Tafuta

Papa Francisko: Wito wa Kikristo Unasimikwa Katika Maamuzi Thabiti ya Maisha

Pale ambapo Wakristo wanakutana na vikwazo wafanye maamuzi mazito ya kuendelea kushuhudia na kutenda mema, sehemu nyingine ya dunia, bila kufungwa na falsafa ya kutaka kuwaridhisha watu.. Ni katika muktadha wa changamoto na magumu katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu anawaswalisha waamini, Je, katika hali na mazingira kama haya, ni yepi wanayotenda?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu anawataka wafuasi wake, kufanya maamuzi magumu katika maisha yao. Hili ni agizo alilolitoa wakati akiwa njiani kwenda mji Mtakatifu wa Yerusalemu, kama hatima ya maisha na utume wake hapa ulimwenguni. Hii ni safari ambayo ilisheheni changamoto pevu ya mateso, kifo na hatimaye ufufuko wake kwa wafu. Lakini kabla ya yote haya, akiwa njiani, Wasamaria hawakumpokea wala kumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Na wanafunzi wake Yakobo na Yohane, wakatoa ushauri kwa Kristo Yesu, ili “awashikishe adabu kwa kuwadhibu” lakini Kristo Yesu akawakanya kwa sababu hakuja ulimwenguni kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Amekuja ulimwenguni ili kuwasha moto wa upendo wa huruma ya Baba wa milele. Rej. Lk 9:51- 58. Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Kristo Yesu kwa wafuasi wake, akiwataka kuondokana na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, kusoma alama za nyakati sanjari na kupokea kwa moyo wa unyenyekevu na sadaka changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maisha na utume wao kama wafuasi wa Kristo Yesu. Wawe ni watu wenye maamuzi mazito, wanaojiaminisha mbele ya Mwenyezi, ili hatimaye, waweze kuwa na utulivu, amani ya ndani na uvumilivu, daima wakijitahidi kutenda mema.

Licha ya joto kali mjini Vatican, waamini wamehudhuria Sala ya Malaika wa Bwana: Ushuhuda
Licha ya joto kali mjini Vatican, waamini wamehudhuria Sala ya Malaika wa Bwana: Ushuhuda

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya XIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, tarehe 26 Juni 2022. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mtindo na mfumo huu wa maisha, si udhaifu, bali ni kielelezo cha ukomavu na nguvu ya ndani inayoratibu na kuongoza hasira na chuki. Hii ndiyo njia mbadala aliyotumia Kristo Yesu kwa wanafunzi wake, walipoamua kuondoka na kwenda mpaka kijiji kingine. Rej. Lk 9: 58. Pale ambapo Wakristo wanakutana na vikwazo na malango ya nyoyo za watu yamefungwa, wafanye maamuzi mazito ya kuendelea kushuhudia na kutenda mema, sehemu nyingine ya dunia, bila kufungwa na “falsafa ya kutaka kuwaridhisha watu.” Ni katika muktadha wa changamoto na magumu katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu anawaswalisha waamini, Je, katika hali na mazingira kama haya, ni yepi wanayotenda?

Wito wa Kikristo unasimikwa katika maamuzi thabiti ya maisha
Wito wa Kikristo unasimikwa katika maamuzi thabiti ya maisha

Je, wamekuwa wakitaka kujilazimisha kupendwa hata kama wanayo huzuni nyoyoni? Wakati mwingine waamini wanaweza kufikiri kwamba, bidii yao inatokana na hisia ya haki, kumbe, ni “kichaka” cha kuficha: kiburi, udhaifu na hali ya kukosa subira. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwakirimia nguvu ya kumfuasa kwa maamuzi thabiti, na kamwe wasiwe ni watu wa kutaka kulipiza kisasi, kukosa uvumilivu na saburi matatizo, magumu na changamoto za maisha zinapojitokeza katika maisha na hasa pale waamini wanapojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kueleweka! Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa tafakari yake, amewaalika waamini kumwomba Bikira Maria ili awaombee waweze kuwa na maamuzi thabiti ya kubaki wakiwa wamesimika upendo wao kwa Kristo Yesu hadi mwisho!

Wito wa Kikristo

 

26 June 2022, 14:40

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >