Tafuta

Papa Francisko anasema kila mwamini ni mdau katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kila Mkristo daima ni mfuasi mmisionari. Papa Francisko anasema kila mwamini ni mdau katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kila Mkristo daima ni mfuasi mmisionari.  

Ujumbe wa Papa Francisko Siku ya 59 ya Kuombea Miito: Askofu Mkuu Mstaafu Lebulu Atia Neno

Daraja Takatifu ya Upadre watambue kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya neema na huruma ya Mungu. Watawa wajisikie kwamba, wao ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu na unabii kwa ubinadamu mpya. Wito wa ndoa iwe ni majitoleo kwa wenza wa ndoa; wao ni wazazi na walezi wa Injili ya maisha. Kila wito ndani ya Kanisa ni kwa ajili ya huduma na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 anawaalika waamini kutafakari kwa pamoja maana pana ya “wito” ndani ya muktadha wa Kanisa la Kisinodi, Kanisa linalomsikiliza Mwenyezi Mungu na Ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kukuza moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu kutembea kwa pamoja kama kielelezo cha Kanisa la Kisinodi kwa kutambua kwamba, kila mwamini ni mdau katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kila Mkristo daima ni mfuasi mmisionari. Wakristo wanaitwa kusimama kidete kuwalinda ndugu zao na mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kuutazama Uso wa Mwenyezi Mungu anayewaita kuwa watakatifu, kwa kutambua kwamba, utakatifu ni wito kwa watu wote unaowawezesha kutumia karama na fursa mbalimbali wanazowezeshwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Daraja Takatifu ya Upadre ni chombo cha neema na huruma ya Mungu
Daraja Takatifu ya Upadre ni chombo cha neema na huruma ya Mungu

Mchakato wa utakatifu wa maisha unanogeshwa kwa: Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Sala inayomwilishwa katika huduma makini, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaitikia wito wa upendo wa Mungu na hivyo kugundua uwezo na mapungufu yao katika maisha. Kwa wale wanaojisikia kuitwa katika Daraja Takatifu ya Upadre watambue kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya neema na huruma ya Mungu. Watawa wajisikie kutoka katika undani wao kwamba, wao kweli ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu na unabii kwa ubinadamu mpya. Wito wa ndoa ambao ni msingi wa miito yote mitakatifu ndani ya Kanisa, iwe ni sadaka na majitoleo kwa wenza wa ndoa, kwa kutambua kwamba, wamepewa dhamana ya kuwa ni wazazi na walezi wa Injili ya maisha. Kila wito ndani ya Kanisa anasema Baba Mtakatifu ni fursa ya huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni nafasi ya kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo adili na matakatifu.

Watawa ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu na unabii wa ubinadamu mpya
Watawa ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu na unabii wa ubinadamu mpya

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, katika ujumla wao wanaitwa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu ulimwenguni; kwa kuzingatia umoja na utofauti wao unaojenga Fumbo la Kanisa. Ni katika muktadha huu, Kanisa lazima liwe ni la Kisinodi, ili kukuza na kudumisha moyo wa: kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili hatimaye, kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Kila wito hauna budi kupania kutekeleza ndoto ya Mungu kwa binadamu, yaani ujenzi wa udugu wa kibinadamu uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu, katika Sala yake ya Kikuhani kwa kusema “Wote wawe na umoja” Yn 17:21. Lengo ni kuwawezesha watu wote wa Mungu kufanya kazi katika ushirika, ili hatimaye, familia kubwa ya Mungu iweze kushuhudia ushirika katika upendo, kielelezo cha upendo uliompelekea hata Mwenyezi Mungu akamuumba mwanadamu!

Familia ni msingi na chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa
Familia ni msingi na chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa

Wakati huo huo, Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha Tanzania, katika maadhimisho ya Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya Kuombea Miito Mtakatifu ndani ya Kanisa, anawakumbusha waamini kwamba, Ukristo ni zawadi na wito maalum kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko wa kujivunia wito hui unaowataka kufikiri na kutenda; kupenda na kuchukia; kuzungumza na kuhusiana na wengine kama Kristo Yesu alivyofanya katika maisha na utume wake. Kumbe, Wakristo wanapaswa kuhakikisha kwamba, maisha na mtendo yao yote yanafanana na yale ya Kristo Yesu. Katika wito wa kuwa Wakristo, kuna baadhi yao, Mwenyezi Mungu amewachagua ili waweze kufikiri na kutenda; wahisi na kunena kama Kristo Yesu; yaani wawe ni: Mkuhani, Manabii na Wafalme. Katika wito huu wa jumla, kuna waamini walei ambao wanaitwa kuunda familia kama Kanisa dogo la nyumbani, msingi na nguzo thabiti ya miito yote mitakatifu ndani ya Kanisa. Kuna baadhi yao, Mwenyezi Mungu amependa kuwachagua kuwa Mapadre na Watawa. Wote hawa anasema, Baba Mtakatifu Francisko wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kama sehemu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Askofu mkuu Lebulu Miito
07 Mei 2022, 13:31