Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani.  

Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi ya Haramu ya Dawa za Kulevya 2022: Utu!

Biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile: kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni vitendo vyenye madhara makubwa kwa ustawi wa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar Es Salaam.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mambo haya yanapaswa kutambuliwa kama yalivyo na viongozi wote wa kidini, wanasiasa, viongozi wa kijamii na watunga sheria wa kitaifa na kimataifa! Waathirika wakuu wa janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana wa kizazi kipya wanaopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake, changamoto kwa watu wote wenye mapenzi mema kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya uzalishaji, uchakataji, usambazi na matumizi haramu ya dawa hizi sehemu mbali mbali za dunia. Ni dhamana pevu kwa serikali kuhakikisha kwamba, zinapambana kufa na kupona na biashara pamoja na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuwashughulikia kisheria wale wote wanaoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo miongoni mwa vijana!

Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya waathirika wakuu ni vijana
Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya waathirika wakuu ni vijana

Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na kwamba, vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hili, kiasi cha kupoteza maana ya maisha. Kutokana na changamoto hizi, Mama Kanisa anapenda kujipambanua katika masuala haya, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Utu wa binadamu ndiyo msingi wa Injili ya huruma ya Mungu. Ni kutokana na msingi huu, Wakristo wanapaswa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji ili kusaidia mchakato wa kuzuia, kuganga na kuponya magonjwa yanayotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, Kanisa linataka kumweka binadamu kuwa ni kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Mama Kanisa ataendelea kushirikiana na kushikamana na wadau sehemu mbali mbali za dunia katika kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu. Ushindi dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano kati ya taasisi, familia na sekta ya elimu katika ujumla wake.

Tangu mwaka 1989, Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni, inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani. Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupambana na dawa za kulevya na uhalifu, “United Nations Office on Drugs and Crime, UNODC” inasema, lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kupambana na biashara hii ambayo ina madhara makubwa katika afya, utawala bora, ulinzi na usalama wa raia na mali zao! Ikumbukwe kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kwa upande wake Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasisitiza viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao pamoja na masuala mengine ya kisiasa, wakemee biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar Es Salaam. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema “Tukabiliane na Changamoto za Dawa za Kulevya kwa Ustawi wa Jamii.” Mheshimiwa Majaliwa amesema wanasiasa hawana budi kutumia vikao na mikutano yao katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya. “Tumieni vikao vyenu vya ngazi mbalimbali pamoja na mikutano ya hadhara kuunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.”

Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni hatari kwa ustawi wa jamii.
Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni hatari kwa ustawi wa jamii.

Waziri Mkuu amesema viongozi wa dini wanapotekeleza jukumu lao la kutoa mafundisho ya kiroho na kukemea dhambi na uovu pia, waweke msisitizo katika kukemea biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya kwani huo ni uhalifu kama ulivyo uhalifu wa aina nyingine. Kwa upande wa wanahabari, Waziri Mkuu amewataka watumie vyombo vyao vya habari kuendelea kukemea matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Kwa upande mwingine toeni habari kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya. “Serikali yetu inafanya mambo makubwa sana tangazeni ili Wananchi wote waweze kufahamu na kwa wale walioathirika waweze kutumia huduma zinazotolewa na hatimaye wapate tiba kamili na kuendelea kuchangia nguvu kazi ya taifa letu.” Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuwalea watoto katika misingi ya maadili ili kuwaepusha na vitendo viovu ikiwemo matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. “Turejee kwenye asili yetu ambapo jamii nzima ilihusika katika malezi ya watoto na ilishirikiana katika kukemea maovu.”

“Nitumie nafasi hii kuwasihi wananchi wote wenye taarifa muhimu kuhusu wafanyabiashara wa dawa za kulevya toeni taarifa hizo katika vyombo husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema na haraka. Wasafirishaji, wauzaji na watumiaji ni sehemu ya jamii yetu, tunao ndani ya nyumba zetu. Katika hili ninawasihi tuwe na uzalendo, tutoe taarifa, tukinyamaza tutazidi kuangamiza nguvu kazi ya taifa letu.” “Kama nilivyosema hapo awali, suala la mapambano dhidi ya dawa za kulevya linahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu. Hivyo basi nazisihi pia asasi za kiraia pamoja na wasanii kuendelea kutoa elimu ya athari ya dawa za kulevya kwa kukemea bila kuchoka matumizi ya dawa hizi.” Naye, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gelard Musabila Kusaya amesema dawa za kulevya ni tatizo linaloathiri maendeleo ya jamii hivyo wananchi wanatakiwa kushirikiana katika kudhibiti changamoto zinazotokana na matumizi ya dawa hizo. Maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha jamii kushiriki katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kwa vijana
Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kwa vijana

Amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo mwaka 2022 imetimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake imefanikiwa kudhohofisha mitandao ya dawa za kulevya nchini Tanzania pamoja kwa kukamata wafanyabiashara na kuteketeza dawa hizo. “Pia, imefanikiwa kudhibiti matumizi na athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya. “Kipekee nichukue nafasi hii kuvipongeza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano na kwa jitihada zao za kufanya kazi usiku na mchana bila kuchoka kuhakikisha tatizo la dawa za kulevya linadhibitiwa.” Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliokuwa wakitumia dawa za kulevya waliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kupambana na kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini na kuwasihi vijana wenzao kutojiingiza katika matumizi ya dawa hizo kwa kuwa madhara yake ni makubwa ikiwa ni pamoja na kutoaminika, kutengwa na familia na jamii kwa ujumla.

Dawa za Kulevya
07 July 2022, 14:11