Tafuta

Padre Federico Lombardi, SJ., anasema kwamba, hii ni safari ya pamoja kati ya watu asilia nchini Canada, Kanisa Katoliki nchini Canada pamoja na Baba Mtakatifu Francisko. Padre Federico Lombardi, SJ., anasema kwamba, hii ni safari ya pamoja kati ya watu asilia nchini Canada, Kanisa Katoliki nchini Canada pamoja na Baba Mtakatifu Francisko. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Uchambuzi wa Kihistoria

Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger katika makala hii anachambua kwa kina umuhimu wa hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kama sehemu ya mchakato wa ujasiri wa uponyaji wa madonda ya kihistoria, ili kuanza mchakato wa: Upatanisho wa Kitaifa na Utamadunisho wa Injili kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Padre Federico Lombardi, SJ., Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger katika makala hii anachambua kwa kina umuhimu wa hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kama sehemu ya mchakato wa ujasiri wa uponyaji wa madonda ya kihistoria, ili kuanza mchakato wa: Upatanisho wa Kitaifa na Utamadunisho wa Injili kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Padre Federico Lombardi, SJ., anasema kwamba, hii ni safari ya pamoja kati ya watu asilia nchini Canada, Kanisa Katoliki nchini Canada pamoja na Baba Mtakatifu ambaye ametia nia ya kukoleza mchakato huu. Watu asilia wa Canada wanaishi katika makundi 634 yanayozungumza lugha 50 tofauti, ambao wawakilishi wao, hivi karibuni walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Papa Francisko anapenda kusaidia mchakato wa toba, wongofu na upatanisho
Papa Francisko anapenda kusaidia mchakato wa toba, wongofu na upatanisho

Kile kinachoitwa “Ugunduzi wa Amerika ya Kusini” na Ukoloni ni kati ya mambo yaliyochangia kufifisha utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, kiasi hata cha kung’olewa kutoka katika ardhi yao asilia.Canada kama taifa lilizaliwa kunako mwaka 1867. Lakini, Mama Kanisa katika maisha na utume wake, amekuwa mstari wa mbele kutetea utu, na heshima ya binadamu kwa kupinga na kukataa mifumo yote ya ukoloni: yaani: Ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na sasa ukoloni wa kiitikadi kwa sababu mifumo yote hii inakwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anafuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetembelea nchini Canada kunako mwaka 1984, 20 Septemba 1987 na hatimaye, mwaka 2002. Baba Mtakatifu Francisko kama hujaji wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, anataka kusaidia, ili tunu hizi za Kiinjili ziweze kumwilishwa katika vipaumbele na uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu nchini Canada kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha huduma kwa watu wote wa Mungu, kumbe, toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Canada.

Shule za Makazi ya Watu kwa sehemu kubwa zilichangia sana kuenzi sera za ubaguzi wa rangi zilizosimikwa kwenye nidhamu kali, matumizi pekee ya lugha ya Kiingereza pamoja na kuongokea Ukristo. Shule hizi kwa kiasi kikubwa zilifadhiliwa na Serikali na baadhi yake kuwekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Kidini. Zilikuwa ni chache ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi na matokeo yake zikawa na msongamano mkubwa wa wanafunzi, waliojikuta wakikabiliana na lishe pamoja na afya duni; ugumu na ukali wa masomo. Ni wanafunzi waliokuwa wanafariki dunia katika mazingira ya kutatanisha na wengi wao walisumbuliwa na Ugonjwa wa Kifua Kikuu. Serikali iliwekeza kidogo sana katika maboresho ya shule hizi. Wanafunzi waliokuwa wanafariki dunia kwa ghafla walizikwa mara moja, ili kupunguza gharama na ushahidi. Lakini shuhuda nyingi zinaonesha kwamba, wanafunzi hawa walinyanyaswa pia kijinsia. Mchakato wa upatanisho wa Kitaifa ulianzishwa rasmi kunako mwaka 1991.

Ubaguzi wa rangi, chakula hafifu na mazingira yalipelekea vifo vya wanafunzi Canada
Ubaguzi wa rangi, chakula hafifu na mazingira yalipelekea vifo vya wanafunzi Canada

Jumuiya ya watu asilia wa Canada inasema kwamba, ina uthibitisho wa makaburi ya wanafunzi 215 waliozikwa kwenye shule ya “British Columbia School”, moja ya shule zilizokuwa zimetengwa ili kutoa nafasi kwa wazawa kuweza kushiriki katika maisha ya jamii nzima. Makaburi haya yamegunduliwa hivi karibuni kwenye eneo la “Kamloops Indian Residential School” iliyofanya kazi zake kuanzia mwaka 1890 hadi mwaka 1970. Hawa ni wanafunzi waliopotea katika mazingira ya kutatanisha na wazazi na walezi wao hawakupatiwa maelezo ya kutosha. Shule kama hizi zilikuwa zinaongozwa na kuendeshwa na Makanisa nchini Canada.Tume ya Haki na Upatanisho wa Kitaifa nchini Canada inasema kuna zaidi ya wanafunzi 4, 100 waliofariki dunia katika mazingira ya kutatanisha. Matukio haya anasema Padre Federico Lombardi, SJ., yameibua tena hisia za uchungu katika historia ya watu asilia wa Canada. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za watu asilia.

Mama Kanisa anataka kwa mara nyingine tena kuomba toba na msamaha kwa makosa yaliyotendeka katika historia ya watu asilia wa Canada, ili kuanza mchakato wa kuganga na kuponya madonda haya, ili kujielekeza zaidi katika upatanisho wa Kitaifa na ujenzi wa matumaini miongoni mwa watu wa Mungu nchini Canada. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mara nyingi Kanisa limekuwa mpatanishi katika kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto zinazoathiri amani, umoja na mafungamano ya kijamii, migogoro ya ardhi; Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; haki msingi za binadamu na za kiraia. Kumbe, Mama Kanisa anaposhiriki mchakato wa upatanisho wa Kitaifa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wake katika ulimwengu mamboleo. Rej. Evangelii gaudium 65. Upatanisho wa Kitaifa unakwenda sanjari na mchakato wa kuziinjilisha tamaduni, ili kuitamadunisha Injili, ili kutakasa: mila, tamaduni na desturi za watu, ili ziweze kukua na kukomaa, tayari kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Padre Lombardi
24 Julai 2022, 16:04