Tafuta

Siku ya Pili ya Wazee na Wajukuu inaadhimishwa tarehe 24 Julai 2022. Siku hii inanogeshwa na kauli mbiu “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15. Siku ya Pili ya Wazee na Wajukuu inaadhimishwa tarehe 24 Julai 2022. Siku hii inanogeshwa na kauli mbiu “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15.  

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Pili ya Wazee na Wajukuu 24 Julai 2022

Uzee ni kipindi cha neema na baraka; wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii, mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni pamoja na: imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao ya kila siku. Wazee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee na Mababu Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai na kwa mwaka huu, hii ni Siku ya Pili na inaadhimishwa tarehe 24 Julai 2022. Siku hii inanogeshwa na kauli mbiu “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea wazee ili waweze kuongoka na kuwa ni waalimu wa huruma na upendo; ili uzoefu na mang’amuzi yao, yaweze kuwasaidia wazee kuangalia ya mbeleni kwa matumaini na uwajibikaji. Uzee ni kipindi cha neema na baraka; wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii, mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni pamoja na: imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao ya kila siku. Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana kiasi cha kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Wazee ni utajiri na amana ya jamii
Wazee ni utajiri na amana ya jamii

Wazee ni watu ambao walikuwa ni mwamba na ngome salama wakati ambapo wajukuu wao walipokuwa wanajisikia kutofahamika, wakiogopa changamoto za maisha! Wazee wakawa wa kwanza kuwakimbilia na kuwapokea kwa faraja, huku wakipangusa machozi yaliyokuwa yamefichika machoni na ndoto iliyokuwa imezama katika undani wa sakafu ya nyoyo zao. Ni kwa njia ya huruma na upendo wa wazee, leo hii wale waliokuwa watoto sasa ni watu wazima na wanajitegemea na kutembea kwa miguu yao wenyewe. Wazee waliorutubisha maisha ya watoto wao, wana kiu ya kuwaona wajukuu wao, wakiwatunza na kuwaonesha ukarimu na upendo wa dhati. Wazee wanataka kusikia uwepo wa vijana wa kizazi kipya, changamoto kwao ni kuinua macho ili kuwaangalia wazee kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya, anawaalika wazee kutoogopa uzee na kudhani kwamba, uzee ni ugonjwa na kamwe wasielemewe na utamaduni wa kutupa, usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Bali watambue kwamba, maisha marefu kadiri ya Maandiko Matakatifu: wazee ni baraka, ishara hai ya wema na huruma ya Mungu ambaye ni chemchemi ya maisha. Heri nyumba anamoishi mzee na heri kwa familia inayotunza na kuwaheshimu wazee. Jamii inapaswa kuhakikisha kwamba, sera na mikakati kwa ajili ya huduma kwa wazee, zinawajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwani hata katika uzee wao wataendelea kuzaa matunda. 

Katika uzee, watu wanatambua kwamba, nguvu zinapungua na afya inaanza kudhohofu kiasi cha kuanza kujihisi kwamba, “si mali kitu katika jamii inayowazunguka.” Ikumbukwe uzee si huku ya kifo, bali ni chemchemi ya baraka na neema. Ni mwaliko wa kuendelea kuboresha hata maisha ya kiroho kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa sanjari na kuendelea kuboresha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na huduma makini kwa jirani, wanaohitaji sala, sadaka na uwepo wao angavu! Baba Mtakatifu anawataka wazee wawe ni baraka na neema kwa jirani wanaowazunguka. Uzee si wakati wa kutaka wala kukatishwa tamaa na wala wazee hawapaswi kuelemewa na mawazo wala hofu zisizo na miguu wala kichwa! Wazee wawe ni vyombo na mashuhuda wa mapinduzi ya huruma na upendo; wazee wanahimizwa kujielekeza katika mapinduzi ya maisha ya kiroho yasiyokuwa na vurugu, kwa kuwajibika barabara. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, wazee kwa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, madhara ya vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urussi bila kusahau matatizo na changamoto mbalimbali zinazozisibu familia katika ulimwengu mamboleo. Changamoto zote hizi zinahitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuwaona na kuwathimini watu wengine kama ndugu wamoja.

Wazee waboreshe maisha yao ya kiroho kwa sala, Neno la Mungu na huduma
Wazee waboreshe maisha yao ya kiroho kwa sala, Neno la Mungu na huduma

Ni katika muktadha huu, wazee wanaweza kuwa ni walimu makini wa njia ya amani duniani, kwani Maandiko Matakatifu yanasema, heri wenye upole maana hao watairithi nchi. Rej Mt 5:5. Huu ni wakati kwa vijana wa kizazi kipya kuwathamini, kuwajali na kuwahudumia mababu na wazee wao, kwa kuonesha huruma na upendo kwa watoto wadogo wanaoteseka kwa vita nchini Ukraine, Afghanstan na Sudan ya Kusini. Wazee wawe ni chachu ya furaha na matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo, ili wao pia waweze kuonja amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza wazee kuwa ni mafundi wa huruma ya Mungu katika ulimwengu mamboleo, kwa kuthamini tunu msingi walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Wachote amana na utajiri kutoka katika Maandiko Matakatifu; kwa kuwakumbuka na kuwaombea wote wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia, ili kweli Injili ya uhai iweze kudumishwa dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, Maadhimisho ya Siku ya Wazee na Mababu Duniani ni fursa ya kutangaza na kushuhudia kwamba, Mama Kanisa anataka kusherehekea pamoja na mababu na wazee Injili ya uhai kama njia ya kuwaenzi na kuwatunuku wazee. Siku hii ijulikane na kuadhimishwa kuanzia kwenye familia, jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na huko parokiani kwa kuwatafuta na kuwaenzi wazee wanaoishi pweke. Iwe ni siku ya kuwatembelea na kuwafariji wazee wanaoishi majumbani mwao au wale wanaotunzwa kwenye nyumba za wazee. Iwe ni fursa ya kuwatembelea na kuwajulia hali, ili kuanza ujenzi wa urafiki mpya. Kuwatembelea na kuwasaidia wazee pweke ni sehemu ya matendo ya huruma na kwa njia hii, hata wazee wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda na mafundi wa mapinduzi ya huruma, hasa kwa wazee wanaoteseka kutokana na wimbi kubwa la vita na upweke hasi, ili hatimaye, kuikomboa dunia kutokana na ghasia zote hizi.

Papa Wazee 2022

 

21 July 2022, 17:25