Makanisa ya Kipentekoste na Kanisa Katoliki: Miaka 50 ya Majadiliano ya Kiekumene
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa pamoja wanataka kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie kutumia karama na mapaji yao kwa kujikita katika Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kuna uhusiano mkubwa kati ya mafundisho ya Makanisa ya Kipentekoste na Kanisa Katoliki kuhusiana na karama pamoja na mapaji ya Roho Mtakatifu.
Hizi ni karama zinazopaswa kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima. Karama hizi zimekuwemo ndani ya Kanisa tangu wakati wa Agano Jipya. Huu ni mwaliko wa kushikamana kwa pamoja ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni changamoto ya kutubu, kuongoka na kujipatanisha, ili Kristo Yesu aweze kuwa kweli ni Bwana na Mwalimu katika hija ya maisha ya waamini wake. Ni katika muktadha wa kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Tume ya Majadiliano ya Kiekumene Kati ya Makanisa ya Kipentekoste na Kanisa Katoliki ilipoundwa Papa Francisko amewatumia ujumbe wa pongezi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anawashukuru wadau wote wa majadiliano ya kiekumene waliojisadaka hadi kufanikisha tukio hili. Hii ni safari ya majadiliano ya tafakari ya kina, iliyoyawezesha Makanisa haya kujenga urafiki, mshikamano na maelewano.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jubilei ya Miaka 50 ya Tume hii ya pamoja, itasaidia kuimarisha kifungo cha upendo na mshikamano; ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Habari Njema ya Wokovu kama Mitume wamisionari; mintarafu jumuiya zao na jamii katika ujumla wake. Lengo ni kutekeleza agizo la Kristo Yesu, “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” Yn 17:21-23. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wajumbe wa Tume hii, watawasaidia ndugu zao katika Kristo Yesu kutambua na kuonja nguvu ya upendo, huruma na neema ya Mungu katika maisha yao.