Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Wananchi wa DRC na Sudan Kusini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ametia nia ya kutembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, mjini Kinshasa na Goma tarehe 2-5 Julai 2022 sanjari na Juba, Sudan ya Kusini tarehe 5-7 Julai 2022, lakini hija hii ya kitume imesogezwa mbele hadi hapo itakapotajwa tena kutokana na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa kukabiliana na changamoto ya afya. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa watu wa Mungu nchini DRC na Sudan ya Kusini, anapenda kuonesha masikitiko yake makubwa kutokana na kuhairishwa kwa hija hii ya kitume, iliyokuwa inapania pamoja na mambo mengine, kunogesha mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. Jambo la msingi kwa watu wa Mungu anasema Baba Mtakatifu ni kutokata tamaa, bali waendelee kuwa na matumaini, kwani panapo majaliwa, atawatembelea, ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anaendelea kuwabeba katika sakafu ya moyo wake kwa njia ya sala, akikumbuka mateso, mahangaiko na changamoto wanazokabiliana nazo kwa muda mrefu. DRC kwa mfano ni nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikinyonywa sana rasilimali zake asilia, vita na ukosefu wa amani na usalama kwa raia na mali zao.
Maeneo ya Mashariki wa DRC yamegeuka kuwa ni uwanja wa vita ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Jambo la kusitikisha ni kuona watu wengi wameigeuzia DRC kisogo. Baba Mtakatifu anasema, watu wa Mungu Sudan ya Kusini wanaendelea kupaaza sauti zao, huku wakililia amani ya kudumu. Wananchi wengi wa Sudan ya Kusini kwa muda mrefu sasa wanateseka kwa vita na umaskini. Wana kiu ya kutaka kuona mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa vinashika mkondo wake. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani pamoja na Mchungaji John Chalmers, ambaye aliwahi kuwa Mchungaji mkuu wa Kanisa la Presibiterian huko nchini Scotland, wanapenda kuchangia katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene nchini Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anakosa maneno mazuri zaidi ya kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu nchini DRC na Sudan ya Kusini. Jambo la msingi kamwe wasikubali watu wachache wawapoke matumaini yaliyomo ndani mwao, kwani mbele yake na machoni pa Mwenyezi Mungu ni wana wateule wa Mungu, mwaliko wa kujiaminisha na kuendelea kumtumainia.
Watambue kwamba, kuanzia kwa wanasiasa, pamoja na watu wote wanao utume nyeti unaowataka washiriki kikamilifu katika kuandika ukurasa mpya wa upatanisho wa Kitaifa, msamaha; amani, utulivu na maendeleo. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na watu wote, kwa kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hii ni ndoto kubwa kwa vijana wanaotaka kuona mapambazuko ya amani, kwa kuweka silaha chini na hatimaye, kuondokana na chuki, ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa udugu wa kibinadamu. Machozi yanayomwagika ardhini na kwa njia ya sala ni muhimu sana na kamwe hayatapotea bure. “Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani.” Yer 29: 11. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaombea amani ya Mwenyezi Mungu ili iweze kuwashukia nyoyoni mwao na kwamba, anapenda kukutana na hatimaye, kuonana mubashara. Lengo la uwepo wake miongoni mwao ni kuwapatia baraka zake za kitume, kuwaombea pamoja na kujenga mahusiano bora zaidi na watu wa Mungu katika nchi hizi mbili. Amewapatia baraka zake na kuwaomba wandelee kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.