Tafuta

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu.  

Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Waraka wa "Laudato si" Utunzaji wa Mazingira Nyumba ya Wote

Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unagusia kuhusu: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umegawanyika katika sura kuu sita: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani Duniani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na jinsi vinavyohusiana na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni kuhusu umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani, Sakramenti za Kanisa pamoja na sala. Waraka huu una mwelekeo wa umoja na mshikamano ambao unadhihirishwa na mchango uliotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiikolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya mafao ya watu wote duniani.

Utunzaji bora wa mazingira usaidie kupambana na baa la umaskini duniani
Utunzaji bora wa mazingira usaidie kupambana na baa la umaskini duniani

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya kwanza ya Waraka wa “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote anaonesha madhara makubwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira pamoja na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu unaoendelea kuleta mabadiliko makubwa katika dunia, nyumba ya wote kiasi cha kuigeza kuwa ni shimo la takataka. Hali hii inaweza kubadilishwa kwa kuwa na mwelekeo mpya wa uzalishaji unaojikita katika matumizi bora ya rasilimali ya dunia pamoja na teknolojia rafiki. Mabadiliko ya tabianchi ni janga la kimataifa anasema Papa Francisko, kama ilivyo pia haki ya maji safi na salama; yanayopaswa kutunzwa vyema kwani ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kwa ajili ya wote na kwamba, haki hii inaambata utu wa mwanadamu. Kiini cha yote haya anasema Baba Mtakatifu ni kutunza utofauti unaojitokeza katika bayianuai kwani kutokana na utunzaji mbaya wa mazingira kila mwaka kunatoweka jamii za mimea na za wanyama, ambazo kamwe watoto wetu hawataziona tena. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, kuna deni kubwa la ikolojia, kati ya Nchi za Kaskazini na zile zilizoko Kusini; zinazounganishwa kutokana na uwiano duni wa biashara. Nchi changa duniani zinaelemewa na deni la nje, hali ambayo inatumiwa sasa kama chombo cha kudhibiti maendeleo, jambo ambalo halifanyiki katika deni la kiikolojia. Kutokana na kuendelea kumong’onyoka kwa mazingira na jamii anasema Baba Mtakatifu waathirika wakuu ni maskini duniani ambao hawapewi uzito unaostahili. Kumbe, mwelekeo sahihi wa kiikolojia hauna budi kufumbatwa katika mwelekeo wa kijamii na wala si kwa kudhibiti kiwango cha watu kuzaliana; bali kuwa na mtazamo mpya juu ya ulaji wa kupindukia na tabia ya kuchagua vyakula kupita kiasi hali ambayo inaendelea sehemu nyingine za dunia. Kuna haja ya kuwa na mabadiliko katika mawazo yanayowajibisha mtu katika ulimwengu mamboleo, ili kujenga mfumo wa sheria utakaohakikisha usalama wa mifumo ya mazingira.

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya pili anasema kwamba, mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi wa pamoja unaopaswa kutunzwa na wala si kuharibiwa, kwani ni amana ya binadamu wote. Baba Mtakatifu akiongozwa na simulizi za Maandiko Matakatifu kuhusu kazi ya Uumbaji anaonesha mambo makuu matatu: binadamu na Mwenyezi Mungu, jirani na ardhi. Kila kiumbe kina nafasi yake na kinaonesha wema wa Mungu, matumizi mabaya ya viumbe wa Mungu ni kinyume cha utu wa binadamu. Utunzaji wa viumbe hai unapaswa kusindikizwa na wema na wajibu kwa ajili ya binadamu. Ndiyo maana hapa anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi na matumizi binafsi yanapaswa kuzingatia kwanza kanuni hii. Mapokeo ya Kikristo yanakazia kwa namna ya pekee mwelekeo wa kijamii zaidi kuliko masuala binafsi. Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya tatu anazungumzia utunzanji na uwajibikaji makini wa kazi ya Uumbaji. Kwa namna ya pekee, Papa Francisko anapembua kwa kina na mapana kuhusu: teknolojia, binadamu kama kipaumbele cha kwanza, kazi pamoja na mazao ya “GMO” ambayo yamerutubishwa vinasaba kwa njia bayoteknolojia. Licha ya kutambua mafanikio makubwa yaliyoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu, anaonya kwamba, wakati mwingine teknolojia, ujuzi na maarifa vimetumiwa kama nguvu ya kiuchumi na hivyo kuwanyonya watu wengine duniani.

Mazingira yanapaswa kutunzwa kama wajibu wa kimaadili
Mazingira yanapaswa kutunzwa kama wajibu wa kimaadili

Changamoto nyingine inayoendelea kuibuka ni mwelekeo wa sasa wa mwanadamu kutotambua sheria asilia, ili kuona nafasi ya binadamu duniani, ili aweze kutawala kwa kuwajibika ulimwenguni. Falsafa hii ya maisha imepelekea mwanadamu kujenga mantiki ya kutumia na kutupa; kwa kutoguswa na mahangaiko ya watu na matokeo yake ni watoto kufanyishwa kazi za suluba; kuwatelekeza wazee na kuwageuza binadamu wengine kuwa watumwa, kiasi cha kushindwa kuacha nguvu ya soko iweze kujirekebisha. Kuna biashara haramu ya binadamu na viungo vya watu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kashfa ya kuwatupa watoto ambao hawajazaliwa kwa kisingizio kwamba, hawaendani na mpango wa wazazi wao. Kutokana na changamoto zote hizi, anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kuwa ujasiri wa kufanya mageuzi ya kijamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahusiano kati ya watu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea maisha ya binadamu wote kwa sababu utunzaji wa mazingira ni kinyume kabisa cha uhalalishaji wa vitendo vya utoaji mimba, vinavyokumbatia utamaduni wa kifo.

Hapa kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kusimama kidete kulinda na kutetea kazi kwa kusema kwamba, watu wote wana haki ya kupata na kufanya kazi halali kwani kwa njia hii wanapata maana ya kuishi duniani. Msukumo wa pekee unapaswa kuelekezwa katika kuwekeza kwenye rasilimali watu badala ya kutaka kupata faida kubwa kwa njia ya mateso na mahangaiko ya watu. Watu wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na nguvu ya fedha wadhibitiwe, ili kweli uchumi huria uweze kuwanufaisha watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu anasema kwamba, mazao ambayo yamerutubishwa vinasaba kwa njia bayoteknolojia, yaani “GMO” ni suala tete kwani kwa upande mmoja ni suluhu ya changamoto za kiuchumi na kwa upande mwingine ni jambo ambalo linaendelea kuibua dhana ya uzalishaji unaomilikiwa na watu wachache ndani ya jamii. Hapa Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kufanya majadiliano ya kisayansi na kijamii kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi na kila kitu kipewe jina linalostahili.

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya nne anasema kwamba, mazingira ni chanda na pete na mafao ya wengi na kwamba, hii ni sehemu ya haki kwani mwanadamu ana mwingiliano wa pekee na mazingira na kwamba, hii ni sehemu inayozunguka maisha yake. Athari za mazingira na maisha ya kijamii zinakwenda sawa sawa na wala haziwezi kutenganishwa, kumbe hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha urafiki wa kiraia na mshikamano kati ya vizazi na vizazi ili kulinda na kutunza mazingira. Utunzaji mkamilifu ni sehemu ya mafao ya wengi, changamoto ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema kuna haja pia ya kuhakikisha kwamba, Jamii inalinda na kudumisha utajiri wa tamaduni za binadamu kama vile za jamii ya Waborigini na mazingira ya mijini, ili kufanya maboresho ya maisha ya binadamu, kwa kuheshimu pia maeneo ya wazi, makazi ya watu na usafiri mijini mambo ambayo wakati mwingine yanaathari kubwa kwa maisha ya watu. Lengo ni kuhakikisha kwamba, mwili wa mwanadamu unathaminiwa kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kuipokea dunia kama nyumba ya wote na hivyo kushinda kishawishi cha mantiki ya kutawala.

Kuna mwingiliano mkubwa kati ya mwanadamu na mazingira bora
Kuna mwingiliano mkubwa kati ya mwanadamu na mazingira bora

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya tano anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kujadiliana, ili kuamua na kutenda. Kanisa haliwezi kujidai kwamba, lina majibu ya kisayansi wala kuchukua nafasi ya kisiasa, bali linapenda kuhimiza mchakato wa majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi ili mahitaji na sera mbali mbali zisiharibu mafao ya wengi. Majadiliano ni muhimu katika masuala ya kiuchumi na kisiasa, kwa ajili ya huduma kwa maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kutoa maamuzi machungu kuhusiana na utunzaji bora wa mazingira, kuliko ilivyojitokeza miaka ya nyuma. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kuwa na utawala bora, utakaosimamia mafao ya wengi, kwa kuwekeza zaidi katika utunzaji bora wa mazingira, ili kudhibiti kuibuka tena kwa ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kuna haja ya kuangalia pia mfumo wa kutaka kulinda Mabenki ambao unapania daima kupata faida kubwa, lakini waathirika wakuu wakiwa ni wananchi wa kawaida. Kama Jumuiya ya Kimataifa haitakuwa makini kwa kudhibiti ukiritimba unaofanywa na Mabenki, watu wanaweza kukabiliwa tena na mtikisiko wa uchumi kama ilivyotokea miaka kadhaa iliyopita. Baba Mtakatifu anasema, masuala ya kisiasa na kiuchumi hayana budi kupata mwelekeo mpana zaidi badala ya kujikita katika sera zinazotaka kupata mafanikio ya muda mfupi kwa ajili ya chaguzi. Mchakato wa maamuzi makubwa kwa ajili ya mafao ya wengi hauna budi kujikita katika ukweli na uwazi pamoja na kusimama kidete kupambana na rushwa pamoja na ufisadi na mafao binafsi; mambo ambayo yana madhara makubwa katika jamii. Sera na mikakati ya kiuchumi ijikite katika kanuni maadili na masuala ya fedha yasimamiwe kwa kuzingatia ubora wa maisha ya watu. Wanaharakati mbali mbali wanapaswa kujielekeza katika utunzaji wa mazingira, utetezi wa maskini na ujenzi wa mtandao wa mshikamano unaosimikwa katika heshima na udugu.

Mazingira bora ni muhimu kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Mazingira bora ni muhimu kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya sita na ya mwisho anakazia umuhimu wa elimu na majiundo ya kweli ya mwanadamu kama moja ya changamoto kubwa katika nyakati hizi. Hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa mtindo wa maisha, kwani binadamu bado ana uwezo wakufanya marekebisho makubwa katika maisha yake katika mchakato wa ujenzi wa nyumba ya wote. Hapa kuna haja ya kuanza na mambo ya kawaida katika utunzaji wa mazingira kwa kutofautisha ukusanyaji wa taka, kuwa na matumizi bora ya maji, taa na viyoyozi, lakini zaidi kwa kuondokana na masuala ya uhalifu na ubinafsi, ili kujenga utamaduni wa kuwa na kiasi. Baba Mtakatifu anawataka watu kuwa huru kwa kujinyima anasa na kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha. Kwa njia hii, watu wote watajisikia kwamba, wanawajibika na kutegemezana katika ulimwengu huu, kwa kuwa wakweli na waaminifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia Sakramenti za Kanisa ili kuona jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anavyotumia mambo ya kawaida katika maisha ya mwanadamu kama ilivyo kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalounganisha mbingu na dunia, changamoto na mwaliko wa kuwa ni watetezi wa mazingira. Shida, mahangaiko na mapambano mbali mbali yanayojitokeza duniani, isiwe ni sababu ya kukosa furaha na matumaini, kwani katika moyo wa dunia daima upo upendo wa Mungu. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anasema “Laudato si” Sifa iwe kwako Ee Mungu Muumbaji, sala inayohitimisha Waraka wa Kitume wa kuhusu mazingira. Huu ni wimbo ulioimbwa na Mtakatifu Francisko wa Assis alipokuwa anatembea kwani baada ya maisha haya, tutakutana uso kwa uso na uzuri wa Mungu.

Laudato si 2022
13 July 2022, 16:55