Tafuta

Papa Francisko amesema kila siku katika sakafu ya moyo wake, anaendelea kuwakumbuka watu wa Mungu nchini Ukraine wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Papa Francisko amesema kila siku katika sakafu ya moyo wake, anaendelea kuwakumbuka watu wa Mungu nchini Ukraine wanaoendelea kuteseka kutokana na vita.  

Papa: Madhara ya Vita Katika Ustawi, Maendeleo na Mafao ya Wengi

Papa Francisko anamwomba Mungu Mwenyezi mwingi wa huruma na mapendo, apende kufungua malango ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Ukraine na Urussi katika ujumla wao. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwasaidia watu wa Mungu nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, inapozuka, vita huwa “mauaji ya kinyama yasiyo ya lazima” na “tukio lisiloweza kurudi nyuma tena” linalohatarisha hali ya sasa ya binadamu na kutishia hali yake ya baadaye. “Hakuna kinachopotea kwa kuwa na amani, lakini kinyume chake ni kwamba kila kitu kinaweza kupotea kwa vita. Madhara yanayosababishwa na mapambano ya kutumia silaha hayawi ya kimwili tu bali pia ya kiroho. Hatimaye, vita ni “kushindwa kwa utu wa kweli wa ubinadamu wote,” “vita daima ni kushindwa kwa ubinadamu. Utafutaji wa ufumbuzi mbadala wa kutatua migogoro ya kimataifa inayohusu vita leo, limekuwa suala muhimu na linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka sana. Umuhimu huu unatokana na ukweli kwamba ule uwezo mkubwa wa kufanya uharibifu ambao hata nchi ndogo zinaweza kuwa nao na pia yale mahusiano ya karibu sana ya watu wa ulimwengu mzima, yanafanya kuwe na ugumu au kusiwe na uwezekano kabisa wa kuzuia madhara ya hiyo migogoro.” Kwa hiyo, ni jambo la muhimu kutafuta sababu za migogoro hii ya kivita hasa ile inayohusiana na masuala ya haki msingi za binadamu, umaskini na unyonyaji ambazo zinahitaji uingiliaji kati ili kuziondoa.”

Vita inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa ustawi. maendeleo na mafao ya wengi
Vita inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa ustawi. maendeleo na mafao ya wengi

Kwa hiyo, neno jingine linaloweza kutumika badala ya ‘amani’ ni maendeleo. Kama vile kulivyo na uwajibikaji wa pamoja wa kuzuia vita, kuwe pia na uwajibikaji wa pamoja wa kukuza maendeleo, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Rejea Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, 497-499. Ni katika muktadha huu, wa majanga makubwa yanayosababishwa na vita, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2022 amesema kila siku katika sakafu ya moyo wake, anaendelea kuwakumbuka watu wa Mungu nchini Ukraine wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Hivi karibuni zaidi ya watu 18 wamepoteza maisha kutokana na shambulio la kombora, katika Kituo cha biashara kwenye mji wa Kremenchuk, nchini Ukraine, tarehe 27 Juni 2022. Inakadiriwa kwamba, kituoni humo, kulikuwemo watu zaidi ya watu elfu moja, wakiendelea na shughuli mbalimbali za maisha wakati wa shambulio hilo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali bila kuchoka kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, apende kufungua malango ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Ukraine na Urussi katika ujumla wao. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwasaidia watu wa Mungu nchini Ukraine. Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki na upendo; ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu kuilinda na kuiendeleza. Amani ni tunda la upatanifu ulioundwa na Mwenyezi Mungu katika jamii ya mwanadamu. Vurugu, ghasia na mipasuko ya kijamii kamwe si jibu. Ulimwengu mamboleo unawahitaji manabii wa amani, wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya raia 21, 000 wamekwisha kupoteza maisha nchini Ukraine kutokana na vita inayoendelea kati yake na Urussi. Watu wanafariki dunia kwa kushambuliwa, kwa njaa na magonjwa pengine hata kwa kukosa huduma.

Majadiliano katika ukweli na haki  ni muhimu katika kudumisha amani duniani.
Majadiliano katika ukweli na haki ni muhimu katika kudumisha amani duniani.

Takwimu kwa upande wa Urussi zinabainisha kwamba askari zaidi 1, 351 wamekwisha kupoteza maisha na wengine zaidi 3, 825 wamejeruhiwa. Wachunguzi wa mambo wanasema, takwimu hizi zinaweza zisioneshe ukweli wa janga la vita kwa pande zote mbili. Kuna uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, linakadiria kwamba, kuna zaidi ya wakimbiizi na wahamiaji milioni 6.8 ambao wamelazimika kuikimbia Ukraine. Nalo Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, linasema kwamba kuna watu zaidi ya milioni 7.1 ambao hawana makazi ya kudumu nchini Ukraine hadi kufikia Mwezi Mei 2022. Vita hii inatishia hali ya usalama na uhakika wa chakula duniani pamoja na kuchochea mfumuko wa bei ya mazao ya chakula na nishati ya mafuta. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba zaidi ya watu bilioni 1.4 sehemu mbalimbali za dunia wanaweza kuathirika kutokana na uhaba wa nafaka pamoja na mbolea, ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa inazalishwa nchini Ukraine.

Vita Ukraine

 

 

30 June 2022, 14:59