Tafuta

Papa Francisko: Maria Amechagua Fungu Bora: Neno la Mungu

Kristo Yesu anatambua fika mchango wa Martha katika kumkirimia, lakini Maria alikuwa amechagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang’anywa. Waamini wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kumsikiliza Kristo Yesu, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele, ambaye kwa njia ya Neno lake, mateso, kifo na ufufuko wake, amejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maandiko Matakatifu yanasema kwamba, imani inapata chimbuko lake kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, kiasi kwamba, Biblia inapaswa kuwa ni Maktaba ya kwanza kabisa kuwamo ndani ya Familia ya Kikristo, ili familia hizi ziweze kuonja uwepo angavu na endelevu wa Yesu Kristo mkombozi wa dunia katika maisha na vipaumbele vyao. Kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia, kuna maanisha ujenzi wa mchakato wa kurithisha imani inayofumbatwa katika ukimya wa Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Tafakari ya Neno la Mungu ndani ya familia inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, umeliwezesha Kanisa kuwarudishia tena waamini Biblia mikononi mwao, ili Neno la Mungu liweze kuwa ni dira, mwongozo na mwanga katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza waamini kujitaabisha: kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, wakianzia kwenye maisha ya mtu binafsi, familia, jumuiya ndogo ndogo na kwenye vyama vya kitume.

Neno la Mungu lipewe kipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa
Neno la Mungu lipewe kipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa

Tafakari makini ya Neno la Mungu inaweza kuwapatia mwanga wa imani na matumaini wanafamilia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kuna uhusiano wa pekee kati ya Neno la Mungu, Kanisa na maisha ya Ndoa na Familia, ndiyo maana Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza wanandoa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa kuwalea watoto wao kadiri ya imani na mafundisho ya Kanisa, kwani wao kimsingi ni watangazaji wa kwanza wa Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili, matakatifu na ukarimu. Kimsingi Kanisa linapaswa kuwa ni shule ya utakatifu, ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati, lakini wakati mwingine, tunu hizi zinakosekana na ushuhuda wa Kanisa unatoweka kama ndoto ya mchana! Parokia inapaswa kuwa kama familia, mahali ambapo waamini wanajifunza ukarimu na upendo kwa kusaidiana na kufarijiana kwa hali na mali. Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ameamua kukaa kati pamoja na waja wake, kumbe, uwepo wa Mungu unapaswa kushuhudiwa ndani na nje ya Kanisa. Parokia zijenge na kudumisha ukarimu kama sehemu ya mchakato wa kuwaonjesha watu wa Mungu furaha ya Injili ya Kristo Mfufuka.

Ushuhuda mkubwa uliotolewa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake ni ukaribu wake kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hawa akawarejeshea tena utu na heshima yao; akawakirimia mahitaji yao msingi; akawaponya magonjwa na hatimaye, akawaondolea dhambi zao. Ni katika muktadha huu wa usikivu makini wa Neno la Mungu pamoja na fadhila ya ukarimu inayomwilishwa katika matendo mema, imeongoza tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika ya 16 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, tarehe 17 Julai 2022. Mwinjili Luka anamwonesha Kristo Yesu akiwa ndani ya familia ya Martha, Maria na Lazaro. Maria aliketi miguuni pake Yesu akasikiliza maneno yake, lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi, kiasi cha kumwendea Yesu na kumtaka amwambie Maria aende kumsaidia kazi jikoni kama ushuhuda wa ukarimu. Lakini, Yesu akamjibu na kumwambia: “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang'anywa.” Lk 10:41-42.

Neno la Mungu liwe ni chachu ya ushuhuda wa ukarimu kuanzia kwenye familia
Neno la Mungu liwe ni chachu ya ushuhuda wa ukarimu kuanzia kwenye familia

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mara nyingi majibu ya Kristo Yesu, yanawaacha watu wengi wakiwa wamepigwa bumbuwazi. Falsafa iliyokuwa inamwongoza Martha ilikuwa, kwanza wajibu, raha baadaye! Kimsingi ukarimu unapaswa kumwilishwa katika matendo kwani mikono mitupu kamwe hailambwi, ili kweli mgeni aweze kujisikia kwamba, amepokelewa na kukaribishwa vyema. Kristo Yesu anatambua fika mchango wa Martha katika kumkirimia, lakini Maria alikuwa amechagua fungu lililo jema, ambalo hatanyang’anywa. Waamini wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kumsikiliza Kristo Yesu, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele, ambaye kwa njia ya Neno lake, mateso, kifo na ufufuko wake, amejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Neno la Mungu linapaswa kuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha, chemchemi ya furaha na matumaini mapya. Shughuli nyingine zote zinazotekelezwa na waamini zipyaishwe kwa njia ya Neno la Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujibidiisha kutafuta muda wa kusoma, kutafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao. Waamini wajenge utamaduni wa kusoma Neno la Mungu kwa furaha na hivyo kuliachia liweze kuzama taratibu katika undani wa maisha yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuianza siku yao kwa “cheche za Neno la Mungu” ili liweze kuwa ni dira na mwongozo kwa siku nzima. Bikira Maria awafunze waamini kuchagua fungu lililo jema, ambalo hawatanyang’anywa hata kidogo.

Papa: Fungu Jema
17 July 2022, 14:47

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >