Tafuta

Familia ya Mungu nchini Italia inamlilia na kumwombolezea Bwana Eugenio Scalfari, moja wa nguri za tasnia ya mawasiliano ya jamii nchini Italia. Familia ya Mungu nchini Italia inamlilia na kumwombolezea Bwana Eugenio Scalfari, moja wa nguri za tasnia ya mawasiliano ya jamii nchini Italia. 

Hayati Eugenio Scalfari 6 Aprili 1924 - 14 Julai 2022: Mchango Wake Katika Tasnia ya Habari

Eugenio Scalfari alikuwa ni mtu wenye akili ya ajabu sana na ujuzi wa kusikiliza kwa makini, alikuwa jasiri, mkweli na muwazi, kiasi hata cha kuelezea hisia zake za ndani, hakukatishwa tamaa na kurasa za historia ya maisha yake, bali alionekana kuwa ni mtu mwenye matumaini makubwa kwa yale yaliyokuwa yanakuja mbeleni. Kwa hakika, alikuwa ni rafiki mwaminifu wa Papa Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bwana Eugenio Scalfari aliyezaliwa tarehe 6 Aprili 1924, huko Civitavecchia nchini Italia, amefariki dunia, tarehe 14 Julai 2022. Familia ya Mungu nchini Italia inamlilia na kumwombolezea Bwana Eugenio Scalfari, moja wa nguri za tasnia ya mawasiliano ya jamii nchini Italia aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa Saratani, akiwa na umri wa miaka 98. Alikuwa ni mwandishi wa habari mahiri, mtunzi wa vitabu na mwanasiasa. Ni muasisi mwenza wa Gazeti la L’Espresso na Muasisi binafsi wa Gazeti la Repubblica lililoanzishwa kunako mwaka 1976. Magazeti yote haya yanachapishwa kila siku nchini Italia. Baba Mtakatifu Francisko anaungana na watu wa Mungu nchini Italia kumkumbuka na kumwombea Marehemu Bwana Eugenio Scalfari ambaye katika uhai wake, alibahatika kufanya naye mahojiano ya kina. Ni Mlei aliyekuwa mwerevu sana, kiasi cha kuvutiwa na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Eugenio Scalfari alikuwa ni mtu wenye akili ya ajabu sana na ujuzi wa kusikiliza kwa makini, alikuwa jasiri, mkweli na muwazi, kiasi hata cha kuelezea hisia zake za ndani, hakukatishwa tamaa na kurasa za historia ya maisha yake, bali alionekana kuwa ni mtu mwenye matumaini makubwa kwa yale yaliyokuwa yanakuja mbeleni.

Hayati Eugenio Scalfari
Hayati Eugenio Scalfari

Kwa hakika, alikuwa ni rafiki mwaminifu wa Baba Mtakatifu Francisko, aliyetamani sana kubadilishana naye mawazo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, alikuwa na shauku ya kutaka kufahamu mambo kwa kina, ni mtu aliyeipenda na kuithamini kazi yake kama mwandishi wa habari, akawashirikisha wengi na bado watu wengi zaidi wanaendelea kushiriki katika taaluma yake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika mahojiano yake na Hayati Scalfari aliwahi kumuuliza kwanini aliamua kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi, akamwambia kwamba, alipenda kutoa vipaumbele mambo makuu matatu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, yaani; Maskini, Mazingira na Amani Duniani, mambo ambayo yanajionesha kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa maisha na katika Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium.” Katika mahojiano maalum, walikazia hasa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Eugenio Scalfari ametoa mchango mkubwa katika tasnia ya habari Italia
Eugenio Scalfari ametoa mchango mkubwa katika tasnia ya habari Italia

Haya ni mambo ambayo yameacha chapa ya kudumu katika taaluma ya Hayati Eugenio Scalfari. Alithamini sana utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyobainishwa katika Maandiko Matakatifu, akatamani kuona watu wa Mataifa wanajenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, huku wakijitahidi kuishi kwa amani na utulivu! Haya ni kati ya mambo mazito ambayo Baba Mtakatifu Francisko anakumbuka, wakati huu, anapomwombolezea rafiki yake mpendwa Bwana Eugenio Scalfari aliyeaga dunia tarehe 14 Julai 2022 na kuzikwa Jumamosi, tarehe16 Julai 2022, mazishi ambayo yamehudhuriwa na Rais Sergio Mattarella na Waziri mkuu Mario Draghi pamoja na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Italia.

Eugenio S.

 

16 July 2022, 15:06