Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen Shuhuda wa Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., wa Shirika la Wayesuit, aliishi na kufanya utume wake nusu ya Karne ya 17, kati ya watu waliokuwa wanaishi kijijini huko Württemberg nchini Ujerumani. Alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kiasi cha kujitahidi kuwafikia watu wa makundi yote ya kijamii. Alikuwa na ari na mwamko mkubwa wa shughuli za kichungaji, huku akisukumwa na ibada maalum kwa Bikira Maria. Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., ni mfano bora wa kuigwa katika harakati za kuwasaidia watu wengine kuonja ile furaha ya Injili. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 17 Julai 2022. Wakati huo huo, Kardinali Jean-Claude Hollerich, S.J., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Luxembourg, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Julai 2022 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., kuwa ni Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa huko mjini Ellwangen, nchini Ujerumani. Katika mahubiri yake, Kardinali Jean-Claude Hollerich, S.J., kwa namna ya pekee kabisa amekazia kuhusu imani iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., katika maisha na utume wake, kiasi kwamba, leo hii, Mama Kanisa anamtangaza kuwa ni Mtume wa Upendo kwa Mungu na jirani; upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu, chanzo cha huruma, upendo na wokovu wa mwanadamu.
Hii ni imani iliyokuwa inarutubisha maisha yake ya kila siku, kwa kuhakikisha kwamba, anajenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake. Katika mambo yote alijitahidi kuonja uwepo angavu wa Mungu na kwamba, kila sakafu ya moyo wa mwanadamu, palikuwa ni mahali patakatifu pa kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu. Dhana ya uwepo wa Mungu katika maisha Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., ilikuwa, ikakomaa na kuanza kuchanua matunda ya utakatifu wa maisha wakati wa umisionari wake; kwa njia ya tafakari ya kina ya Neno la Mungu, akaonja ufunuo wa huruma, upendo na uwepo angavu wa Mungu katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Kwa njia ya Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, akatambua mpango wa Mungu wa kutaka kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumshirikisha maisha na uzima wa milele. Takwimu zinaonesha kwamba, nusu ya wananchi wa Ujerumani ni Wakristo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha yao adili na matakatifu, yanayopaswa kupambwa kwa Neno la Mungu na maadhimisho mbalimbali ya Mafumbo ya Kanisa na kamwe wasibaki kuwa ni Wakristo wa Dominika peke yake. Kwa njia ya ushiriki mkamilifu wa madhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, waamini wataweza kujichotea furaha ya kweli na hatimaye, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili katika ulimwengu mamboleo unaoonekana kugubikwa kwa hofu na wasi wasi mkuu.
Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., aliuona Msalaba kuwa ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu na kimbilio la wokovu wa binadamu. Fumbo la Msalaba likampatia maana ya maisha yake; likawa ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani, kiasi cha kukuza upendo kwa Mungu na jirani. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, akatambua na kugundua upendo wa Mungu uliokuwa unabubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu ambao kimsingi ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele! Upendo kwa Mungu na jirani ukawa ni dira na mwongozo wa maisha, ili kujibu kilio cha maskini na wahitaji. Watu wa Mungu wakang’amua na kuonja maisha adili, matakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha ya Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ. kiasi cha kumwita “Baba Mwema.” Huu ni mwaliko kwa waamini kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mwenyezi Mungu kwa kuonesha upendo kwa jirani. Waamini wajitahidi kubeba kwa imani na matumaini Misalaba ya maisha yao, pasi na kukata wala kukatishwa tamaa. Watu wajenge tabia ya kuvumiliana, ili kukoleza amani, upendo na mshikamano wa dhati. Wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, kiini cha umisionari wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Upendo kwa Mungu na jirani, uwabidiishe watu wa Mataifa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili kwa njia ya maisha adili na matakatifu, waamini waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo Yesu kwa watu wa nyakati hizi.
Naye Padre Arturo Marcelino Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit anabainisha kwamba, Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ. Ametangazwa kuwa Mwenyeheri wakati huu, Wayesuit wanapoendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Ignas wa Loyola yanayonogeshwa na kauli mbiu “Angalieni mambo yote mapya katika Kristo.” Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola umekita mizizi yake katika Mpango Mkakati wa Maisha na Utume wao katika kipindi cha miaka kumi yaani: 2019-2029. Wayesuit wanamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya toba na wongofu wa ndani. Mwaka wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola ni fursa ya kushirikiana na wadau mbali mbali katika maisha na utume wa Wayesuit, ili kuweza kuyapatanisha yote na Kristo Yesu, anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., alikuwa ni mchapa kazi hodari, aliyetumia muda wake mwingi kwa ajili ya kutoa huduma ya maungamo kwa mahujaji, alikuwa ni mhubiri hodari na kwamba, alitoa kipaumbele cha pekee kwa kufundisha katekesi hasa kwa wanafunzi na watoto wa shule. Alikuwa ni mmisionari aliyejibidiisha kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliokuwa wamekata na kujikatia tamaa, hasa askari, wafungwa na wale waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo. Ni matumaini ya Padre Arturo Marcelino Sosa Abascal, Mkuu wa Shirika ya Wayesuit kwamba, Mwenyeheri Padre Yohanes Filippo Jeningen, SJ., ataendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Wayesuit; kwa ari na moyo wake wa kimisionari, uliomwezesha kujisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Awe ni chachu ya huduma bora kwa watu wa Mungu inayosimikwa katika upatanisho wa kweli, haki, imani na mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.