Tafuta

Papa:Mungu Utatu mmoja aoneshwe kwa matendo zaidi ya maneno!

Sherehe ya Utatu Mtakatifu sio tu zoezi la kitaalimungu,lakini ni mapinduzi ya namna yetu ya kuishi.Mungu anayeishi kwa kila mtu,anaishi kwa ajili ya mwingine,sio kwa ajili yake binafsi.Yeye anatuchangamotisha kuishi kwa ajili ya mmoja na mwingine.Mungu muumba wa maisha,aoneshwe kidogo kwenye vitabu na zaidi aoneshwe kwa njia ya ushuhuda wa maisha.Yeye ni upendo, anajionesha kwa njia ya upendo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Dominika ya sherehe ya Utatu Mtakatifu, tarehe 12 Juni 2022, Baba Mtakatifu Francisko metafakari Injili ya Siku kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican. Akianza tafakari hiyo amesema, katika siku kuu ya Utatu Mtakatifu Injili inatuwakilisha Watu wengine wawili wa kimungu ambao ni  Baba na Roho Mtakatifu. Kwa Roho anasema: kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Na kwa upande wa baba yake anasema: “Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; (Yh 16, 14-15). Hapa tunaona kuwa Roho Mtakatifu anazungumza, lakini sio mwenyewe: anatangaza Yesu na kumfunua Baba. Na kwamba Baba aliye na yote kwa sababu ni asili ya kila kitu, kutoka kwa Mwana yote aliyo nayo, hatunzi lolote kwa ajili yake pekee  na anatoa yote kwa Mwanae.

Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022

Baba Mtakatifu Francisko amesema sasa tujitazame sisi kwa kile ambacho tunazungumza na kile tulicho nacho. Tunapozungumza daima tunataka tusemwe vizuri juu yetu, na mara nyingi tunazungumza juu ya sisi wenyewe tu na kile tukifanyacho. Ni utofauti gani ulipo kulinganisha na Roho Mtakatifu ambaye anazungumza akiwatangaza wengine! Na karibu kile tulicho nacho ni jinsi gani tulivyo na wivu na ugumu wa kufanya kushirikishana na wengine, hata kwa yule anayekosa mambo msingi ya lazima! Kwa maneno tu ni rahisi, lakini baadaye kuweka kwenye matendo ya kweli ni vigumu sana, Papa amebainisha.

Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022

Kwa maana hiyo basi sherehe ya Utatu Mtakatifu sio tu zoezi la kitaalimungu, lakini ni mapinduzi ya namna yetu ya kuishi. Mungu ambaye kila mtu anaishi kwa ajili ya mwingine, sio kwa ajili yake binafsi, anatuchangamotisha kuishi kwa ajili ya mmoja na mwingine. Leo hii tunaweza kujiuliza ikiwa maisha yetu yanahakisi Mungu ambaye tunaamini: Mimi ambaye ninakiri imani kwa Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, ninaamini kweli kuwa kwa kuishi ninahitaji mmoja na mwingine, ninahitaji kujitoa kwa wengine, ninahitaji kuhudumia wengine? Ninathibitisha kwa maneno au kwa maisha?

Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022

Mungu Utatu mmoja, anapaswa aoneshwe namna hiyo, kwa matendo kwanza na baadaye maneno. Mungu muumba wa maisha, anaoneshwe kidogo kwenye vitabu na zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Yeye ambaye kama anavyoandika Mwinjili Yohane, ni upendo (1 Yh 4,16), anajionesha kwa njia ya upendo. Tufikirie watu wema, wakarimu, wapole ambao tulikutana nao. Kwa kuwakumbuka namna yao ya kufikiria na kutenda, tunaweza kuwa na uhakisi wa Mungu upendo. Na nini maana ya kupenda? Si katika kupendezwa na kufanya mema, lakini kabla ya hapo, kiini chake ni  kukaribisha wengine na kutoa nafasi ya wengine.

Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 12 Juni 2022

Ili kuweza kujua vema, tufikirie majina wa watu wa kimungu, ambao tunawataja kila mara tunapofanya ishara ya Msalaba. Kwa kila jina kuna uwepo wa mwingine. Baba kwa mfano hasingekuwa hivyo bila Mwana: na vile vile Mwana hawezi kufikiriwa yeye peke yake, lakini daima kama Mwana wa Baba. Na Roho Mtakatifu kwa mara nyingine tena ni Roho wa Baba na Mwana. Kwa kifupi Utatu unatufundisha kuwa haiwezekani kukaa bila mwingine. Baba Mtakatifu Francisko amesema sisi sio kisiwa,  bali ni ulimwengu wa kuweza kuishi sura ya Mungu, walio wazi, wenye kuhitaji wengine, na wenye kuhitaji msaada wa wengine. Na kwa maana hiyo tujiulize swali la mwisho: katika maisha ya kila siku, je hata mimi ninahakisi Utakatifu? Ishara ya Msalaba ninayofanya kila siku inabaki kuwa ishara pekee au inayonipa chachu ya namna yangu ya kuzungumza, ya kukutana, ya kujibu, ya kuhukumu na ya kusamehe? Mama, Mwana wa Baba, Mama wa Mwana, na Mchumba wa Roho atusaidie kupokea na kushuhudia katika maisha fumbo la Mungu upendo.

TAFAKARI YA PAPA KATIKA SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU 12 JUNI 2022
12 June 2022, 12:18