Tafuta

Ni Mitume waliopambana na kupigana vita vilivyo vizuri, mwendo wakaumaliza na imani wakaitunza. Rej. 2 Tim 4:7, changamoto kwa Maaskofu wakuu, Papa na watu wa Mungu kushuhudia Injili. Ni Mitume waliopambana na kupigana vita vilivyo vizuri, mwendo wakaumaliza na imani wakaitunza. Rej. 2 Tim 4:7, changamoto kwa Maaskofu wakuu, Papa na watu wa Mungu kushuhudia Injili.  (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Kutangaza na Kushuhudia Injili ya Kristo Kwa Mataifa

Papa Francisko amekazia: Mang’amuzi ya Fumbo la Ufufuko: Inuka na Ondoka Upesi; Kanisa la Kisinodi linapaswa kusimama na kuondoka upesi kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika: Kukesha, Kufundisha, huku kila mwamini akijitahidi kutekeleza: wito, dhamana na wajibu wake barabara. Huu ni ushiriki unaofumbatwa katika ari na mwamko wa kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, ni kumbukumbu endelevu ya ushuhuda wa Mitume wa Yesu waliomtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu hata kwa kumwaga damu yao kwa ajili ya Injili ya Kristo. Ni Mitume waliopambana na kupigana vita vilivyo vizuri, mwendo wakaumaliza na imani wakaitunza. Rej. 2 Tim 4:7. Hii ni changamoto kwa waamini wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinod linalosimikwa katika msingi wa: Umoja, Ushiriki na Utume. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani, Jumatano, tarehe 29 Juni 2022 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu: Mang’amuzi ya Fumbo la Ufufuko: Inuka na Ondoka Upesi; Kanisa la Kisinodi linapaswa kusimama na kuondoka upesi kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika: Kukesha, Kutangaza, Kufundisha, huku kila mwamini akijitahidi kutekeleza: wito, dhamana na wajibu wake barabara. Huu ni ushiriki unaofumbatwa katika ari na mwamko wa kitume.

Watakatifu Petro na Paulo ni mashuhuda na watangazaji makini wa Injili.
Watakatifu Petro na Paulo ni mashuhuda na watangazaji makini wa Injili.

Hii ni vita vizuri vinavyopania kujenga ulimwengu unaosimikwa katika msingi wa utu wema, mshikamano wa udugu wa kibinadamu pamoja na kutoa kipaumbele cha pekee kwa uwepo wa Mungu. Maaskofu wakuu waliokabidhiwa Pallio Takatifu, wanaitwa kuamka na kuondoka kwa upesi ili kuwaongoza watu watakatifu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Mtakatifu Petro baada ya kukamatwa na kufungwa wakati wa Mfalme Herode, aliokolewa na Malaika wa Bwana aliyemtaka asimame na kuondoka upesi kutoka katika usingizi wa kifo na mauti, tayari kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo na kwa namna ya pekee kabisa Jumuiya ya Kikristo, kuamka na kuondoka kwa haraka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kadiri ya mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, hii ni changamoto ya kuondokana na tabia ya mazoea na uvivu, ili kujizatiti katika mchakato wa kuyaendea mapambazuko mapya, huku wakiwa na ari na mwamko mpya wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayosimikwa katika upya wa maisha na kipaji cha ubunifu kinacho pata chimbuko lake katika Injili. Kamwe imani isiangukie katika taratibu na mazoea, kiasi cha kugeuza dini kuwa ni sherehe na ibada ya mapambano machafu na faraja inayowapaka “waamini mafuta kwa mgongo wa chupa”. Matokeo yake Ukristo unapokwa na Makleri, unageuka kuwa ni sehemu ya taratibu za kawaida na hatimaye, kuzimika “kama kibatari” na kuonekana kuwa ni mgumu sana.

