Askofu Alain Clément Amiezi Jimbo la Odienné, Pwani ya Pembe
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Alain Clément Amiezi, wa Jimbo Katoliki la Bondoukou, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Odienné nchini Pwani ya Pembe “Ivory Coast”. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Alain Clément Amiezi, alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Kanisa kuu la “Santa Odilla.” Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Alain Clément Amiezi, wa Jimbo Katoliki Odienné, nchini Pwani ya Pembe alizaliwa tarehe 28 Septemba 1970 huko Dimbokro, Jimbo Katoliki la Bondoukou. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, Mei Mosi 1999 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, Kama Padre amewahi kuwa Paroko-usu, Mkurugenzi wa Miito na Idara ya Mawasiliano Jimbo. Kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2008 alitumwa na Jimbo kujiendeleza zaidi na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma.
Baada ya kurejea nchini mwake, alipewa dhamana ya kuwanoa Majandokasisi Seminari kuu ya Anyama katika kozi ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Alikuwa pia Jaalimu wa Chuo Kikuu cha UCAO: “Université Catholique de l’Afrique de l’Ouest (UCAO), Taasisi ya Taalimungu ya Shirika la Wayesuit, Abijan kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2021. Kuanzia mwaka 2011 alikuwa ni Katibu mtendaji Tume ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe. Tangu mwaka 2021 hadi kuteuliwa kwake tarehe 30 Juni 2022 na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Odiennè, alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Kanisa kuu la “Santa Odilla.”