Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani: Maaskofu wapya wanapewa Pallio Takatifu watakazo vishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican, ili kunogesha ushiriki wa watu wa Mungu. Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani: Maaskofu wapya wanapewa Pallio Takatifu watakazo vishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican, ili kunogesha ushiriki wa watu wa Mungu. 

Sherehe Ya Watakatifu Petro Na Paulo: Maaskofu Wakuu Na Pallio Takatifu

Kuna Maaskofu wakuu wapya 44 walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka 2021 hadi 2022. Kati yao kutoka Barani Afrika ni Maaskofu wakuu 9 na Kanisa la Afrika Mashariki ni Maaskofu wakuu 5 kutoka Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi, Nairobi, Kenya, Kampala, Uganda na Jimbo kuu la Gitega, Burundi. Pallio Takatifu ni kielelezo cha Yesu Mchungaji Mwema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 29 Juni ya kila mwaka anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume, Miamba wa Imani na Mashuhuda wa Upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Simoni alikuwa ni mvuvi kutoka Bethsaida na ni kati ya Mitume wa kwanza waliochaguliwa na Kristo Yesu. Rej. Mk1:16-20; Mt. 10:2 na hatimaye, kupewa jina la Petro, yaani mwamba. Kristo Yesu akampatia pia dhamana ya kuliongoza Kanisa lake. Rej. Mt. 16: 13-19; Lk 22: 31-32; Yn 21: 15-19. Paulo wa Tarso alionja huruma na upendo wa Kristo Mfufuka alipokuwa njiani kuelekea Dameski. Rej. Mdo 9: 1-19; Fil 3: 12. Paulo Mtume, baada ya wongofu wake alijisadaka kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa watu wa Mataifa, huku akitoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, aliyekuwa anaishi ndani mwake. Mtume Paulo anasema, “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1:22-23. Hiki ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani, kiini na ukweli wa historia ya wito wake, sasa anatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku akiwa ni mtu huru kabisa. Rej. Ef 3:1-4; 1 Kor 9:16; Rum 6:4 na Gal 2:20.

Pallio Takatifu ni kielelezo cha Kristo Yesu Mchungaji mwema.
Pallio Takatifu ni kielelezo cha Kristo Yesu Mchungaji mwema.

Watakatifu Petro na Paulo, Mitume kwa pamoja wameshiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia ya Kristo kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kiasi hata cha kumwaga damu yao, ambayo kwa sasa imekuwa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu humwita mtu kadiri ya hali na mazingira yake ambayo wakati mwingine, huwashangaza wanadamu. Hakuna jambo linalotendeka kwa bahati mbaya, bali kila kitu ni sehemu ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, changamoto kwa waamini ni kutekeleza mapenzi ya Mungu na kutekeleza utume ambao Mwenyezi Mungu amemwandalia kila mtu. Kwa njia ya neema na baraka zake, Mwenyezi Mungu anawaita waja wake, kumbe, ni vyema ikiwa kama watatambua neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao, kiasi cha kuwaletea mabadiliko makubwa katika maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kikristo kwa watu wa Mataifa. Neema ya Mungu ilete toba na wongofu wa ndani kwa wadhambi; ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, ili hatimaye, waweze kuona njia mpya ambao Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake!

Hii ni sherehe ambamo Maaskofu wakuu wa Majimbo makuu pamoja na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki wanapewa Pallio Takatifu watakazovishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika. Kuna Maaskofu wakuu wapya 44 walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka 2021 hadi 2022. Kati yao kutoka Barani Afrika ni Maaskofu wakuu 9 na Kanisa la Afrika Mashariki ni Maaskofu wakuu 5 kutoka Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi, Nairobi, Kenya, Kampala, Uganda na Jimbo kuu la Gitega, Burundi. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Siku kuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa Maaskofu wakuu katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume. Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu, Mapatriaki pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Ushuhuda wa ushiriki na mshikamano na Papa.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Ushuhuda wa ushiriki na mshikamano na Papa.

Baada ya mabadiliko yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wakuu wapya wanavishwa Pallio Takatifu na Mabalozi wa Vatican majimboni mwao, ili kuwashirikisha waamini wengi katika tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia! Maaskofu wakuu wapya kutoka Barani Afrika ni pamoja na:

Askofu mkuu Luzizila Kiala, Jimbo kuu la Malanje, Angola.

Askofu mkuu George Desmond Tambala, O.C.D., Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi.

Askofu mkuu Philip A. Anyolo, Jimbo kuu la Nairobi, Kenya.

Askofu mkuu Bienvenu Manamika Bafouakouahou, Jimbo kuu la Brazzaville, Congo.

Askofu mkuu Paul Ssemogerere, Jimbo kuu la Kampala, Uganda.

Askofu mkuu Jean-Paul Vescovo, Jimbo kuu la Alger, Algeria.

Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba, Jimbo kuu la Kisumu, Kenya.

Askofu mkuu Bonaventure Nahimana, Jimbo kuu la Gitega, Burundi.

Askofu mkuu Lucius Iwejuru Ugorji Jimbo kuu la Owerri, Nigeria.

Miamba wa imani
28 June 2022, 15:38