Papa ameomba neema ya amani kati ya Urussi na Ukraine!
Angella Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko ameomba wanahija kuomba neema kwa ajili ya amani nchini Ukraine na Urusi na ili vita viishe na watu wa Ukraine wasiteseke tena. Na ndiyo wazo alilowasindikiza nalo kwa maombezi ya Mama yetu wa Loreto, kwa wanahija karibu elfu mbili walioshiriki hija hiyo iliyohitimishwa asubuhi ya Dominika tarehe 12 Juni 2022 katika Uwanja wa Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto. Papa Francisko alifanya hivyo kwa njia ya simu kwa washiriki hao wa Hija kutoka Macerata-Loreto nchini Italia kwa miguu, waliofanya kuanzia usiku wa Jumamosi kuamkia Dominika. Maneno ya Papa kwa Simu ni haya: “Mwombeni Mama yetu neema ya amani, tujifunze kuishi kwa amani, tuombe vita hivi viishe na watu wa Ukraine wasiteseke tena, ninawasindikiza kwa wazo hili na ombi hili kwa Mama yetu. Na pia tafadhali mniombee!
Kardinali Zuppi, upendo una nguvu zaidi ya ubaya
Katika hija ya 44, iliyoongozwa na mada: "Kwa Mungu kila kitu kinawezekana!”, imerudi katika uwepo wake mara baada ya miaka miwili ya janga la Uviko, hija ambayo iliwaona ushiriki wa watu wapatao elfu mbili hivi waliofika Loreto alfajiri sana baada ya kusafiri usiku kucha, takriban kilomita thelathini na kufika mahali Patakatifu.
Katika tukio hilo lililoanza usiku wa Jumamosi 11 Juni na sherehe ya Ekaristi, iliyoongozwa na Kardinali Matteo Zuppi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Bologna Italia na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Italia, ambaye alielezea jinsi gani hofu inataka kushawishi kwamba ni bora kukaa kimya, ikichochea kujifikiria sisi wenyewe bila wengine, ili kujiokoa wenyewe. Na kwa maana hiyo katika ushauri wake alisema kwamba kila kitu kinaweza kubadilika kwa sababu upendo una nguvu zaidi kuliko ubaya na unakuwa ujenzi wa ulimwengu huo wa Fratelli tutti yaani Wote ni Ndugu ambao ndiyo njia pekee ya kuzuia ulimwengu husiharibike.