Jubilei ya Miaka 75 ya Caritas Hispania: Huduma Kwa Wengine!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Injili ya Upendo ni huruma ya Mungu inayowatafuta na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi. Mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo, wawe na ujasiri wa kujifunza kutoka katika shule ya maskini, kwani hawa ni kielelezo makini cha Madonda Matakatifu ya Yesu! Kuwahudumia kwa ari na moyo mkuu ni sawa na kukutana na Kristo Yesu kati pamoja na waja wake! Uwepo wa maskini, iwe ni chachu ya toba na wongofu wa ndani, tayari kutubu na kumwongokea Mungu ili kuachana na yale mambo yanayopelekea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mtindo na tunu msingi za Kiinjili ziwe ni dira na mwongozo wa huduma ya upendo kwa maskini, kama Mtakatifu Paulo Mtume, anavyofafanua maana ya upendo katika Utenzi wake katika Waraka wa Kwanza kwa Wakorintho 13:7. Huu ni upendo unaowaambata na kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Hawa ni walengwa wa kwanza wa mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Umoja, upendo na mshikamano wa utu na udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa.
Katika muktadha huu mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani sanjari na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa upendo na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini. Kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani, uhasama na vita. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao. Mtakatifu Paulo VI aliwahi kusema, Injili ya upendo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu ambao kwa wakati wake, utashinda chuki, kinzani na vita. Huu ni ushuhuda wa mshikamano unaotekelezwa na Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas katika ngazi mbalimbali.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Hispania “Cáritas Española” Mwaka 2022 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Miaka 75 ya Huduma Kwa Wengine.” Huu ni muhtasari wa maisha na utume wa Caritas Hispania katika kipindi chote hiki. Caritas Hispania imekuwa ni chombo cha faraja, matumaini, msaada na ujenzi wa urafiki. Maadhimisho ya Jubilei ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake. Ni wakati wa kufanya mang’amuzi kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ili kugundua njia mpya za kufuata katika kipindi hiki. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni wakati wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama kielelezo cha upendo wa mshikamano unobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2 Kor 8:9.
Huu ni mwaliko kwa Caritas kutoka nje na kuwaendea maskini ili kuwapatia huduma inayosimikwa katika maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kujali na kuthamini utu na haki zao msingi. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ya Miaka 75 ya utume wa Caritas Hispania kiwe ni kipindi cha kupyaisha huduma inayosimikwa katika Injili ya huruma na upendo sanjari na kuendeleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kweli huduma kwa maskini, iweze kuwa hai zaidi. Huduma ya upendo inapaswa kupyaishwa siku kwa siku, kwa kujenga, kudumisha na kuimarisha udugu wa kibinadamu katika ngazi mbalimbali, ili kuwa na upeo mpana zaidi. Huduma ya upendo inayotolewa na Caritas Hispania, ijitanue ili kuwafikia watu wengi zaidi, kama kielelezo na ushuhusa wa ujirani mwema, upendo na mshikamano wa kidugu.