Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Mahojiano na Kardinali Pietro Parolin
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia Dominika tarehe 24 hadi Jumamosi tarehe 30 Julai 2022 inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo kuu la hija hii ni kusaidia kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, kwa kugusa madonda ya ukosefu wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, mambo waliyotendewa watu asilia wa Canada katika historia yao. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa anataka kuomba tena msamaha unaopania kuwa ni mwanga angavu wa hija ya matumaini na upatanisho wa Kitaifa, unaofumbatwa katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kuleta utakaso wa kumbukumbu. Kwa kuguswa na mahangaiko haya, Baba Mtakatifu anataka kuonesha ukaribu wake katika mateso na mahangaiko ya watu asilia wa Canada, ili Kanisa liendelee kujizatiti katika kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika hija hii, anakutana na Kanisa mahalia nchini Canada linalokabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda. Baba Mtakatifu anataka kusali na kutembea kati pamoja na watu wa Mungu nchini Canada katika ujumla wao.
Hayo yamebainishwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News wakati huu wa hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu anaendelea kuyapatia uzito wa pekee katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii inajionesha wazi katika Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” na katika Waraka wake wa Kitume “Querida Amazonia” uliochapishwa mwaka 2020 baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Lengo lilikuwa ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazokidhi mahitaji ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na Habari Njema ya Wokovu! Ni Sinodi iliyojikita zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi utu na heshima ya binadamu!
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anataka kutembelea na kujionea mwenyewe hali ya maisha ya watu asilia wa Canada, kwa kugusa mateso ya watu hawa kwa uwepo wake angavu; kwa kusali na kutembea kati pamoja nao. Mchakato huu, ulianza tangu mwezi Aprili 2020 kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na wawakilishi wa watu asilia wa Canada. Kumbe, kiini cha hija hii ya kitume pamoja na mambo mengine ni: toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa Kitaifa, ili kuganga na kuponya majereha ya ukosefu wa haki msingi za binadamu, tayari kuanza mchakato wa udugu na matumaini; kwa kukazia tunu msingi za maisha zinazofumbatwa kwenye mila, desturi na tamaduni njema za watu asilia wa Canada. Tunu hizi anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ni pamoja na kuthamini familia, jamii; kwa kujizatiti katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mahusiano na mafungamano thabiti kati ya kizazi kimoja hadi kizazi kingine; ulinzi, heshima na huduma makini kwa wazee.
Ni katika muktadha wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Canada, familia ya watu wateule na watakatifu wa Mungu, tarehe 26 Julai 2022 wanaadhimisha pamoja Sikukuu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, ili kuenzi tunu msingi za maisha ya familia. Wazazi wake Bikira Maria, wanaonesha umuhimu wa familia kama shule ya upendo, imani na utakatifu wa maisha. Kumbukumbu hii ni muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu, kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Canada. Hawa ni mashuhuda amini wa imani. Matukio kama haya ni fursa ya kukuza na kudumisha ndani ya nyoyo za watu: faraja, upendo, huruma, imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu aliye asili ya wema na utakatifu wa maisha.
Baba Mtakatifu Francisko alitamani kuona kwamba, sherehe hii inaadhimishwa huko Edmont kwenye “Ziwa la Mtakatifu anna” “Lac Ste. Anne” ili kutoa fursa kwa wagonjwa na wale wote waliojeruhiwa kupata nafasi ya kujitakasa, tayari kuanza kutembea katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika utamadunisho na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kama kielelezo cha imani tendaji! Haya ni matembezi ya pamoja katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, tayari kukuza na kudumisha utamaduni wa kusikilizana kwa makini. Lengo ni kutangaza na kushuhidia Injili ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi. Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa kutembea katika njia ya upatanisho na uponyaji, ili kutakasa kumbukumbu, ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na Injili ya matumaini.