Mahojiano Maalum na Papa Francisko: Maisha na Utume Wake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na Shirika la Habari la Argentina Tèlam yaliyodumu kwa takribani saa moja. Katika mahojiano haya, amedadavua kwa kina na mapana Janga la Ugonjwa wa UVIKO-19; Utunzaji bora wa mazingira unaosimikwa katika wongofu wa kiikolojia. Amegusia kuhusu vijana, siasa na hotuba za chuki na uhasama zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa. Vita ya Tatu ya Dunia ni matokeo ya ukosefu wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Umoja wa Mataifa na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Mwaka 2023 Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha kumbukizi la miaka 10 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Nguvu na umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii katika kukuza na kudumisha ukweli. Mwishoni, Baba Mtakatifu anayaangalia mabadiliko muhimu yanayoendelea kujitokeza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 amekuwa ni sauti ya upendo, matumaini na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Wakati watu wengi walipokuwa wanafariki dunia na hofu kutanda juu ya uso wa dunia, Serikali nyingi zilitoa kipaumbele cha kwanza kwa wananchi wao katika chanjo dhidi ya UVIKO-19. Katika hali kama hii, Bara la Afrika lilisahauliwa. Hii imekwa ni changamoto ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa imeungana na kushikamana katika udugu wa upendo, iweze kuvuka kipindi cha balaa la UVIKO-19, gonjwa ambalo halina mipaka. Lakini, Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza watu wote wa Mungu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya tiba na huduma ya afya; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kuwasahau wale ambao wamejenga ujirani mwema kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, wazee na watu waliokuwa pweke. Kipindi cha janga la UVIKO-19 si wakati wa kujitajirisha kwa maafa ya watu wengine, bali ni muda wa kujenga mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, kwa muhtasari unazungumzia mambo yanayoibuliwa katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya Ikolojia na maisha ya kiroho.Anasema, wongofu wa ikolojia ni changamoto pevu kwa ajili ya kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Anakazia umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafisishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waraka huu ni tafakari ya kina na mang’amuzi binafsi pamoja na changamoto iliyotolewa na viongozi wa Serikali ya Ufaransa, wakimsihi aandike kuhusu utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Bila kuchelewa, Baba Mtakatifu akakutana na wanasayansi wa mazingira, akawapatia changamoto ya utunzaji bora wa mazingira na kuzifanyia kazi na kuziboresha kwa chapa ya kitaalimungu. Na huo ukawa ni mwanzo wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Wongofu wa kiikolojia unatoa kipaumbele cha kwanza: Mahitaji msingi ya binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanatishia sana maisha ya mwanadamu.
Ni vijana wachache ambao wanaamua kujiunga katika medani za kisiasa, hotuba za chuki na uhasama ni hatari katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika majadiliano ya Kimataifa ili kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuachana na tabia ya kulalama kuhusu siasa chafu na viongozi dhaifu, bali wajizatiti kushiriki kikamilifu katika maboresho ya mfumo wa siasa katika nchi zao. Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi yanayowashirikisha wadau mbalimbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani. Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, haki, ustawi na maendeleo ya wengi.
Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kidini na kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa! Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, ubinafsi na uchoyo; hali ya watu kukata na kujikatia tamaa pamoja na litania ya malalamiko ni kati ya matatizo yanayomwanadamu mwanadamu, kiasi hata cha kukosa matumaini na matokeo yake, imani inayoyumba sana kutoka katika sakafu ya nyoyo za waamini. Vita ya Tatu ya Dunia inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia ni matokeo ya ukosefu wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kiburi cha mwanadamu cha kutotaka kujenga utamaduni wa kusikilizana. Tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, lakini bado ni Taasisi inayokabiliwa na changamoto pevu, kiasi hata cha wakati mwingine kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Amani duniani inahatarishwa sana kutokana na vitisho vya silaha za nyuklia na mchakato wa kuendelea kuwekeza katika biashara na matumizi ya silaha duniani.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, kinzani wala mipasuko ya kijamii bali ni matunda ya haki, maendeleo, mshikamano wa udugu wa kibinadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kuwekeza sana katika biashara na matumizi ya silaha kama inavyojionesha katika vita inayoendelea sasa kati ya Urussi na Ukraine: Mauaji ya kimbari nchini Rwanda kunako mwaka 1994. Katika kipindi cha miaka 10 vita bado inaendelea nchini Siria; Mipasuko ya ndani na kinzani nchini Lebanon bila kusahau yale yanayoendelea kujiri nchini Myanmar. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusilikiza kwa makini. Tangu baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, walimwengu bado hawajaweza kujifunza madhara yanayotokana na vita. Jambo hili linasikitisha sana. Mwezi Machi 2023 Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufanya kumbukizi la miaka 10 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, akitoa kipaumbele cha kwanza kwa: maskini, amani na mazingira, changamoto ni kutoa msukumo wa pekee kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican ni sehemu ya utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Makardinali kunako mwaka 2013. Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima.
Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, ameridhia Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Baba Mtakatifu anakaza kusema: Kipaumbele cha kwanza ni wongofu wa kimisionari, ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kanuni kuu nne zinazoweza kulisaidia Kanisa katika kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu: Wakati ni mkubwa kuliko mahali; Umoja hushinda vurugu; Mambo halisi ni muhimu kushinda fikra na kwamba, kitu kizima ni kikubwa kuliko sehemu yake. Haya ni mambo muhimu sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao na amani katika jamii. Rej. Evangelii gaudium, 217-237.
Vyombo vikubwa vya mawasiliano ya jamii, kwa sasa vinaonekana kubinafsishwa na watu wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi: kisiasa, kiuchumi na kijamii. Baba Mtakatifu anataja kanuni kuu nne zinazopata msingi wake katika: falsafa, siasa na masuala jamii, anakazia: ukweli, umoja sanjari na rasilimali muda. Mchakato wa mawasiliano ya jamii hauna budi kuangalia kinzani zinazoibuliwa, ili kuzipatia majibu muafaka, kwa wadau kuhusika kikamilifu kutoa ukweli wa mambo. Dhambi kubwa kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo ni habari za kughushi na kashfa za watu: Ukweli wa mambo na uaminifu wa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamiii ni mambo msingi katika mchakato wa mawasiliano fungamani ya binadamu. Mawasiliano ni sehemu ya mpango wa Mungu kwa binadamu na ni njia muhimu ya kung’amua na kujenga mshikamano kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wana uwezo wa kujieleza na kushirikishana ukweli, uzuri na wema. mawasiliano ya jamii ni muhimu katika huduma ya ukweli kwa kuondokana na habari potofu zinazofichama katika maamuzi ya kisiasa na azma ya kutaka kukuza mapato kiuchumi. Usambazaji wa habari potofu unatumia kwa ujanja mitandao ya kijamii na kwa mantiki ya kuhakikisha inafanya kazi.
Habari za uongo zinaweza kuenea kwa haraka sana na hivyo kuhatarisha sifa za watu wengine. Baba Mtakatifu anakazia ukweli katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili ukweli uweze kuwaweka watu huru, kwa kukazia haki na amani. Mihimi mikuu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili inapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu anasema, utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ameipokea kwa heshima kubwa. Anatambua karama na mapungufu yake ya kibinadamu anaendelea kujifunza ili kweli aweze kuwa mkarimu na Msamaria mwema. Katika hija ya maisha, kuna: wasamaria wema, akina Simoni wa Kirene, Veronika na wale wanawake wa Yerusalemu wanaoendelea kumtia shime, ili kuubeba vyema Msalaba wa huduma kwa watu wa Mungu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Anapenda kuwahimiza viongozi wote wa Kanisa wajitahidi kuwa ni wachungaji wema, wenye huruma na upendo. Katika kipindi cha maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: Fadhila ya huruma na upendo, imeendelea kukua na kuchanua kama maua ya kondeni. Amejifunza kuwa na fadhila ya uvumilivu sanjari na kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini.