Tafuta

Papa Francisko tarehe 20 Julai 2022 amekutana na Mfalme Albert II wa Monaco na ujumbe wake: Mkazo: Amani, Udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira Papa Francisko tarehe 20 Julai 2022 amekutana na Mfalme Albert II wa Monaco na ujumbe wake: Mkazo: Amani, Udugu wa kibinadamu na utunzaji bora wa mazingira 

Papa Francisko Akutana na Mfalme Albert II: Amani, Udugu, Utunzaji Bora wa Mazingira na UVIKO-19

Na kati ya zawadi zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mfalme Albert II pamoja na ujumbe ni: Ujumbe wa Siku 55 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2022, “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Amewazawadia kitabu cha "Statio Orbis" Kumbukumbu ya kuomba huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 20 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na Mfalme Albert II kutoka Monaco pamoja na ujumbe wake waliomtembelea mjini Vatican wakati huu wa Kipindi cha Likizo ya Kiangazi. Baba Mtakatifu pamoja na wageni wake, waliweza kuzungumza kwa faragha kwa muda wa nusu saa na baadaye, ujumbe mzima, uliweza kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu. Baadaye, walibadilishana zawadi. Na kati ya zawadi zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ni Ujumbe wa Siku 55 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2022, iliyoadhimishwa hapo tarehe 1 Januari 2022 na kunogeshwa na kauli mbiu “Elimu, Kazi Na Majadiliano Kati ya Vizazi: Nyenzo za Ujenzi wa Amani ya Kudumu.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu alikazia umuhimu wa wajumbe wa amani, majadiliano kati ya vizazi kama nyenzo ya ujenzi wa amani; mafunzo na elimu kama vikolezo vya amani; utengenezaji wa fursa za ajira unasaidia kujenga amani. Na kati ya zawadi zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ni Ujumbe wa Siku 55 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2022, “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho.

Papa Francisko amekutakana na kuzungumza na Mfalme Albert II kutoka Monaco
Papa Francisko amekutakana na kuzungumza na Mfalme Albert II kutoka Monaco

Amewazawadia pia “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kwa kuwatambua, kuwathamini na kuwaendeleza: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko anasema “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na matunda yake ni Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Malengo ya Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbalimbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Staio Orbis: Sala kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu dhidi ya UVIKO-19
Staio Orbis: Sala kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu dhidi ya UVIKO-19

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewazawadia wageni wake Kitabu maalum “Statio Orbis” cha tarehe 27 Machi 2020. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliadhimisha Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu. Tukio hili liliambatana na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kutoa baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kimya kikuu kilitawala, huku mvua ikinyeesha, Baba Mtakatifu akaongoza sala kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika kipindi hiki maalum katika historia ya mwanadamu kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Katika mapambano dhidi ya UVIKO-19, Mama Kanisa anaendelea kuwahimiza watoto wake: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbalimbali; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, bado up ona unaendelea kuwatafuna watu taratibu. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulikuwa tupu, watu wachache sana waliokuwa wanahusika na ulinzi na usalama pamoja na mawasiliano ndio walionekana katika maeneo haya. Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa imeingia katika Vita kuu ya Dunia isiyokuwa na mshindi, kwani kila mtu ameguswa na kutikiswa kwa namna yake.

Papa Monaco

 

 

21 July 2022, 16:44