Tafuta

Baba Mtakatifu ametia nia ya kukutana na kuzungumza na watu asilia nchini Canada na hivyo kuchangia katika safari ya uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu ametia nia ya kukutana na kuzungumza na watu asilia nchini Canada na hivyo kuchangia katika safari ya uponyaji na upatanisho wa Kitaifa.  

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Toba na Umoja wa Kitaifa Nchini Canada: Ushuhuda

Papa ametia nia ya kukutana na kuzungumza na watu asilia nchini Canada, ili kuchangia katika safari ya uponyaji na upatanisho. Baba Mtakatifu anatambua mchango uliotolewa na Wakristo wengi katika mchakato wa utamadunisho, lakini pia kuna taasisi za kidini ambazo zilichangia sera ambazo zimekwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia Dominika tarehe 24 hadi Jumamosi tarehe 30 Julai 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Haya ni matembezi yanayohitaji kuwa na mwelekeo na lengo maalum yaani: Upatanisho unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu ametia nia ya kukutana na kuzungumza na watu asilia nchini Canada na hivyo kuchangia katika safari ya uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anatambua mchango uliotolewa na Wakristo wengi katika mchakato wa utamadunisho, lakini pia kuna taasisi za kidini ambazo zilichangia sera ambazo zimekwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Katika jitihada za kutembea pamoja, Baba Mtakatifu amekwisha kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa watu asilia wa Canada, ili kuonesha machungu yaliyogandamana na sakafu ya moyo wake na mshikamano kwa matatizo waliyokumbana nayo. Kumbe, hija hii ya kitume nchini Canada ni mchakato wa kutembea pamoja ili kukoleza uponyaji na upatanisho wa Kitaifa ambao tayari umekwisha kuanza. Kwa upande wake, Askofu mkuu Ivan Jurkovič, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Canada anabainisha umuhimu wa hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko katika kukoleza mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Canada ni nchi kubwa yenye utajiri wa watu, tamaduni, mila na desturi mbalimbali.

Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Canada 1984, 1987 na 2002
Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Canada 1984, 1987 na 2002

Kumbe, uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu katika mchakato wa wongofu, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa ni muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika sheria ya upendo, inayowataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutenda mema, wasishindwe kwa uovu, bali waushinde uovu kwa wema.  Rej. Rum 12: 21. Askofu mkuu Ivan Jurkovič, anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu anatembelea nchini Canada ambapo katika kipindi cha miaka ya hivi kumekuwepo na wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, usalama, ajira na maisha bora zaidi. Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume na maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na: fursa, matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu ni kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na udugu wa mshikamano wa dhati.

Zote hizi ni changamoto ambazo, Baba Mtakatifu anapenda kukabiliana nazo uso wa kwa uso nchini Canada. Hii ni hija inayolenga kuwa ni chemchemi ya faraja, upendo, ushirika na umoja wa udugu wa kibinadamu. Kanisa nchini Canada liko katika kipindi cha mpito na kwamba, nchi nzima ina Maaskofu 80. Pamoja na kutambua udhaifu na mapungufu yaliyojitokeza katika historia ya maisha na utume wa Kanisa nchini humo, kwa sasa Kanisa linataka kujielekeza na yale ya mbeleni kwa ari na moyo mkuu na kwamba, Kanisa linataka kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada imeandaliwa kwa kuzingatia Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha adilifu na uchaji wa Mungu. Ni mafundisho yanayochota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mchakato wa toba, wongofu na upatanisho wa kitaifa lazima usonge mbele
Mchakato wa toba, wongofu na upatanisho wa kitaifa lazima usonge mbele

Ni katika muktadha huu, tunu hizi zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni dira na mwongozo thabiti wa kufuata ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zilizojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna tofauti ya tamaduni, mila na desturi za watu, lakini imani kwa Kristo Yesu inapaswa kuwa ni moja. Hii ni imani inayosimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu: Mungu Baba Muumbaji; Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Roho Mtakatifu ni Bwana na Mleta uzima, anayelitakatifuza Kanisa, na kulisaidia kukua na kukomaa. Uinjilishaji wa kina hauna budi kwenda sanjari na mchakato wa Utamadunisho, unaopaswa kutekelezwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Habari Njema ya Wokovu iwafikie watu wa Mataifa mahali popote pale walipo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukuza na kujenga ndani mwao ari na moyo wa kimisionari, tayari kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima wakiwa chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu. Wawe wanyenyekevu na watii kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watangaze na kumshuhudia Kristo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ndani pamoja na Kanisa. Wajenge na kuimarisha umoja, ushiriki na utume wao kwa Kanisa mahalia, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mchakato wa utamadunisho usaidie kweli na tunu msingi za Kiinjili kupenya na hivyo kugusa maisha ya watu watakatifu wa Mungu. Injili isafishe, igange na kuponya misigano, kinzani na mipasuko kati ya Injili, mila desturi na tamaduni mbalimbali, ili hatimaye, imani iweze kupenya katika maisha na kukita mizizi yake katika vipaumbele vya maisha ya watu. Lengo ni kukuza na kudumisha umoja, ushiriki na utume kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Utamadunisho anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovič ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utamadunisho ni mchakato ambao viongozi wa Kanisa wanapaswa kuutumia ili kuwahamasisha waamini walei kuweza kuiishi imani kadiri ya mazingira na watu anaoishi nao; kwa kusoma alama za nyakati, tayari kuishi, kuadhimisha na kushuhudia imani yao; katika furaha na majonzi ya maisha.

Papa Francisko Hujaji wa toba, wongofu na upatanisho wa kitaifa
Papa Francisko Hujaji wa toba, wongofu na upatanisho wa kitaifa

Utamadunisho ni sanaa inayopania kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kutunza kumbukumbu ya Kristo Yesu na amana kutoka kwa wahenga, kwani hawa wamesaidia mchakato wa kurithisha imani inayojikita katika sala, upendo na maisha. Familia, Parokia na Shule zimesaidia kukuza na kuendeleza imani ambayo inaendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Waamini walei watunze kumbu kumbu hai ya imani, asili na utambulisho wao unaojikita katika Sakramenti ya Ubatizo, kielelezo cha neema ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, vita ina madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Tangu Urussi ilipoivamia Ukraine kijeshi kumekuwepo na athari kubwa sana katika medani mbalimbali za maisha ya watu katika Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na athari za kiuchumi, ambako kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta kumepelekea mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma.

Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi nyingi zinalazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili huathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi nyingi na hivyo kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu. Urussi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imesababisha bei ya chakula kuongezeka maradufu. Vita inaendelea kutishia kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi duniani. Mabilioni ya rasilimali fedha iliyokuwa inatumika katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga, maradhi na athari za mabadiliko ya nchi kwa sasa yanaelekezwa katika mapambano ya kivita huko nchini Ukraine. Hali hii imepelekea kushuka kwa kiwango cha ubora wa huduma katika sekta ya elimu, afya, mapambano dhidi ya umaskini, ustawi na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Askofu Raymond Poisson, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada "The Canadian Conference of Catholic Bishops (CCCB)” anabainisha kwamba, hii ni hija ya kitume inayokita umuhimu wake katika misingi ya toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, ili kuwarejeshea tena matumaini watu wa Mungu nchini Canada, waliokuwa wamelikatia tamaa Kanisa kutokana na udhaifu na mapungufu yaliyojitokeza katika maisha na utume wake. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anafuata nyayo za Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetembelea nchini Canada kunako mwaka 1984, mwaka 1987 na hatimaye mwaka 2002. Baba Mtakatifu Francisko kama hujaji wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, atasaidia sana, ili tunu hizi za Kiinjili ziweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu nchini Canada. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na ni chombo cha huduma kwa watu wote wa Mungu, kumbe, upatanisho wa Kitaifa ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Kiasi cha dola milioni 30 za Canada zimetengwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kama sehemu yam radi mkubwa wa utamadunisho na majadiliano ya kitamaduni. Nchini Canada kuna jumla ya Jumuiya 600 za watu asilia wa Canada na Maaskofu mahalia wanajitahidi sana kujenga ujirani mwema na wananchi hawa ili waweze kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa la Kristo.

Papa Francisko Canada
22 July 2022, 17:17