Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Julai 2022, alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Julai 2022, alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani”  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Ulinzi na Tunza ya B. Maria

Kama sehemu ya utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Julai 2022, alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, ili kujikabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, wakati huu anapojiandaa kwa hija yake ya Kitume nchini Canada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 22 Julai 2022, alikwenda kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, ili kujikabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, wakati huu anapojiandaa kwa hija yake ya Kitume nchini Canada. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi amini wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kweli waamini wanataka kuwa wafuasi amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Waamini wanahimizwa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria
Waamini wanahimizwa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria

Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati pamoja na watu wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa kuanzia sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini.” Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa liliadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao umewawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini.

Bikira Maria ni Mama mfariji na kimbilio la wakosefu
Bikira Maria ni Mama mfariji na kimbilio la wakosefu

Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini, asaidie watu kusambaza na kueneza wema na huruma ya Mungu kama njia ya kuganga na kuponya madonda yanayomwandama mwanadamu, tayari kusimama na kupiga moyo konde, ili kusonga mbele kwa neema na baraka ya Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kumkomboa mwanadamu kutojka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ni changamoto pia kwa waamini kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali katika maisha kwa kuwa na jicho la: huruma na huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha, imani na matumaini”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya. Bikira Maria awe ni mfano na kielelezo cha wanawawake wote ambao wamekuwa kweli ni tabernakulo ya Injili ya uhai, ili kuwaheshimu na kutambua dhamana, wito na utume wao kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hata katika ukimya wao, wanawake ni nguvu ya matumaini.

B. Maria Afya ya Warumi
22 July 2022, 16:56