Papa Francisko: CELAM Boresheni Huduma Kwa Watu wa Mungu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, utume na dhamana ya Kanisa Amerika ya Kusini una mielekeo mikuu miwili; kwanza kabisa ni mbinu mkakati wa shughuli mbalimbali za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa Amerika ya Kusini. Pili ni mwelekeo wa utekelezaji wa utume huu katika uhalisia wa maisha ya watu wa Makanisa mahalia. Utekelezaji wa majukumu ya shughuli za kichungaji unahitaji mabadiliko ya miundo mbinu ya Kikanisa kutoka katika mfumo wa sasa na kuanzisha mifumo mipya kabisa, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Huu ni mchakato unaojikita katika undani wa maisha ya waamini, unaowaalika waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kujenga na kuimarisha ndani mwao ari, mwamko na moyo wa kimissionari. Kuna changamoto kuu mbili zinazolikabili Kanisa katika mazingira ya Amerika ya Kusini; mosi ni Utume wa Kimisionari unaolichangamotisha Kanisa kufanya mabadiliko ya ndani katika maisha na utume wake, tayari kutoka kifua mbele ili kujadiliana na ulimwengu unaolizunguka.
Pili, watambue kwamba Kanisa limeanzishwa na kutumwa na Kristo Yesu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Linapaswa kuwa ni mchumba mwaminifu wa Kristo Yesu, Mhudumu wa Neno la Mungu, Mafumbo Matakatifu ya Kanisa na msimamizi wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Askofu mkuu Héctor Miguel Cabrejos Vidarte O.F.M. wa Jimbo kuu la Trujillo na Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, CELAM, kama sehemu ya kubariki na hatimaye, kuzindua Makao makuu mapya ya CELAM, hapo tarehe 12 Julai 2022, huko nchini Colombia amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu walioshiriki kikamilifu katika tukio hili muhimu la kihistoria la maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Huu ni mradi mkubwa utakaosaidia mchakato wa uinjilishaji Amerika ya Kusini, malezi na majiundo makini ya watu wa Mungu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanaendelea kujenga maisha na utume wao juu ya msingi wa Mitume na Manabii na kwamba, Kristo Yesu ndiye jiwe kuu la msingi. Re, Efe 2:20.
Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu wa CELAM kumwomba Kristo Mfufuka ili aweze kuwasaidia kutoa msukumo mpya sanjari na kuimarisha utume wa Kikanisa, tayari kusoma alama za nyakati na kupambana na changamoto mamboleo, ili hatimaye, kuwajengea watu waaminifu na watakatifu wa Mungu msingi thabiti wa imani, matumaini na mapendo. Miundo mbinu iwe ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na wala si vinginevyo. Maaskofu wa CELAM watambue kwamba, kuna vishawishi vikuu vitatu vinavyotishia njia ya watu wa Mungu Amerika ya Kusini: kwanza kabisa ni upatanisho wa maisha ya kiroho, ufahamu wa idadi ya waamini na utendaji unaowaongoza kujisimika zaidi katika ramani ya njia kuliko kuiambata njia yenyewe. Hivi ni visawishi ambavyo kamwe havina uvumilivu na daima vinalenga kuona ufanisi wa mambo peke yake.