Kumbukizi la Papa Francisko Kutembelea Kisiwa Cha Lampedusa Julai, 2013
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wakimbizi na wahamiaji ni neema na baraka kwa Kanisa Barani Ulaya; ni kielelezo cha umoja, ukatoliki na ushuhuda wa utume wa Kanisa, na kwamba, wanaweza kuwa ni chachu ya toba, wongofu na utakatifu wa maisha; urafiki na kama sehemu ya majadiliano ya: kitamaduni, kidini na kiekumene yanayokita mizizi yake katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma ya kichungaji kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Wakimbizi na wahamiaji wakiweza kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya nchi zinazowapatia hifadhi ni baraka na utajiri mkubwa unaoiwezesha jamii kukua na kukomaa katika mchakato wa udugu na mshikamano wa kibinadamu.
Ilikuwa ni tarehe 8 Julai 2013 kwa mara ya kwanza kabisa, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alipofanya ziara yake ya kwanza kutoka mjini Vatican ili kwenda kwenye Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa Kisiwani hapo. Itakumbukwa kwamba, vipaumbele vya Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni: Maskini, Amani na Mazingira. Baba Mtakatifu pia alipenda kusali na kuwaombea wale wote waliofariki dunia na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania na makaburi yao hayana alama wala kumbu kumbu tena! Hili ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kiasi hata cha kuanzisha Idara ya Wakimbizi na wahamiaji kwenye Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, inayowajibika moja kwa moja kwake binafsi!
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika maadhimisho ya Kumbukizi la kutembelea Kisiwa cha Lampedusa, mawazo yake bado yanawaendea maskini wanaomlilia Kristo Yesu, ili aweze kuwaokoa na shida pamoja na magumu yanayowaandama. Hawa ndio wale wanaorubuniwa kutokana na umaskini wao na baadaye kutelekezwa kwenye jangwa na utupu wa maisha! Ni watu wanaoteswa, kunyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao vinasiginwa. Ni watu wanaodharirishwa na kubakwa katika kambi na vizuizi vya wakimbizi na wahamiaji. Hawa ni wale wanaopambana na mawimbi mazito ya Bahari ya Mediterrania; watu wanaoteseka kwenye vizuizi vya wakimbizi na wahamiaji kwa muda mrefu. Hii ni mifano ya watu ambao Yesu anawataka wafuasi wake kuwaonesha upendo na huruma na hatimaye, kuwainua tena katika utu, heshima na haki zao msingi.
Inasikitisha kuona kwamba, pembezoni mwa miji mbalimbali duniani kumesheheni watu wanaotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni watu wanaotengwa na kubaguliwa; wanaonyanyaswa na kudhulumiwa; maskini, wagonjwa na wale wote wanaoteseka. Kristo Yesu, kwa njia ya Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho yake makuu, anawataka wafuasi wake kuwafariji na kuwahurumia wale wanaoteseka; kuwalisha na kuwanywesha wenye njaa na kiu ya haki; ili wasikie kutoka katika undani wa maisha yao kwamba, wanapendwa na Mungu na hatimaye, kuwaonesha njia inayowapeleka mbinguni kwa Baba.Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa si wakimbizi peke yao, bali ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kielelezo cha maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Huu ni wajibu na dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanashirikiana ili kuleta wokovu na ukombozi kwa watu hawa. Jambo hili linawezekana kwa njia ya umoja, ushirikiano na mshikamano. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma, ulinzi na ustawi wa wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni alama ya utu, shukrani na mshikamano wa dhati!