Hayati Kardinali Jozef Tomko: Aliitwa, Akawekwa Wakfu na Kutumwa Kulihudumia Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mara baada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa, aliyefariki dunia tarehe 8 Agosti 2022 mjini Roma, akiwa na umri wa miaka 98, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio.” Ibada ya Misa takatifu imeongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ambaye katika mahubiri yake, amepembua wasifu wa Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa, kama ni kiongozi aliyeitwa, akawekwa wakfu na kutumwa kulihudumia Kanisa katika nyadhifa mbalimbali, kwanza kabisa kama Padre na hatimaye kama Kardinali katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Mama Kanisa amewakusanya watoto wake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 11 Agosti 2022 kumsindikiza Kardinali Tomko katika usingizi na maisha ya uzima wa milele kwa kusukumwa na imani kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa kwamba, “Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.” 2 Kor 5:1. Na huko waamini wataungana na kumwona Mungu jinsi alivyo, ili kushiriki upendo wake usiokuwa na kikomo!
Kardinali Jozef Tomko, ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika huduma katika Sekretarieti kuu ya Vatican, akabahatika kukabidhiwa nyadhifa nyingi katika maisha na kuziona kuwa kama wito wa kuhudumia watu wa Mungu. Hii ni huduma aliyoitoa kwa hekima, busara na weledi, daima akiwa na utambuzi wa Kikanisa “Sensum Ecclesiae. Alikuwa ni mtu mtulivu, mwenye uwezo mkubwa kiakili, aliyependwa na wengi na kwa hakika alikuwa nadhifu katika maisha na utume wake. Hayati Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa alizaliwa tarehe 11 Machi 1924 huko mjini Udavské, Jimbo kuu la Košice, nchini Slovakia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 12 Machi 1949 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, lakini hakuweza kurejea tena nchini Slovakia kutokana na madhulumu ya utawala wa Kikomunisti nchini mwake, na hivyo akabaki na kuendelea na utume wake Jimbo kuu la Roma. Kati ya mwaka 1962 hadi mwaka 1966 aliteuliwa kuwa ni Afisa mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Hapa akaonesha karama na mapaji yake kwa kuchapisha makala zilizoonesha ukomavu na upevu wake wa imani, kiasi cha kuwavutia watu wengi.
Mtakatifu Paulo VI mwezi Desemba mwaka 1974, akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Tarehe 12 Julai 1979, akateuliwa kuwa Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu na kupandishwa hadhi kuwa Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 15 Septemba 1979 kwenye Kikanisa cha Sistina, kama kielelezo cha Mama Kanisa kwa watoto wake waliokuwa wanadhulumiwa chini ya utawala wa Kikomunisti nchini Slovakia. Kauli mbiu yake ya Kiaskofu ikawa ni “Ut Ecclesia aedificetur” yaani “Kwa ajili ya Ujenzi wa Kanisa.” Katika maisha na utume wake, alijipambanua kama mtaalam aliyebobea katika masuala ya Sinodi za Maaskofu na kunako mwaka 1985 akapewa dhamana ya kuandaa kumbukizi la Miaka 20 tangu kufungwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya waamini walei iliyoadhimishwa kunako mwaka 1987. Alijiekeza pia katika maisha na utume wa kiekumene, na mara nyingi aliteuliwa kuwa ni kiongozi wa ujumbe wa Vatican katika majadiliano ya kiekumene kati ya Vatican na Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, The Lutheran World Federation, LWF; Kwa lugha ya Kijerumani “Lutherischer Weltbund.” Ni kiongozi aliyejisadaka sana katika majiundo endelevu ili kuhakikisha kwamba, anaendelea kusoma alama za nyakati, licha ya ratiba yake “kubanana sana.”
Hayati Kardinali Jozef Tomko, alipenda pia kutoa huduma za kichungaji kwenye Parokia mbalimbali za Jimbo kuu la Roma kadiri ya mahitaji. Amewahi kuwa ni Mwakilishi wa Vatican kwenye Mikutano ya Kanda ya Makanisa Katoliki Barani Asia, huko Manila mwaka 1970, Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Oceania, Sydney mwaka 1973, Mkutano wa Puebla wa Mwaka 1979, Jubilei ya Miaka 25 ya CELM mwaka 1980 na Mkutano wa SECAM ulioadhimishwa mjini Yaoundè Cameroon kunako mwaka 1981. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili akamteuwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kuanzia tarehe 27 Mei 1985 hadi 9 Aprili 2001. Hayati Kardinali Jozef Tomko, akaonesha ari na mwamko mkubwa wa shughuli za kimisionari na kitume, kwa kutambua kwamba, Mama Kanisa alikuwa na dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya duniani, Kristo Yesu, akiwa ni kiini na hatima ya Habari Njema. Akachakarika kukoleza mchakato wa kuanzisha Majimbo, Seminari na Nyumba za malezi, pamoja na kuanzishwa kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwenye majimbo mbalimbali duniani, kama sehemu ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.
Mwaka 1980 aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Rais Mwakilishi wa Sinodi ya Maaskofu kwa Ajili ya Bara la Ulaya. Kati ya tarehe 15 Oktoba 2002 hadi tarehe 1 Oktoba 2007 aliteuliwa kuwa ni Rais wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa. Ilikuwa ni tarehe 25 Mei 1985 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Tarehe 8 Agosti 2022 akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 98 si haba hata kidogo, matendo makuu ya Mungu. Mwinjili Yohane anasema “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Yn 141-3. Maneno haya yawe ni faraja na changamoto kwa viongozi wa Kanisa wanapomsindikiza Kardinali Jozef Tomko, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais mstaafu wa Kamati ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa, ili hata wao, waweze kuhitimisha maisha na utumishi wao wakiwa waaminifu kwa Mungu, Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao, ushuhuda makini ambao umeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi kwa kifo cha Kardinali Tomko.
Sasa apumzike katika usingizi wa amani akiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Amina. Takwimu zinaonesha kwamba, kwa kifo cha Kardinali Jozef Tomko, kwa sasa Baraza la Makardinali linaundwa na Makardinali 206 kati yao kuna Makardinali 116 wenye haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wakati ambapo wengine 90 wamekwisha kupoteza sifa na haki ya kupigiwa kura katika uchaguzi mkuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. “In paradisum deducant te Angeli, in tuo adventu suscipiant te martyres et perducant te in sanctam civitatem Jerusalem.” Yaani: “Malaika wakupokee peponi; mashuhuda wa imani wakukaribishe na kukuongoza katika mji Mtakatifu wa Yerusalemu.