Papa ameomba Jumuiya ya Kimataifa isiwasahau watu wa Myanmar
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika 19 Juni 2022 ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuchukua hatua kwa watu wa Myanmar ambao wanaendelea kukumbwa na ghasia na kufurushwa baada ya mapinduzi ya kijeshi tangu mnamo tarehe 1 Februari 2021.
Akizungumza mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Papa Francisko alisema kuwa anaungana na wito la maaskofu wa nchi hiyo pendwa inayoomba Jumuiya ya Kimataifa kutowasahau watu wa Birmania, bila kusahau utu wao wa kibinadamu na heshima kwa haki, maishani na pia kwa ajili ya mahali pa ibada, hospitali na shule.
Papa Francisko amebainishha “Hata hivyo tena tunasikia kilio cha uchungu cha watu wengi nchini Myanmar ambao bado wanakosa msaada wa lazima wa kibinadamu na ambao wanalazimika kuacha makazi yao kwa sababu, wanachomwa moto na kuepuka ghasia.”
Juma hili Maaskofu katoliki wa Myanmar walihitimisha Mkutano wao Mkuu kwa kutoa taarifa ya mwisho huku wakieleza wasi wasi wao mkubwa juu ya madhala ya raia wanaoendelea kubeba mzigo mkubwa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo.