Tafuta

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.”  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Akutana na Watu Asilia

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Kutembea Pamoja.” kama kauli mbiu ya hija yake ya kitume ni kielelezo makini cha ujasiri wa uponyaji wa madonda ya kihistoria, ili kuanza mchakato wa: Toba, wongofu wa ndani, Upatanisho wa Kitaifa na Utamadunisho wa Injili kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lengo kuu la hija ya 37 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Canada, kuanzia tarehe 24 hadi 30 Julai 2022 ni kusaidia kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, kwa kugusa madonda ya ukosefu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, mambo ambayo walitendewa watu asilia wa Canada katika maisha na historia yao. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa anataka kuomba tena msamaha unaopania kuwa ni mwanga angavu wa hija ya matumaini na upatanisho wa Kitaifa, unaofumbatwa katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu. Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Hiki ni kielelezo makini cha ujasiri wa uponyaji wa madonda ya kihistoria, ili kuanza mchakato wa: Toba, wongofu wa ndani, Upatanisho wa Kitaifa na Utamadunisho wa Injili kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Umuhimu wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kitaifa
Umuhimu wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kitaifa

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika: Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 24 Julai 2022 amewasili mjini Edmonton, Canada na kulakiwa na watu asilia wa Canada. Huu ni mwanzo wa matukio makuu katika hija hii ya kitume inayokita ujumbe wake katika toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa.

Umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa ni msingi wa amani na udugu
Umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa ni msingi wa amani na udugu

Tayari Baba Mtakatifu Francisko kuomba msamaha kutokana na madhara yaliyosababishwa na Ukoloni, Ubaguzi wa rangi na nyanyaso dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baada ya kukutana na kusalimiana na wenyeji wake, Baba Mtakatifu alielekea kwenye Seminari kuu ya St. Joseph. Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 Baba Mtakatifu anakutana na watu mahalia wa Canada na baadaye anakutana na kuzungumza na wajumbe wa Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Edmonton. Kwa upande wake, Askofu mkuu Richard Smith wa Jimbo kuu la Edmonton, Canada anasema, Baba Mtakatifu yuko kati pamoja na watu asilia wa Canada ili kuwafunulia Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele kwa waja wake. Huu ni muda muafaka kwa Kanisa nchini Canada kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na watu asilia wa Canada, ili kuganga na kutibu madonda ya watu asilia wa Canada, tayari kujikita katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa.

Mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, ulianza mapema, tangu nyakati za hija za kitume zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kutangaza na kushuhudia: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu. Hii ni fursa ya kuwa karibu na kutembea na watu wa Mungu nchini Canada, ili kuwajengea watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Uponyaji na utakaso wa kumbukumbu ni mchakato unaopaswa kujikita katika undani wa watu binafsi na jamii katika ujumla wake, tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa, ndiyo maana watu wote wa Mungu nchini Canada wanahimizwa kutembea pamoja.

Watu asilia Canada
25 July 2022, 14:54