguni! Ni ushuhuda wa Yesu aliyemfufua Lazaro; ufunuo wa Uso wa Mungu asiyeonekana! Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwani katika udhaifu wao wa kibinadamu, neema ya Mungu inaweza kuwainua na kuwakirimia matumaini mapya kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu baada ya kupata Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!
Ufufuko wa Kristo ni ushuhuda kwamba, kifo hakina sauti ya mwisho na hata katika mazingira kama haya ya kukatisha tamaa, bado Injili ya uhai inaweza kupeta na kung’ara. Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa kushinda dhambi na udhaifu wa binadamu. Fumbo la Pasaka lilileta mabadiliko makubwa katika maisha ya Mitume, hapa, ujasiri unatiliwa mkazo zaidi. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini ili kweli mwanga wa Kristo Mfufuka uweze kupenya katika maeneo yenye giza. Hii ndiyo changamoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapatia vijana katika maisha yao, huku wakitambua kwamba, kwa hakika wanapendwa na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Kwa njia hii, safari ya maisha inasonga mbele pasi na woga wala wasi wasi unaowakatisha tamaa vijana wengi. Vijana watoke kwa haraka kumwendea Kristo na kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao, huku wakiwa wamesheheni upendo, imani na furaha ya kweli!
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 akiwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, aliweka sahihi kwenye Wosia wa Kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Wosia huu umezinduliwa rasmi, tarehe 2 Aprili 2019. Wosia huu ni matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Mang’amuzi na Miito”. Huu pia ni mwendelezo wa mchakato wa Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya familia, kwani utume wa Kanisa kwa familia na vijana ni sawa na chanda na pete; unategemeana na kukamilishana! Wosia huu wa kitume umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana na Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Wosia huu umegawanyika katika sura tisa amana na utajiri unaobubujika kutoka katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, iliyoadhimishwa mwezi Oktoba 2018. Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anakita tafakari yake kwenye Neno la Mungu kuhusu vijana tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya. Sura ya Pili inamwonesha Kristo Yesu ambaye daima ni kijana na chemchemi ya ujana wa Kanisa kama ilivyo hata kwa Bikira Maria, msichana wa Nazareti.
Sura ya tatu, Vijana wanaambiwa kwamba, wao ni leo ya Mungu inayofumbatwa katika matamanio halali ya vijana, madonda wanayokumbana nayo katika hija ya maisha yao pamoja tafiti endelevu kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya ujana. Baba Mtakatifu anagusia changamoto za ujana zinazoibuliwa katika ulimwengu wa kidigitali, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na kuonesha mwanga unaoweza kuwaokoa vijana kutoka katika giza hili la maisha. Sura ya nne ni mbiu kwa vijana wote kwamba, “Mungu ni upendo”, Kristo Yesu anaokoa na kwamba, yu hai kabisa na kwa njia ya Roho Mtakatifu, vijana wanaweza kuboresha maisha yao. Sura ya tano inaonesha mapito ya ujana katika makuzi na ukomavu; vijana wanaojisadaka na kujitosa kwa ajili ya huduma kwa jirani zao. Vijana wanakumbushwa kwamba, wanaitwa na kutumwa kama wamisionari jasiri, ili kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya maisha yao katika ukweli, hii ni changamoto kwa vijana wote! Sura ya sita, inawaonesha vijana waliokita mizizi yao katika mambo msingi ya maisha. Hawa ni wale vijana wenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na wazee; ili kumwilisha ndoto na maono, ili kwa pamoja, wazee na vijana waweze kuthubutu!
Sura ya saba ni kuhusu utume wa Kanisa kwa vijana, kwa kuwasindikiza na kuwaongoza, wao wenyewe wakionesha kipaji cha ubunifu. Mkazo katika utume kwa vijana: tafiti na ukuaji! Kanisa linapaswa kujenga mazingira yatakayosaidia kumwilisha vipaumbele hivi. Kanisa pia linapaswa kuwekeza zaidi katika utume wa vijana kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu; kwa kuendesha pia utume wa vijana katika “vijiwe vya vijana” ili kuwatafuta na kuwaendea huko huko waliko, daima kwa kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu. Daima vijana wakumbuke kwamba, wao ni wamisionari, kumbe, utume kwa vijana unapaswa kujikita katika umisionari, huku vijana hawa wakiwa wanasindikizwa na watu wazima na wakomavu, ili kujitambua na kwamba, wanapaswa kutembea bega kwa bega, huku wakiheshimu na kuthamini uhuru wao! Sura ya nane, Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu miito, kwa kukazia upendo na familia, ili kujisadaka bila ya kujibakiza katika kazi na hatimaye, ujenzi wa familia bora! Baba Mtakatifu anatambua fika changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana, lakini wawe wepesi kusoma alama za nyakati kwa kuondokana na kishawishi cha kutaka kuchagua kazi, jambo la msingi kwanza ni huduma!
Baba Mtakatifu anahitimisha sura ya nane kwa kuangalia wito maalum unaowasukuma vijana kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao katika maisha ya kipadre na kitawa, kama utimilifu wa maisha yao! Sura ya tisa ni kuhusu: Mang’amuzi ambao ni mchakato unaomwezesha kijana kutambua wito wake katika maisha! Hii ni dhamana inayohitaji ukimya na tafakari ya hali ya juu, ili kuweza kutoa maamuzi mazito katika maisha. Mang’amuzi ya miito yanapaswa kuzingatia mambo makuu matatu: kusikiliza kwa makini; kufanya maamuzi ya busara na hatimaye, kusikiliza kutoka katika undani wa maisha, ili kutambua ni mahali gani ambako Mwenyezi Mungu anamtaka kijana huyu kwenda. Baba Mtakatifu anahitimisha Wosia huu wa kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” kwa kuonesha hamu ya furaha ya moyo wake kwani anataka kuwaona vijana ambao wanaonekana kwenda taratibu na waoga katika maisha, kuanza kutimua mbio na kumwendea Kristo Yesu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa linahitaji ari na mwamko wa vijana wa kizazi kipya; maoni yao, lakini zaidi imani inayomwilishwa katika ushuhuda wa matendo! Baba Mtakatifu kwa unyenyekevu anawakumbusha vijana kwamba, wakifanikiwa kwenda mbio na kufika mwishoni mwa safari, wawe na uvumilivu ili kuwasubiria wazee wanaojikongoja!