Tafuta

2022.05.18 Ujumbe wa Papa kwa Katholikentag 2022.05.18 Ujumbe wa Papa kwa Katholikentag 

Papa kwa Katholikentag:Kutoa na kujitolea kunawezekana kila wakati

Ujumbe wa Papa Fransisko kwa tukio la Tamasha la Imani Katoliki linaloendelea huko Stuttgart hadi Mei 29: “Hata katika machafuko ya sasa,tunamshukuru Mungu,tunaweza kuona jinsi nia ya wengi ya kujitolea kwa ajili ya wengine pia ni kubwa”.Kutoa na kujitolea kunawezekana kila wakati.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alioandika katika fursa ya toleo la 102 la Siku za Wakatoliki, linalofanyika  mjini Stuttgart wa Ujerumani kuanzia tarehe 25 hadi 29 Mei 2022 na kujikita katika mada kuu: “Kushirikishana maisha” amejikita kuweza kuwa:  “Kwa mawazo yetu tuko karibu na watu wa Ukraine na tunawaombea wanadamu wote, ambao maisha yao yanatishiwa na kuwekewa masharti, kwa wale wote wanaotamani utimilifu wa maisha ambao Bwana pekee anaweza kuwapa. Tunaomba amani yake”.

Tamasha katoliki huko Ujerumani
Tamasha katoliki huko Ujerumani

Papa Francisko amesema inawezekana kutoa uhai, kwa namna nyingi: “Ninafikiria, kwa mfano, juu ya akina mama au baba ambao wamejitolea kabisa kwa watoto wao, watu wengi ambao katika huduma ya kikanisa au katika taaluma za kijamii au za kihisani huweka maisha yao mahali pa mwisho kutumikia na kusaidia wengine. Hata katika matatizo ya sasa, tukimshukuru Mungu, tunaweza kuona jinsi wengi wanavyojitoa sadaka kwa ajili ya wengine pia. Hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Sote tumekaa kwenye mashua moja. Kwa sababu hiyo ni muhimu tujenge ufahamu kwamba sisi sote ni watoto wa Baba mmoja, kaka na dada; kwamba sisi sote tunaishi katika nyumba moja, ambayo imekabidhiwa sisi sote pamoja; kwamba kitu kimoja kinaishi kwa kingine na kwamba hatuwezi kujizuia kushiriki maisha yetu. Pamoja tu tunasonga mbele”.

Kila mtu hakosi cha kutoa

Katika ujumbe wake, Papa Francisko, akikumbuka sura ya Mtakatifu Martin aliyemkatia maskini  joho lake, amesema anatuhimiza kufuata mafundisho yake: “Wale wote wanaobeba jina la Yesu Kristo wameitwa kufuata na kushiriki katika njia zetu na uwezekano wetu. Je ni watu wangapi wanahitaji msaada. Tuko makini tunapopitia maisha yetu na tutaona hivi pale tunapohitajika”. Hata watu maskini zaidi, wana kitu ambacho wanaweza kuwapatie wengine. Vile vule ni ukweli kwamba “Kila mtu, hata tajiri zaidi  anapungukiwa na anahitaji karama za watu wengine. Kukubali kitu kutoka kwa wengine wakati mwingine ni ngumu zaidi kuliko kutoa kitu, kwani hii inamaanisha kukiri kutokamilika kwa mtu mwenyewe. Petro alilazimika kujifunza kutokana na shida kukubali utumishi wa Bwana wake wakati wa kumuosha miguu. Sisi pia tunaomba unyenyekevu ili kuweza kukubali kitu kutoka kwa wengine”.

26 May 2022, 16:29