Tafuta

Nia za Papa Francisko kwa mwezi Julai 2022: Umuhimu wa wazee katika jamii. Nia za Papa Francisko kwa mwezi Julai 2022: Umuhimu wa wazee katika jamii. 

Nia za Papa Francisko Mwezi Julai 2022: Umuhimu wa Wazee Katika Jamii

Papa Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Julai, 2022 katika ujumbe wake kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakazia kuhusu: Umuhimu wa wazee katika jamii. Wazee ni kielelezo maalum cha mizizi na kumbukumbu hai ya jamii husika na kwamba, uzoefu na mang’amuzi; hekima na busara yao iwasaidie vijana kuwajibika barabara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uzee ni kipindi cha neema na baraka. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii. Mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Wazee ni watu ambao walikuwa ni mwamba na ngome salama wakati ambapo wajukuu wao walipokuwa wanajisikia kutofahamika, wakiogopa changamoto za maisha! Wazee wakawa wakwanza kuwakimbilia na kuwapokea kwa faraja, huku wakipangusa machozi yaliyokuwa yamefichika machoni na ndoto iliyokuwa imezama moyoni! Ni kwa njia ya huruma na upendo wa wazee, leo hii wale waliokuwa watoto sasa ni watu wazima na wanajitegemea wenyewe! Wazee waliorutubisha maisha ya watoto wao, wana kiu ya kuwaona wajukuu wao, wakiwatunza na kuwaonesha ukarimu na upendo wa dhati. Wazee wanataka kusikia uwepo wa vijana, changamoto kwao ni kuinua macho ili kuwaangalia wazee kama anavyofanya Kristo Yesu katika maisha yao!

Vijana wanapaswa kushikamana na wazee katika huduma
Vijana wanapaswa kushikamana na wazee katika huduma

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Julai, 2022 katika ujumbe wake kwa njia ya video inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakazia kuhusu: Umuhimu wa wazee katika jamii. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya wazee, kielelezo maalum cha mizizi na kumbukumbu hai ya jamii husika, ili kweli uzoefu na mang’amuzi; hekima na busara yao iwasaidie vijana wa kizazi kipya kuangalia ya mbeleni kwa matumaini na uwajibikaji. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya wazee duniani. Jambo la kusikitisha ni watu kushindwa kuishi vyema katika kipindi hiki cha uzee katika historia ya maisha ya mwanadamu. Kuna miradi mingi inayotoa huduma ya usaidizi kwa wazee, lakini ipo michache sana inayoangalia Injili ya uhai. Baba Mtakatifu anasema, wazee wanahitaji huduma bora za afya, wanahitaji muda wa kutafakari na kuonja huruma na upendo. Kwa hakika, wazee wakitunzwa vyema, wanaweza kuwa ni mashuhuda na walimu wa huruma na upendo.

Katika kipindi hiki ambacho kuna vita, kinzani na migogoro mingi, wazee wanahitaji kuona mageuzi makubwa ya huruma na upendo na kwamba, wao katika muktadha huu, wanao wajibu mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wazee kwani wao ni “chakula” kinacho rutubisha maisha yao; hekima na busara inayofichama katika jamii ya watu” ni katika muktadha huu, wazee wanapaswa kuadhimishwa, ndiyo maana anasema Mama Kanisa ameanzisha Siku ya Wazee Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Dominika ya Nne ya Mwezi Julai na kwa mwaka huu ni hapo tarehe 24 Julai 2022, yaani Dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Watazaa matunda hadi wakati wa uzee.” Zab 92:15. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea wazee ili waweze kuongoka na kuwa ni waalimu wa huruma na upendo; ili uzoefu na mang’amuzi yao, yaweze kuwasaidia wazee kuangalia ya mbeleni kwa matumaini na uwajibikaji.

Wazee wakitunzwa vyema wanakuwa ni mashuhuda na walimu wa huruma na upendo
Wazee wakitunzwa vyema wanakuwa ni mashuhuda na walimu wa huruma na upendo

Baba Mtakatifu anasema, leo hii kuna haja ya kujenga mahusiano na mafungamano mapya kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, ili kushirikishana amana na utajiri wa maisha, ili hatimaye waweze kuota ndoto ya pamoja, kwa kuvuka kinzani na mipasuko kati ya kizazi na kizazi, tayari kujiandaa kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Bila ya mwelekeo huu mpya wa maisha, matamanio hayo halali yatakufa kwa baa la njaa kutokana na kuongezeka kwa upweke hasi; uchoyo na ubinafsi, nguvu za ubaguzi na utengano. Ubinafsi ni hatari katika maisha ya kijamii. Neno la Mungu linatoa mwaliko kwa waamini kushirikishana jinsi walivyo na kile walicho nacho; yaani vijana na wazee wanaweza kushikamana. Kwani wazee wana ndoto na vijana wana unabii. Vijana ni manabii wa siku za usoni, lakini wazee ni chimbuko la historia na kamwe hawawezi kuchoka kuendelea kuota ndoto na kurithisha uzoefu na mang’amuzi yao kwa vijana wa kizazi kipya, bila kuwa ni kizingiti kwa maisha yao ya mbeleni!

Kumbe, hii ni changamoto kwa vijana wa kizazi kipya kushikamana na wazee na iwe hivyo pia kwa jamii na Kanisa katika ujumla wake. Ni wakati wa kusimama kidete kukusanya, kutunza na kuhudumia kwa upendo. Wazee ni watu wanaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii kwani ni hazina, amana na utajiri mkubwa, kwa sababu ndani mwao wanatunza kumbukumbu! Bila mizizi ya kumbukumbu hii, mwanadamu si mali kitu! Ni wajibu wa jamii kulinda maisha ya wazee, kwa kuwarahisishia matatizo na changamoto za maisha. Ni wakati wa kusikiliza, kujibu na kuwatekelezea mahitaji yao msingi, ili kamwe wasielemewe na upweke hasi. Wazee wanapaswa kulindwa ili maisha na ndoto zao, ziweze kuendelea, ili kwa siku za mbeleni, asiwepo mtu anayejuta kwa kuwa alishindwa kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kwa watu waliowapenda upeo na kuwakirimia zawadi ya maisha!

Nia za Mwezi Julai

 

04 July 2022, 15:13