Tafuta

Papa,Scholas Occurrentes:wokovu wa sayari kutoka shairi&ujasiri wa wanawake

Alasiri,tarehe 19 Mei 2022,Baba Mtakatifu alikutana na Jumuiya ya Kielimu kimataifa iliyoanzishwa hivi karibuni kama harakati ya waamini wenye tabia ya kimataifa.Kutoka Ukumbi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana cha Roma,Baba Mtakatifu ametoa somo la uzinduzi wa 'Shule ya Laudato Si' inayowashirikisha vijana kutoka nchi mbali mbali zinazohusika na huduma ya nyumba ya wote.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika hali ya sherehe, iliyohuishwa na nyimbo na ngoma za vijana washiriki,  uzinduzi wa Shule ya Laudato Si’ inayoongozwa na Papa Francisko, imefanyika alasiri  tarehe 19 Mei 2022 katika Ukumbi Mkuu  wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha  Urbaniana, Roma. Mkutano huo ulishuhudia ushiriki wa watu mashuhuri wa sanaa, muziki, michezo na teknolojia, lakini pia wawakilishi wa asasi za kiraia kutoka nchi mbali mbali za ulimwengu ambamo Scholas Occurentes inafanya kazi, na ilikuwa mazingira ya kudhibitisha hali mpya ya kisheria ya chombo hicho,  ambacho hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko  alikabidhi sifa na kukijumuisha na waamini wenye tabia ya kimataifa.

Scholas Occurrentes ilianzishwa kama chama cha kimataifa cha waamini

Mkutano huo ulihudhuriwa na takriban wanafunzi 50 kutoka Argentina, Bolivia, Brazil, Chile, Colombia, Hispania, Haiti, Italia, Mexico, Panama, Paraguay, Ureno na Mexico. Kwa mwaka mzima, vijana hawa watajishughulisha na kazi ya uumbaji na wataendeleza mipango  yenye athari za kijamii na kimazingira katika jamii zao. Baada ya kuorodhesha changamoto zinazopaswa kukabiliwa leo hii, vijana hao walimwambia Papa kwamba kundi hili litakwenda katika mabara mawili kutangaza Habari Njema na kusema kwamba ni lazima watunze nyumba yetu ya pamoja. Na, kushukuru Scholas kwa kuwapa zana muhimu kwa kazi hii, ya kujitolea kutunza kazi ya uumbaji na kutangaza utunzaji wa Nyumba ya Pamoja.

Nguvu ya wanawake ya kubadilisha ulimwengu

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na kiongozi wa bendi maarufu ya U2 ya Ireland, Bono Vox, aliyekuwa zamani anaitwa Paul David Hewson, ambaye aliwashukuru waandaaji kwa uzoefu huu wa kushiriki katika Shule ya Laudato Si ', kwa kuhamasisha  utamaduni wa kukutana na kwa hilo, kuhamasisha Scholas Occurrentes kama Harakati za Kielimu za Kimataifa. Akizungumzia juu ya upekee wa kuwa mwanamke, Bono alimuuliza Papa Francisko kama uwezo maalum walio nao wanawake katika kubadilisha ulimwengu pia ni aina ya nguvu kuu inayofaa kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya sayari. Baba Mtakatifu alijibu, akisema kwamba “kwa ujumla tunaelekea kuzungumza juu ya dunia mama, si ya baba duniani”. Zaidi ya hayo, Papa alisisitiza kwamba “wanawake wana kipawa cha asili cha kujua jinsi gani ya kubadili mambo” na akirejea sura za kwanza za kitabu cha Mwanzo, alithibitisha kwamba “tangu siku hiyo ya tunda, wao ni wahusika wakuu”.

Papa na Scholas Occurrentes
Papa na Scholas Occurrentes

Mmoja wa washiriki vijana, aitwaye Irene, alimuuliza Papa kwa nini alichagua Scholas kupeleka mbele  Laudato Si 'ulimwenguni. Papa Francisko alieleza kwamba “mashairi na ujasiri vinahitajika ili kufanya waraka huo ujulikane”. Na kwamba “maisha katika mashairi hayajifunzi kutoka katika vitabu, lakini kwa kazi, kwa kutafakari asili”. Na, akirejea katika tafakari yake juu ya wanawake, Baba Mtakatifu alisema kwamba “wanawake wana wito wa kutoa maisha yao. Ni kuhusu kuishi na ulinzi wa asili ni mapambano ya maelewano na wanawake katika jambo hili wanafahamu zaidi”. Kwa hilo Schola Occurrentes wana uwezo wa kutunga mashairi na mabadiliko. Mkutano huo uliendelea na uwasilishaji wa mipango mbalimbali ambayo Scholas Occurrentes inaendeleza katika sehemu mbalimbali za dunia, ambapo watu mashuhuri kutoka ulimwengu wa sanaa, michezo na teknolojia wanahusika, pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia.

Papa na Scholas Occurrentes
Papa na Scholas Occurrentes

Tarehe 17 Mei 2022, Ofisi ya Wanahabari Vatican ilitoa maandishi ya Papa Francisko, iliyotiwa saini kwenye Maadhimisho ya Mtakatifu Joseph tarehe 19 Machi 2022, na kuanzisha Scholas  Occurentese kama “chama cha faragha cha waamini chenye  tabia ya kimataifa. Kwa kuzingatia kwamba, Msingi wa Kipapa unaendelea leo kupanua shughuli zake za upendo na kujiunda kama  jumuiya na harakati ya elimu ya watu wa kimataifa, inahitaji muundo mpya wa kisheria kulingana na ukweli huu mpya”(Rej. katika maandishi ya mkono Papa kuhusu Scholas Occurrentes,Mei 17, 2022).

Papa na Scholas Occurrentes
Papa na Scholas Occurrentes

Katika maandishi ya kkono wake ya Papa anakumbusha kwamba "Scholas Occurrentes ina mizizi yake katika:'Shule ya Mtaani na Shule za Dada zilizoendelezwa kwenye mitaa ya miji ya  Buenos Aires, kwa mpango wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa wakati huo, Kadinali Jorge Mario Bergoglio (yaani Papa Francisko), na inakua kila wakati, kwa kuwa leo ni mtandao mkubwa wa kimataifa wa shule, zinazoshirikishana mali zao, zenye malengo ya pamoja, kwa kuzingatia hasa wale walio na rasilimali chache.

PAPA FRANCISKO NA HARAKATI YA SCHOLAS OCCURRENTES
20 May 2022, 10:52