Kanisa la Kisinodi linaloadhimishwa wakati hu, linapaswa kusimama na kuondoka upesi kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika: Kukesha, Kutangaza, Kufundisha, huku kila mwamini akijitahidi kutekeleza: wito, dhamana na wajibu wake barabara; kwa kuwaendea watu wote bila ubaguzi. Huu ni ushiriki unaofumbatwa katika ari na mwamko wa kitume bila ya kujiwekea kuta wala minyororo, tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuhimiza ushiriki mkamilifu chini ya maamuzi na maongozi ya Roho Mtakatifu, mhimili mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji. Kanisa linapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, ili kuwaendea watu wote na kuwakaribisha kwa furaha. Mtakatifu Paulo anasema, “nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.” 2 Tim 4:7. Muktadha huu wa vita unagusa maeneo mbalimbali ya maisha na utume wake katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni vita aliyopigana dhidi ya nyanyaso na madhulumu. Hii ni vita endelevu itakayowawezesha watu wengi zaidi waweze kumfuasa Kristo Yesu kwa ukamilifu zaidi, huku wakijitahidi kuondokana na uchoyo, ubinafsi pamoja na kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha kwa vile wanawafuata “walimu wa uwongo.” Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anawataka waamini katika ulimwengu mamboleo kuendeleza vita vilivyo vizuri: kwa kukesha, kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuzingatia Mafundisho ya Kanisa na kila mmoja, akitekeleza utume wake kadiri ya dhamana na majukumu yake ndani ya Kanisa.

Kanisa la Kisinodi kila mwamini ashiriki kikamilifu kadiri ya wito, wajibu na dhamana yake
Kanisa la Kisinodi kila mwamini ashiriki kikamilifu kadiri ya wito, wajibu na dhamana yake

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hii ndiyo dhamana na wito wa waamini wanaohimizwa kuwa ni mitume wamisionari, badala ya kulalama dhidi ya Kanisa, bali wajitoe na kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo; katika: unyenyekevu, ari na mwamko mkuu na kwa njia ya ushiriki mkamilifu, kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake, na wala hakuna mwamini yeyote anayepaswa kujihisi kuwa ni mnyonge na wala si mali kitu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni vita vizuri ya kutangaza, kushuhudia na kujenga Ufalme wa Mungu dhidi ya: uchu wa mali na madaraka; vita, kinzani, rushwa na ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na kuendelea kuishi katika ombwe na mawazo ya kufirika. Vita vilivyo vizuri vinapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na hivyo kuwashirikisha waja wake historia ya mapambano kati ya maisha na kifo; matumaini na hali ya kukata na kujikatia tamaa, hadi pale nguvu za chuki na uhasama pamoja na maangamizi zitakapokuwa zimeshindwa kabisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi uwawezeshe waamini kukoleza utakatifu wa maisha kwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Waamini wasimame kidete: kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote; kwa kupigania: haki, heshima na utu wa wafanyakazi; kwa kuboresha maisha ya wazee, wakimbizi na wahamiaji. Waamini wajizatiti kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; wawatunze na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasimame kidete kupinga uchafuzi wa mazingira, ili furaha ya Injili iweze kung’aa katika maisha ya kila mwamini. Hiki nndicho kiini cha vita vizuri. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika. Kuna Maaskofu wakuu wapya 44 walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka 2021 hadi 2022.Kati yao kutoka Barani Afrika ni Maaskofu wakuu 9 na Kanisa la Afrika Mashariki ni Maaskofu wakuu 5 kutoka Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi, Nairobi, Kenya, Kampala, Uganda na Jimbo kuu la Gitega, Burundi.

Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kiinjili hadi miisho ya dunia
Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kiinjili hadi miisho ya dunia

Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu, Mapatriaki pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema; Kristo Yesu aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Maaskofu wakuu pamoja na Mapatriaki kuungana pamoja naye katika vita vilivyo vizuri, tayari kusimama na kuondoka kwa haraka, huku wakiwa wameungana na kushikamana pamoja na watu watakatifu wa Mungu kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Miamba wa Imani
29 June 2022, 15:49