Hija ya Kitume ya Papa Francisko Kazakhstan 13-15 Septemba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka katika hija yake ya 37 Kimataifa nchini Canada, aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwamba anakabiliana na changamoto za kiafya, lakini bado ametia nia ya kuendelea kufanya hija hizi za kitume kama kielelezo cha: huduma, utume na ukaribu wake kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kushiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi litakaloadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022. Kongamano hili linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili nchini Kazakhstan, Jumanne, tarehe 13 Septemba 2022, jioni baada ya Mapokezi ya Kitaifa, atakutana kwa faragha na Rais na baadaye atazungumza na viongozi wa Serikali, mashirika ya kiraia pamoja wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa. Jumatano tarehe 14 Septemba 2022, Baba Mtakatifu atashiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi. Itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza kwa faragha na baadhi ya viongozi wa dini watakaokuwa wanashiriki katika Mkutao huu, jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.
Alhamisi tarehe 15 Septemba 2022 atakutana na kuzungumza kwa faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Kazakhstan. Anatarajia kukutana na kuzungumza na watu wa Mungu nchini humo kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Msaada wa Daima. Alasiri, atashiriki na kutoa hotuba ya mwisho wakati Wajumbe watakapokuwa wanatoa Tamko la Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi mjini Kaza, Nur Sultan. Baadaye ataondoka na kurejea mjini Roma majira ya saa 2: 15 Usiku. Askofu Adelio Dell’Oro wa Jimbo Katoliki la Karaganda, nchini Kazakhstan katika mahojiano maalum na Vatican News, anasema kwamba, watu wa Mungu nchini humo wamepokea tamko hili kwa furaha na matumaini makubwa na kwamba, Serikali inajipanga ili kuhakikisha kwamba, inatoa msaada wa usafiri kwa watu wanaotaka kwenda kukutana na Baba Mtakatifu Francisko. Kazakhstan ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa watu kutoka katika zaidi ya Mataifa 130, kumbe ni watu wenye dini, imani na mapokeo mbalimbali ya maisha ya kiroho. Kumbe, hija hii ya kitume ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni.
Habari zisizothibitishwa bado zinaonesha kwamba, Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima, anatarajiwa kuhudhuria kwenye mkutano huu. Pengine, hii inaweza kuwa ni fursa ya viongozi hawa wawili kukutana na kuzungumza ana kwa ana baada ya mazungumzo yao nchini Cuba na yale mazungumzo yaliyofanywa kwa njia ya vyombo na mitandao ya kijamii. Kongamano la Kwanza la Viongozi wa Dini Duniani liliadhimishwa kunako Januari 2002 mjini Assisi, Italia, kwa mwaliko wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Lengo lilikuwa ni kuendelea kuimarisha mchango wa dini mbalimbali katika kukuza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Hii ni kutokana na kinzani kubwa zilizoibuka miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali duniani, baada ya shambulizi la kigaidi lililofanyika nchini Marekani tarehe 11 Septemba 2001. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki aliwakutanisha viongozi wa dini mbalimbali huko mjini Assisi, nchini Italia, kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani! Mkutano huu, ukawa ni chachu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kudumisha amani duniani. Sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ni nyenzo msingi ya ujenzi wa amani duniani.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Miaka 25 baadaye, aliwataka waamini wa dini mbalimbali duniani kuendeleza roho na moyo wa sala kutoka Assisi kwa kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene ili kuimarisha maridhiano kati ya watu wa Mataifa; alikazia umuhimu wa vijana kufundwa utamaduni wa haki na amani na kwamba, majadiliano ya kidugu ni muhimu sana katika kukuza haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi; mshikamano wa udugu wa kibibadamu; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waraka huu umekuwa ni rejea makini katika mchakato wa kuganga na kuponyesha madonda yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Ujenzi wa ulimwengu mpya ni mchakato wa watu wote wa Mungu unaojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani duniani. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha majadiliano katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yasaidie kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni sehemu ya hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa sanjari na ujenzi wa siasa ya amani duniani inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, majadiliano pamoja na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa iwekeze katika uchumi fungamani unaojali na kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake!