Tafuta

Baba Mtakatifu wakati wa Ibada ya Misa takatifu na Sala ya Malaika wa Bwana, 29 Juni 2022, ametambua, amekiri na kuwashukuru kwa uwepo na ushiriki wa ujumbe wa Kanisa la Kiorthodox. Baba Mtakatifu wakati wa Ibada ya Misa takatifu na Sala ya Malaika wa Bwana, 29 Juni 2022, ametambua, amekiri na kuwashukuru kwa uwepo na ushiriki wa ujumbe wa Kanisa la Kiorthodox.  (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Ujumbe wa Kiekumene: Ushuhuda wa Imani

Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili ni kwa kadiri ile ile, wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ujumbe wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol umeshiriki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume na miamba wa imani, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, kumekuwepo na utamaduni wa ujenzi wa umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol katika mchakato wa kukoleza na kudumisha majadiliano ya kiekumene. Uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa ufupi kabisa, huu ni uekumene wa maisha. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, unyoofu, uvumilivu na kutumikia katika upendo bila ya kujibakiza.

Ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake unapaswa kusimikwa katika umoja
Ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake unapaswa kusimikwa katika umoja

Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili ni kwa kadiri ile ile, wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Makanisa haya mawili yanatambua kwamba, Petro na Andrea walikuwa ni ndugu wamoja. Ujumbe wa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa mwaka 2022 uliowasili mjini Roma tangu tarehe 28 Juni hadi tarehe 30 Juni 2022 unaongozwa na Askofu mkuu Ihor Wladimir Getcha wa Jimbo kuu la Telmissos Job, na Mwakilishi wa Kudumu wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwenye Baraza la Makanisa ya Kiekumene na Rais mwenza wa Tume ya Pamoja ya Kiekumene Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Baba Mtakatifu wakati wa Ibada ya Misa takatifu na Sala ya Malaika wa Bwana, 29 Juni 2022, ametambua, amekiri na kuwashukuru kwa uwepo na ushiriki wao katika maadhimisho haya. Amemshukuru Patriaki Bartholomeo wa kwanza kwa ujumbe aliomtumia kama sehemu ya maadhimisho ya sherehe hii. Hii ni changamoto ya kufanya hija ya pamoja, ili kwa pamoja waweze kupandikiza mbegu ya Injili na hatimaye, kwa pamoja waweze kuwa ni mashuhuda wa udugu wa kibinadamu ulimwenguni. Watakatifu Petro na Paulo, Miamba na Mashuhuda wa Injili, wawe ni waombezi wa wa Mji wa Roma Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.

Wajumbe

 

29 June 2022, 14:59