Tafuta

Papa Francisko anawataka watu wa Mungu nchini DRC kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. Papa Francisko anawataka watu wa Mungu nchini DRC kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. 

DRC: Mashuhuda wa Haki, Amani, Umoja na Upatanisho wa Kitaifa!

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO linasema, tofauti zao za Kikabila ni utajiri. Ni katika umoja peke yake, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika upatanisho, watu wa Mungu nchini DRC wataweza kuisaidia nchi yao kupiga hatua kubwa ya maendeleo. Wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa unaofumbatwa katika toba & wongofu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali na kuwaombea Watu wa Mungu nchini Jamhuri ya Watu wa Congo, ili amani na upatanisho wa Kitaifa uweze kukita mizizi yake katika maisha yao. DRC ni nchi ambayo imeraruliwa kwa vita na unyonyaji mkubwa wa rasilimali na mali asilia. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Jumuiya ya watu wa Mungu kutoka DRC wanaoishi nchini Italia, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 3 Julai 2022, amewatakia amani ili iweze kuwa ni chemchemi ya furaha ya kweli. Kama wamisionari Mitume, wanaitwa na kutumwa kwenda ulimwenguni kote kutangaza Habari Njema ya Wokovu na kushiriki ujenzi wa Ufalme wa Mungu, daima wakijitahidi kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao. Ujumbe wanaotumwa kuutangaza na kuushuhudia ni amani na upatanisho, ili waweze kuvuka misigano na kinzani za mahali wanapotoka, ukanda, ukabila na udini. Mara nyingi Kanisa limekuwa mpatanishi katika mchakato wa kutafuta suluhu ya matatizo yanayoathiri amani, upatanifu wa kijamii, ardhi; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. Evangelii gaudium, 65.

Kardinali Pietro Parolin anawataka wananchi wa DRC kuwa ni mashuhuda wa haki na amani.
Kardinali Pietro Parolin anawataka wananchi wa DRC kuwa ni mashuhuda wa haki na amani.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO linasema, tofauti zao za Kikabila ni utajiri. Ni katika umoja peke yake, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika upatanisho, watu wa Mungu nchini DRC wataweza kuisaidia nchi yao kuendelea katika nyanja mbalimbali za maisha. Rej. Evangelii gaudium, 230. Amani ya kweli anasema Baba Mtakatifu Francisko ipate chimbuko lake kuanzia kwa watu binafsi, familia na kwa majirani. Waamini wajitahidi kutangaza na kushuhudia ukarimu wa Mungu kwa waja wake, kwa njia ya huruma na mapendo. Watu wateule wa Mungu wanahamasishwa kuondokana na roho ya kutaka kulipiza kisasi, bali wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa hija yake ya kitume nchini DRC kuanzia tarehe 1 – 4 Julai 2022. Akiwa nchini DRC, Kardinali Parolin, amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali ya DRC, wakiwa wanaongozwa na Rais Félix Antoine Tshilombo Tshisekedi pamoja na Waziri mkuu Jean-Michel Sama Lukande.

Kardinali Pietro Parolin, amewataka watu wa Mungu nchini DRC kujenga na kudumisha umoja wa Kitaifa kwa kuvuka mipasuko na migawanyiko inayojionesha kwa sasa. Waondokane na mapambano ya silaha yanayopelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao na hivyo kutoa mwanya kwa wajanja wachache kukwapua utajiri na rasilimali za nchi kwa mafao yao binafsi. Watu wa Mungu nchini DRC wawe ni mashuhuda na wajenzi wa haki, amani na maridhiano. Baraza la Maaskofu Katoliki Congo DRC, CENCO limekazia kwa namna ya pekee: Amani, Udugu wa Kibinadamu na furaha ya Injili. Kardinali Parolin, amewataka Maaskofu kujizatiti katika kutafuta na kudumisha amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC. Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wa Mungu nchini DRC kutokata wala kukatishwa tamaa na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika mchakato wa ujenzi wa famili inayosimikwa katika haki, amani na umoja wa Kitaifa, watambue kwamba, wao ni watoto wa Ufufuko na mashuhuda wa Matumaini.

Amani ya kweli  ianzie katika ngazi ya mtu binafsi, familia na hatimaye jamii
Amani ya kweli ianzie katika ngazi ya mtu binafsi, familia na hatimaye jamii

Itakumbukwa kwamba, Itifaki ya makubaliano kati ya Vatican na DRC ilitiwa mkwaju kunako tarehe 20 Mei 2016 na kuridhiwa na nchi hizi mbili mwaka 2020. Ni itifaki inayolitambua Kanisa Katoliki kisheria na kwamba, Kanisa linaweza kuendesha shughuli zake kwa uhuru kamili bila kuingiliwa na Serikali. Kanisa Katoliki linaweza kuchangia katika sekta ya elimu, afya pamoja na kutoa huduma za kichungaji kwa vikosi vya ulinzi na usalama. Kardinali Fridolin Ambongo, amesema, wanamgambo wenye silaha wanaopigana kule Kaskazini mwa Kivu wanatishia usalama, amani na maridhiano ya Kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO limetiliana pia saini Itifaki ya ushirikiano na Serikali ya DRC katika sekta ya elimu, afya, fedha, shughuli za kichungaji sanjari na huduma za kijamii. Haya ni makubaliano yaliyokuwa yanasubiriwa kwa muda wa miaka sita. Kardinali Pietro Parolin, amepata bahati ya kukutana na kuzungumza na wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO, ambacho kimekuwemo nchini DRC tangu mwaka 1999. Machafuko ya kisiasa Kaskazini mwa Kivu; Ukosefu wa ulinzi na usalama, changamoto ya idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji, ni kati ya mambo ambayo MONUSCO wamemwelezea Kardinali Parolin.

DRC: Umoja, amani na upatanisho

 

04 July 2022, 15:49