Tafuta

Papa Francisko: Njia ya Ukatekumeni Mpya: Mwaliko wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda sanjari na utamaduni wa imani moja inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Papa Francisko: Njia ya Ukatekumeni Mpya: Mwaliko wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda sanjari na utamaduni wa imani moja inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. 

Nia ya Ukatekumeni Mpya: Uinjilishaji na Utamadunisho wa Imani Moja Kwa Kristo Yesu

Papa Francisko amewataka wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kuinjilisha tamaduni mbalimbali kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili zinazobubujika kutoka katika imani moja kwa Yesu na Kanisa lake. Wawe wasikivu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kweli waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu na Kanisa la Mwanzo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Njia ya Ukatekumeni Mpya ilianzishwa kunako mwaka 1968 huko Madrid, nchini Hispania. Wanachama wake wa kwanza ni watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini pamoja na changamoto mbalimbali walizokumbana nazo katika maisha. Njia ya Ukatekumeni Mpya ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto iliyotolewa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Paulo VI, akiwataka wanachama hawa kukita maisha yao katika ukweli wa maisha ya Kikristo, chemchemi ya furaha, matumaini na ushuhuda. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, akawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu wa kimisionari, akiwataka pia kulea na kukuza miito ya kimisionari. Mtakatifu Yohane Paulo II akatambua na kuandika kwamba, asili ya chama hiki cha kitume cha Njia ya Ukatekumeni Mpya ni mwendelezo wa mchakato wa majiundo makini ya kikatoliki, muhimu sana kwa watu wa Mungu kwa nyakati hizi. Mtakatifu Yohane Paulo II akawataka Maaskofu kuthamini mchango na huduma iliyokuwa inatolewa na wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Njia hii inapata chimbuko lake katika Neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa na Maisha ya Kijumuiya yanayosaidia kurutubisha na kujenga udugu na ukomavu wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, imani ambayo inapaswa kumwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji.

Njia ya Ukatekumeni mpya ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Njia ya Ukatekumeni mpya ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Huu ni uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa, changamoto iliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ikapokelewa kwa moyo wa shukrani na unyenyekevu mkuu na Askofu mkuu Casimiro Morcillo wa Jimbo kuu la Madrid kwa wakati ule na hatimaye, kama moshi wa ubani, Njia ya Ukatekumeni Mpya ikaenea pole pole na harufu yake kuijaza Hispania hadi kufikia “miisho ya dunia.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko mpya wa kimisionari. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia waamini ari na nguvu ya kuwa kweli ni wamisionari. Waamini walei wanahamasishwa kuwa ni wamisionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; kwani ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Bwana Francisco Josè Gomes Arguello Wirtz, maarufu kama “Kiko” alijitosa bila ya kujibakiza: kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka na kwa msaada wa Roho Mtakatifu akaanzisha Njia ya Ukatekumeni Mpya, mchakato wa maisha ya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo.

Uinjilishaji na utamadunisho wa imani inayobubujika kutoka katika Utatu Mtakatifu ni muhimu.
Uinjilishaji na utamadunisho wa imani inayobubujika kutoka katika Utatu Mtakatifu ni muhimu.

Bwana Francisco Josè Gomes Arguello katika safari ya maisha yake, alitikiswa sana, hatimaye, akagundua mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto iliyomfanya kuacha yote na kuanza kuandamana na maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani mjini Roma, kuanzia tarehe 22 hadi 25 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”, Baba Mtakatifu alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya, wapatao 430, tayari kuanza utume wao sehemu mbalimbali za dunia baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Baba Mtakatifu amewataka wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kuinjilisha tamaduni mbalimbali kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili zinazobubujika kutoka katika imani moja kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wawe wasikivu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kweli waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu na Kanisa la Mwanzo. Wanatumwa kubatiza, ili Kristo Yesu aweze kuwaondolea watu dhambi zao, tayari kuunda Jamii mpya ya waamini wanaotengeneza Kanisa linalopaswa kukua na kukomaa kwa kuzingatia mila, tamaduni na amali njema za jamii.

Ushuhuda wa maisha adili na matakatifu ni nyenzo muhimu ya uinjilishaji
Ushuhuda wa maisha adili na matakatifu ni nyenzo muhimu ya uinjilishaji

Kuna tofauti ya tamaduni, lakini imani kwa Kristo Yesu inapaswa kuwa ni moja. Hii ni imani inayosimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu: Mungu Baba Muumbaji. Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Roho Mtakatifu ni Bwana na Mleta uzima, anayelitakatifuza Kanisa, na kulisaidia kukua na kukomaa. Uinjilishaji wa kina hauna budi kwenda sanjari na mchakato wa Utamadunisho, unaopaswa kutekelezwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Habari Njema ya Wokovu iwafikie watu wa Mataifa mahali popote pale walipo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukuza na kujenga ndani mwao ari na moyo wa kimisionari, tayari kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima wakiwa chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu. Wawe wanyenyekevu na watii kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watangaze na kumshuhudia Kristo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ndani pamoja na Kanisa. Wajenge na kuimarisha umoja, ushiriki na utume wao kwa Kanisa mahalia, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Waheshimu pia mamlaka za Kiserikali kwa kutenda yote kwa ujasiri na ukarimu wa Kiinjili. Wasichoke kamwe kutangaza na kushuhudia Uso wa huruma ya Baba wa milele, yaani Kristo Yesu.

Ukatekumeni Mpya

 

02 July 2022, 15:19