Tafuta

Papa Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya kuwa ni chachu ya mageuzi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Papa Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya kuwa ni chachu ya mageuzi, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. 

Papa Francisko: Utume wa Vijana Katika Kuleta Mageuzi Duniani

Lengo la jukwaa hili ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kushiriki na kuchangia mawazo yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kati ya mada ambazo zinachambuliwa ni pamoja na mazingira nyumba ya wote; athari za mabadiliko ya tabianchi, sera za ushirikiano wa mambo ya nchi za nje Barani Ulaya, demokrasia pamoja na fursa ya kuzungumza na viongozi mubashara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bunge la Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa Czech, kuanzia tarehe 11-13 Julai 2022 linaendesha Mkutano wa Kwanza wa Vijana mjini Prague, kwa kuwahusisha wanafunzi kutoka shule za sekondari, taasisi za elimu ya juu pamoja vyuo vikuu, ili kujadiliana kuhusu hatima ya Bara la Ulaya kwa Siku za Usoni. Lengo la jukwaa hili ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kushiriki na kuchangia mawazo yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kati ya mada ambazo zinachambuliwa ni pamoja na mazingira nyumba ya wote; athari za mabadiliko ya tabianchi, sera za ushirikiano wa mambo ya nchi za nje Barani Ulaya pamoja na demokrasia. Hii ni fursa kwa vijana kuweza kuzungumza moja kwa moja na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Mkutano wa Kwanza wa Vijana mjini Prague, anawataka vijana kufanya mabadiliko makubwa ili kulipyaisha Bara la Ulaya, utume wa vijana wa Bara la Ulaya, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” uliotiwa mkwaju hapo tarehe 15 Oktoba 2020. Amewaalika vijana kujisomea Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Waraka wa Kichungaji wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.”

Vijana wawe ni chachu ya mabadiliko makubwa duniani: amani
Vijana wawe ni chachu ya mabadiliko makubwa duniani: amani

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana wa kizazi kipya kulipyaisha Bara la Ulaya ili liondokane na uzee, kwa kutokubali kuzamishwa kwenye itikadi zinazokwenda kinyume cha maadili na utu wema; wajenge utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa njia ya kujitolea ili kuwasaidia wahitaji zaidi, pamoja na kuendelea kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Vijana wajenge utamaduni wa kujifunza kwa bidi, juhudi na maarifa, wakiwa na mwelekeo mpana kwa mambo ya mbeleni. Huu ndio utume mpana kwa vijana wa kizazi kipya Barani Ulaya. Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi katika ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa maboresho ya elimu. Huu ni mwaliko kwa jamii kujenga utamaduni wa usikivu kwa vijana wa kizazi kipya; wadumishe: mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ukarimu na mafungamano ya kijamii yanayowawezesha kukutana na vijana wengine kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kama inavyojidhihirisha katika “Mradi wa Erasmus” na kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kujisomea Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Udugu na urafiki wa kijamii kimsingi ni dira na mwongozo wa mchakato wa ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi na unaosimikwa katika misingi ya haki, amani na utulivu, dhamana na wajibu wa: watu wote pamoja na taasisi mbalimbali. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote vita na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Waraka huu unajikita zaidi katika masuala msingi ya kijamii katika maisha ya mwanadamu. “Wote ni ndugu” ni maneno aliyokuwa anatumia Mtakatifu Francisko wa Assisi akiwataka ndugu zake watawa kuishi kadiri ya kanuni msingi za Kiinjili, kama njia ya kumwilisha upendo wa Mungu kwa binadamu, kiasi cha kujenga jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu.

Dumisheni haki na amani ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri pa kuishi
Dumisheni haki na amani ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri pa kuishi

Waraka huu pamoja na mambo mengine, unapania kuwahamasisha walimwengu kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Baba mmoja, yaani Mungu mwenyezi, licha ya tofauti zao msingi. Hapa kipaumbele cha pekee ni majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Waraka “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni nyenzo ya nguvu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na mawasililiano kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za kiikolojia zinazomwandama mwanadamu. Katika Waraka huu wa Kitume, Baba Mtakatifu Francisko kwa muhtasari anagusia mambo yanayotokea katika mazingira; Umuhimu wa kuenzi Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu pamoja na Ikolojia msingi. Baba Mtakatifu anagusia njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni umuhimu wa elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Vijana wawe mstari wa mbele kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Wawe ni wajenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza katika kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Amewataka vijana kuwatambua na kuwaenzi wafiadini, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya ukweli.

Vijana ni matumaini na jeuri ya Kanisa
Vijana ni matumaini na jeuri ya Kanisa

Wosia wa Kitume wa Baba Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi,” unawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwaalika vijana wa kizazi kipya kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa ajili ya jirani zao. Baba Mtakatifu anawataka vijana wawe na uwezo wa kuchangia mawazo mapya, kuwa na maono mapana zaidi katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Wawe wakarimu na watu wenye upendo wa dhati unaomwilishwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Utu, heshima, haki, amani na uhuru kamili vitawale kati ya watu!

Utume wa vijana
12 July 2022, 16:19