Tafuta

Hija ya mshikamano wa udugu wa upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini DRC na Sudan ya Kusini: Upatanosho na ushirika wa watu wa Mungu. Hija ya mshikamano wa udugu wa upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini DRC na Sudan ya Kusini: Upatanosho na ushirika wa watu wa Mungu. 

Mshikamano wa Papa Francisko Na Wananchi wa DRC na Sudan ya Kusini: Hija ya Kardinali Parolin

Kardinali Pietro Parolin kwa niaba ya Papa Francisko kuanzia tarehe Mosi Julai 2022 hadi tarehe 8 Julai 2022 anafanya hija ya kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini, kielelezo cha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Upatanisho wa kitaifa, haki na amani ni kati ya mambo msingi yanayopewa kipembele na Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ni sala ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Kristo Yesu, Mfalme wa amani, ili aweze kuwaondolea mateso watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini na Sudan Kongwe. Awasaidie kukoleza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, ili kukuza amali za kijamii zinazofumbatwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, maridhiano na amani katika nyoyo za watu wa Mungu Barani Afrika katika ujumla wao. Kristo Yesu, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu awasaidie watakatifu wa Mungu kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; ukomavu wa imani na mshikamano wa upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu alikuwa ametia nia ya kutembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, mjini Kinshasa na Goma tarehe 2-5 Julai 2022 sanjari na Juba, Sudan ya Kusini tarehe 5-7 Julai 2022, lakini hija hii ya kitume imesogezwa mbele hadi hapo itakapotajwa tena kutokana na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa kukabiliana na changamoto ya afya.

Mchakato wa haki, amani na umoja wa Kitaifa ni muhimu sana nchini DRC
Mchakato wa haki, amani na umoja wa Kitaifa ni muhimu sana nchini DRC

Baba Mtakatifu Dominika tarehe 3 Julai 2022 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya Jumuiya ya Watu wa Mungu kutoka DRC wanaoishi nchini Italia. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe Mosi Julai 2022 hadi tarehe 8 Julai 2022 anafanya hija ya kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini, kielelezo cha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Upatanisho wa kitaifa, haki na amani ni kati ya mambo msingi yanayopewa kipembele na Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini DRC, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” Yn 17:21. “Wote wawe na umoja” ni changamoto inayosimikwa kwenye mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko bado ametia nia ya kutembelea Sudan ya Kusini, akiwa ameambatana na viongozi wengine wakuu wa Makanisa.

Kardinali Parolin
01 July 2022, 16:41