Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada huko Maskwacis. Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada huko Maskwacis. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Kumbukumbu ya Historia

Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada. Amefafanua: Kumbukumbu, athari za ukoloni katika maisha ya watu asilia wa Canada, toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa na kwamba, maneno yake katika hija hii ya toba yalete faraja kwa watu asilia wa Canada katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022, inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Hiki ni kielelezo makini cha ujasiri wa uponyaji wa madonda ya kihistoria, ili kuanza mchakato wa: Toba, wongofu wa ndani, Upatanisho wa Kitaifa na Utamadunisho wa Injili kwa kuzingatia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Jumatatu tarehe 25 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada huko Maskwacis. Katika hotuba yake amejikita zaidi katika kufafanua maana ya: Kumbukumbu, athari za ukoloni katika maisha ya watu asilia wa Canada, toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa na kwamba, maneno yake katika hija hii ya toba yalete faraja kwa watu asilia wa Canada katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu anasema, hija yake ya Kitume nchini Canada inalenga hasa kuomba msamaha na huruma ya Mungu; kuganga madonda ya kihistoria kwa toba na wongofu wa ndani na hivyo kuanza kujikita katika mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Kumbukumbu ya watoto waliofariki katika mazingira tete, inasikitisha sana kwani watoto kimsingi wanapaswa kupendwa, kuheshimiwa na kutunzwa.

Kumbukumbu ya historia yao ni amana na utajiri unaopaswa kulindwa
Kumbukumbu ya historia yao ni amana na utajiri unaopaswa kulindwa

 

Mchakato wa kutembea kwa pamoja unapania kuhakikisha kwamba, mateso na mahangaiko yaliyopita, yanasaidia kukoleza ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa haki, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Kumbukumbu ya historia na maisha yao ni amana na utajiri mkubwa unaosimikwa katika misingi ya kuwajali wengine, ukweli, ujasiri, heshima, unyenyekevu, uaminifu na busara inayomwilishwa katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya watu! Inasikitisha kuona kwamba, kumbukumbu hii ambayo inasimikwa katika tunu msingi za maisha ya kijamii imechakachuliwa na kuchafuliwa na ukoloni mkongwe ulioambatana na vifo vya kutatanisha vya watoto wa shule za makazi ya watu asilia nchini Canada. Ukoloni ulipelekea kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watoto wakateseka: kiroho, kimwili na kiutu na hivyo kuvuruga mahusiano na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika hija hii ya toba, wongofu na upatanisho wa Kitaifa, anapenda kuchukua fursa hii, kuomba msamaha kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya Wakristo walioshirikiana kikamilifu na wakoloni ili kuwanyanyasa na kuwakandamiza watu asilia wa Canada.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ameomba msamaha kwa niaba ya Kanisa, Taasisi na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume yaliyoshirikiana kwa karibu zaidi na Serikali na matokeo yake, ni kuanzishwa kwa shule za makazi ya watu asilia wa Canada, zilizotumika kuwanyanyasa na kuwadhulumu watu asilia wa Canada. Inasikitisha kuona kwamba, fadhila ya ukarimu inayobubujika kutoka katika Mafundisho ya Kanisa, iliingia mchanga kiasi kwamba, ikawa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, kinyume kabisa cha tunu msingi za Kiinjili, ambazo zingekuwa ni daraja la ujenzi wa mchakato wa utamadunisho. Matokeo yake, tunu msingi za watu asilia wa Canada, lugha, mila, tamaduni na desturi njema zilisiginwa na wakoloni, hali ambayo imeendelea kusababisha mateso na mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu hadi leo hii. Matukio yote haya ni aibu mtupu ndiyo maana anasema Baba Mtakatifu yuko kati yao kuomba msamaha, kwa ajili ya dhambi zilizotendwa na watoto wa Kanisa dhidi ya watu asilia wa Canada. Uchunguzi wa kina hauna budi kufanywa, ili ukweli ufahamike na haki iweze kutendeka na huo utakuwa ni mwanzo wa mchakato wa uponyaji wa kweli. Baba Mtakatifu katika hotuba yake ya kwanza, amekazia umuhimu wa utamadunisho ili kuziinjilisha tamaduni na kuitamadunisha Injili, wa kuheshimu utambulisho wa watu asilia wa Canada.

Upatanisho wa kitaifa ni muhimu ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa
Upatanisho wa kitaifa ni muhimu ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa

 

Huu ni ushuhuda unaofumbatwa katika hotuba, mikutano pamoja na Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” na hasa katika Waraka wake wa Kitume “Querida Amazonia” uliochapishwa mwaka 2020 baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Lengo lilikuwa ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazokidhi mahitaji ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na Habari Njema ya Wokovu! Ni Sinodi iliyojipambanua ili kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi utu na heshima ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa hauna budi kuzamisha mizizi yake katika akili na nyoyo za watu. Na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linataka kuendeleza mchakato huu katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, amepokea mialiko ya kutembelea maeneo nyeti, lakini kutokana na ufinyu wa muda haitawezekana, lakini jambo la msingi ni watu asilia wa Canada kutambua kwamba, wote anawabeba na kuwahifadhi katika sakafu ya moyo wake kwa njia ya sala na sadaka zake. Baba Mtakatifu anatambua changamoto, shida, madhara na fursa zilizopo kwa watu asilia wa Canada. Kumbe, ujumbe wake ni kwa ajili ya watu wote asilia wa Canada.Sehemu ya kwanza, amejikita katika kumbukumbu, ili kuyaangalia yaliyopita, na kuyasikitikia kwa pamoja; na kuyazamisha katika sakafu ya nyoyo zao kwa njia ya ukimya na sala; ili kuomba toba na msamaha wa dhambi tayari kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; badala ya majonzi, kuasha tena Injili ya matumaini, tayari kuanza upya katika Kristo Mfufuka, historia na maisha yanayosimikwa katika mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Ili kuweza kutekeleza yote haya, kwa hakika watu wa Mungu nchini Canada wanahitaji neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu; Nguvu na hekima kutoka kwa Roho Mtakatifu; chemchemi ya upendo na faraja.

Upatanisho ni zawadi ya Mungu kwa binadamu
Upatanisho ni zawadi ya Mungu kwa binadamu

Kwa upande wake, Chifu Wilton Littlechild, Mwakilishi wa watu asilia wa Canada, kwa ufupi amemwelezea Baba Mtakatifu Francisko historia ya maisha yao. Hawa ni baadhi ya wahanga wa nyanyaso hizi, viongozi pamoja na vijana. Kama mjumbe wa Tume ya Ukweli na Upatanisho nchini Canada, anasema, alibahatika kusikiliza ushuhuda wa watu 7, 000 kutoka katika shule za makazi ya watu asilia wa Canada. Ameelezea masikitiko yao. Ukoloni ulifyekelea mbali: lugha, tamaduni pamoja na tunu msingi za maisha ya kiroho. Wanampongeza Baba Mtakatifu kwa kuzunguma ukweli kutoka katika undani wa sakafu ya moyo waake. Wanampongeza kwa kukubali na kuitikia mwaliko wao, ili waweze kutembea kwa pamoja katika njia: Ukweli, uponyaji, upatanisho na hatimaye matumaini. Hotuba ya Baba Mtakatifu itakumbukwa na wengi kama sehemu ya mchakato wa toba, amani na wogofu wa ndani, ili hatimaye, kuganga na kuponya pamoja na kuwajengea watu matumaini.

Papa Kumbukumbu
26 July 2022, 15:45