Rais Sergio Mattarella wa Italia Kumbukizi la Miaka 81 ya Kuzaliwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 23 Julai 2022 amemtumia salam za heri na pongezi nyingi Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa kuadhimisha kumbukizi la miaka 81 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpatia fursa Rais Sergio Mattarella kuwaongoza watu wa Mungu nchini Italia kwa awamu ya pili, huduma ambayo anaendelea kuitekeleza kwa upendo na unyenyekevu mkuu, licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uongozi wake.
Rais Mattarella ni kiongozi ambaye ameonesha uthabiti na umakini katika maamuzi yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia, mfano bora wa kuigwa. Baba Mtakatifu anaungana na watu wote wa Mungu kumtakia heri na fanaka Rais Sergio Mattarella wa Italia anapoadhimisha kumbukizi la Siku yake ya Kuzaliwa. Mwishoni, mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko amempatia Rais Sergio Mattarella baraka zake za Kitume.