Papa:masikitiko ya Papa kuahirisha ziara ya Congo na Sudan Kusini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Utatu Mtakatifu tarehe 12 Juni 2022, Baba Mtakatifu Francisko akiwageukia waamini na mahujaji katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican, amesema: “ Na sasa ningependa kuwalekea watu na mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini. Marafiki wapendwa, kwa masikitiko makubwa, kutokana na matatizo ya mguu, nimelazimika kuahirisha ziara yangu kwa nchi zenu iliyokuwa imepangwa kwa siku za kwanza za Julai. Kiukweli najisikia masikitiko makubwa, kwa kulazimika kuahirisha safari hii niliyoijali sana. Naomba radhi kwa hili. Tuombe pamoja ili, kwa msaada wa Mungu na matibabu, niweze kuja kati yenu na haraka iwezekanavyo. Tunaamini!
Ikumbukwe Papa Francisko analazimika kuahirisha tarehe zilizokuwa zimepangwa za ziara yake ya Kitume barani Afrika, katika Juma la kwanza la Mwezi Julai ambalo lingemwona huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Sudan Kusini kama ilivyokuwa tayari imetolewa tarehe 10 Juni 2022 katika Ofisi za Vyombo vya habari Vatican na Msemaji wake Dk. Matteo Bruni.
Katika taarfa hiyo alikuwa amesema:“Kwa kupokea ushauri kutoka kwa Madaktari, ili kutobatilisha matokeo ya matibabu ya goti ambayo bado yanaendelea, Baba Mtakatifu Francisko kwa masikitiko amelazimika kuhairisha Ziara yake ya Kitume katika Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini, iliyokuwa inatazamiwa mnamo tarehe 2 hadi 7 Julai na tarehe nyingine itaandaliwa.”
"Mhujaji barani Afrika alitazamiwa kwenda sehemu mbili, nchini Congo katika mji Mkuu wa Kinshasa na katika mji wa Goma na wakati huo huko huko Sudan Kusini, katika Mji Mkuu Juba". Hata hivyo "kuahirisha ziara hiyo sio kuifuta", amefafanua hivyo Msemaji wa vyombo vya habari Vatican, Dk. Matteo Brun wakati akijibu maswali kwa waandishi wa habari na kwamba "kumekuwapo na matokeo mazuri katika kufanya mazoezi, hivyo madaktari wamemshauri Papa hasilazimishe sana mguu wake ambapo unaweza kurudisha nyuma hali na kupoteza unafuu alioanza kuwa nao".