Tafuta

Papa Francisko Uchoyo Na Uchu wa Mali Ni Magonjwa Hatari Sana

Papa: Uchoyo na ubinafsi ni kati ya magonjwa yanayopekenyua kwa kiasi kikubwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uchoyo ni chanzo kikuu cha vita, migogoro na kinzani zinazotumia rasilimali kubwa kwa ajili ya masilahi ya watu wachache katika jamii. Kuendelea na kushamiri kwa biashara ya silaha duniani ni matokeo ya uchoyo, ubinafsi, na uchu wa mali na madaraka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, zinaonesha kwamba, kuna chakula cha kutosha kuzima baa la njaa duniani, lakini kutokana na uchoyo, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka pamoja na utandawazi wa kutowajali wengine, matokeo yake ni ongezeko kubwa la watu wanaopekenyuliwa na baa la njaa duniani. Umaskini wa hali na kipato, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; ukosefu wa demokrasia na haki msingi za binadamu; uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote pamoja na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya vyanzo vya baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Chanzo cha mambo yote haya ni uchoyo unaoendelea kuchochea hofu, tamaa na kuporomoka kwa tunu msingi za kijamii na maovu kuzidi kushamiri duniani. Shida kubwa ya uchoyo na ubinafsi ni kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kudhani kwamba, kwa kuwa na utajiri na mali nyingi mtu anaweza “kula kuku kwa mrija” na kusahau mateso na mahangaiko ya duniani. Uchoyo na ubinafsi unaendelea kuzamisha mizizi yake hata katika maisha ya familia nyingi leo hii. Kuna watu wa familia moja wanaendelea kugombana, hawasalimiani na wala hawataki kuonana kwa sababu ya mali ya urithi!

Uchu wa mali na madaraka pamoja na uchoyo ni magonjwa hatari sana kwa jamii
Uchu wa mali na madaraka pamoja na uchoyo ni magonjwa hatari sana kwa jamii

Kristo Yesu katika Injili ya Dominika ya 18 ya Mwaka C wa Kanisa anazama zaidi katika chanzo cha misiba na maafa yote haya yanayomsibu mwanadamu kwa kuonya kuhusu matumizi ya mali za dunia pamoja na mfano wa tajiri mpumbavu akisema “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo” Lk 10: 15. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 31 Julai 2022, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mara baada ya kurejea kutoka kwenye hija yake ya kitume ya 37 Kimataifa huko nchini Canada alikokwenda kama hujaji wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kufafanua maana ya uchoyo “Cupiditas, cupidigia, cupidity, greed & avarice” ambao kimsingi ni ugonjwa hatari sana katika jamii kwa sababu ya uchu wa kutaka kumiliki mali na utajiri, hali ambayo inawageuza baadhi ya watu kuwa ni watumwa, kwa kukosa amani na utulivu wa ndani.

Mali inayopatikana kihalali ni haki ya mtu, inayomwezesha kupata mahitaji yake msingi. Fedha ni kipimo cha amana, inaeleza thamani ya bidhaa au huduma inayotolewa kwa jamii. Inaonesha uwezo wa kununua bidhaa au huduma alio nayo mtu; inatunza na kuonesha uwezo wa kununulia bidhaa na huduma kwa siku za usoni. Kila mtu anahitaji fedha, lakini Mwenyezi Mungu anawaalika waja wake kutoa kipaumbele cha kwanza kwake. Uhuru wa ndani unamtaka mwamini ajinasue kutoka katika mambo na tabia ambazo zinakwenda kinyume na nidhamu ya maisha ya kiroho. Ni changamoto ya kuwa ni mtu wa kiasi, mwenye matumizi sahihi ya fedha na mali na kwa namna ya pekee, kuwa na maadili kuhusu matumizi ya faida ya fedha. Myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa na madhara yake ni matokeo ya kukosa nidhamu katika matumizi ya sera za fedha duniani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, fedha ni thamani inayowekwa katika kitu chochote ambacho unahitaji, fedha badala ya kutumika kama chombo, inaweza kukugeuza na kuwa ni mtumwa.

Uchu wa mali na madaraka vimewageuza watu kuwa watumwa
Uchu wa mali na madaraka vimewageuza watu kuwa watumwa

Uchoyo na ubinafsi ni kati ya magonjwa yanayopekenyua kwa kiasi kikubwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Uchoyo ni chanzo kikuu cha vita, migogoro na kinzani zinazotumia rasilimali kubwa kwa ajili ya masilahi ya watu wachache katika jamii. Kuendelea na kushamiri kwa biashara ya silaha duniani ni matokeo ya uchoyo, ubinafsi, na uchu wa mali na madaraka. Ikumbukwe kwamba, kila mtu ana kiasi fulani cha uchoyo na ubinafsi! Lakini fedha, mali na utajiri ambao Mwenyezi Mungu anamkirimia mtu kwa njia ya halali, isaidie kunogesha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Watu wajifunze kuwa na nidhamu ya kutafuta na kutumia fedha na mali kwa uaminifu na uadilifu na kamwe mambo haya yasigeuzwe kuwa ni ibada na sanamu za kuabudiwa na kutukuzwa, kiasi hata cha kuchukua nafasi ya Mwenyezi Mungu katika maisha.

Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anaonya kuhusu udanganyifu wa fedha na wema wa kweli akisema “Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.” Lk 16:13. Matumizi mabaya ya fedha, mali na utajiri ni kumchukiza Mwenyezi Mungu, hii ndiyo ibada ya sanamu. Ni vyema kutamani kupata utajiri kadiri ya mapenzi ya Mungu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utajiri kwani ni chemchemi ya upendo, ni mwingi wa huruma, rehema na baraka. Utajiri wa Mungu una waambata na kuwanufaisha wote pasi na ubaguzi; ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani. Kuhusu utajiri na mali za dunia hii, Kristo Yesu “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Lk 12: 15.

Jiwekeeni hazina mbinguni
Jiwekeeni hazina mbinguni

Uzima wa mtu unategemea mahusiano na mafungamano mema aliyo nayo mwamini na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwachangamotisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kutafakari na kuamua ni urithi gani wanaotaka kuwaachia wengine? Kitita cha fedha Benki? Vitu vya kimwili au majirani wenye furaha, amani na utulivu; kwa kazi njema ambazo zimewagusa wengi, kiasi cha kuwakuza na kuwakomaza. Bikira Maria Mama wa Mungu awasaidie waamini kutambua amana na utajiri wa kweli katika maisha, mambo yanayodumu milele yote!

Papa Fedha

 

 

31 July 2022, 15:16

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >